Wahanga sita wa mkasa wa moto Kandara wazikwa katika kaburi moja kubwa
NA MWANGI MUIRURI
WAHANGA sita wa familia moja walioangamia katika mkasa wa moto Kaunti ya Murang’a mnamo Aprili 10 walizikwa Jumatano katika hafla iliyojaa majonzi.
Bi Mary Wangui, 60, mabinti wake watatu ambao ni Cecilia Gathoni, 30, Lucy Mumbi, 18, Margaret Wanja 15 sambamba na wajukuu wake wawili ambao ni Jackline Wambui, 7, na Alvin Kiarie aliyekuwa na umri wa miaka mitatu walizikwa katika kijiji cha Gatitu katika kaburi moja kubwa.
Bw George Kung’u ambaye ni msemaji wa familia hiyo alisema kuwa washakubali msiba huo kwa kuwa hauwezi ukabatilishwa, akisema kuwa neema za Maulana na maombi ya walio na nia njema ndio nguzo kuu ambayo imewapa wote katika familia hiyo uwezo wa kustahimili.
“Ni msiba uliotushtua katika familia hii yetu ambayo ni pana kwa kuwa babangu marehemu John Njoroge alikuwa na mabibi wawili na tukazaliwa tukiwa watoto 20. Lakini hayo yote ni tisa, la kumi ni kwamba tumejifunza mengi kutokana na mkasa huu na tunazidi kumtegemea Mungu atupanguze machozi, huku tukiombea roho za waathiriwa zipate utulivu wa milele katika dunia ya kuzimu,” akasema.
Mkasa huo ulitangazwa na maafisa wa polisi kuwa wa jinai ambapo mwendo wa saa saba usiku chumba walimokuwa wamelala wahanga hao kilifungwa kutoka nje kwa kufuli na kisha kikamiminiwa petroli na hatimaye kupigwa kiberiti.
Ndani ya nyumba hiyo ya mkasa kwa wakati huo wa moto kuzuka kulikuwa pia na dadake Bi Wangui ambaye ni Bi Alice Nyambura wa miaka 36 akiwa na watoto wake wawili wa kike.
Jinsi Bi Wangui aliponyoka mauti hayo akiwa na mabinti hao wake wawili na kisha ikabainika kuwa alikuwa ameondoa nguo zao kutoka nyumba hiyo kabla ya moto kuzuka kuliishia kumweka katika shaka ya wapelelezi na akatiwa mbaroni kama mshukiwa mkuu.
Chumbani mwake kulipatikana kibuyu cha petroli na pia mishale ya kiberiti iliyokuwa imetumika. Wapelelezi walimwasilisha katika mahakama ya Kandara mnamo Aprili 11 na wakaomba muda wa siku 21 za kumzuilia uchunguzi ukiendelea na ambapo atarejeshwa mahakamani Mei 3 ili kesi yake itajwe mbele ya hakimu Eric Mutunga wa mahakama ya Kandara.
Ripoti ya upasuaji wa miili hiyo sita iliyoandaliwa na daktari mkuu wa serikali Johansen Oduor ilibaini kuwa wote waliaga dunia wakiwa wamekumbatiana na majeraha ya moto mwilini yalikuwa ya kiwango cha asilimia 100 kwa kila mhanga.
Katika mazishi hayo, hisia za maombolezo zilitanda huku minong’ono ikiwa kwamba familia hiyo imekuwa ikikumbwa na migogoro ya ugavi wa mali ya mwendazake Bw Njoroge aliyeaga dunia mwaka wa 2000.
Pia, bibi yake wa kwanza Bi Alice Wagikuyu aliaga dunia mwaka wa 2008 alipogongwa na ng’ombe wake aliyekuwa akimpa maji. Kwa sasa, Bi Rebecca Wambui ndiye amebaki kati ya mabibi hao wawili lakini kufuatia migogoro ya kifamilia, wote wakinga’ng’ania mali inayokisiwa kuwa ya thamani ya Sh2.3 Bilioni, alihama nyumba ya mumewe na kuwaacha mabinti wake wawili (Bi Wangui na Bi Nyambura) wakivurugana katika hali iliyoishia mkasa huo wa moto.
Viongozi kadhaa wa Kaunti waliofika katika hafla hiyo ya mazishi waliomba serikali itekeleze uchunguzi wa kina na waliohusika katika mkasa huo waadhibiwe kwa mujibu wa sheria.
Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Bw Karuku Ngumo aliwataka wenyeji wasiwe wa kuvuragana katika tamaa ya urithi wa mali, mbali wawe wakijadiliana kama mandugu na wanapoona wanalemewa kusikizana, wawe wakisaka huduma za maridhiano na pia za kisheria.
“Ninasikitika sana kuona majonzi ya kiwango hiki katika maisha ya familia moja. Si haki kamwe. Serikali itatekeleza haki kwa waathiriwa lakini cha msingi ni kwamba, migogoro yoyote haifai kuishia katika maamuzi ya kikatili,” akasema.