Forest Road: Wahudumu wa bodaboda kujua hatima yao Machi 28
NA RICHARD MUNGUTI
WAHUDUMU 17 wa bodaboda wanaodaiwa walmnyang’anya kimabavu afisa wa Ubalozi wa Zimbabwe simu iliyo na thamani ya Sh130,000 na kumdhulumu kijinsia watajua hatma yao Machi 28, 2022 ikiwa watashtakiwa au la.
Mahakimu Robinson Ondieki na Gilbert Shikwe waliagiza washukiwa hao wazuiliwe kwa siku tatu zaidi kuwezesha afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma kusoma na kutoa mwelekeo ikiwa washukiwa hao wataachiliwa au la.
Mabw Ondieki na Shikwe walielezwa na afisa anayechunguza kesi hiyo Inspekta Lyvonne Mwanzia kwamba amekamilisha mahojiano.
“Nimekamilisha mahojiano na kuandika taarifa za mashahidi. Nimepeleka faili kwa afisi ya DPP ushauri utolewe ikiwa watashtakiwa au wataachiliwa,” alisema Inspekta Mwanzia.
Afisa huyo aliomba afisi ya DPP ipewe siku tano kukamilisha zoezi hilo.
Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na washukiwa hao wakisema, “wamekuwa rumande kwa siku 15 na walitazamia uamuzi wa kuwashtaki umetolewa ndipo wajue hatma yao.”
Kila mmoja wa washukiwa hao alipinga kuzuiliwa kwa siku nyingine tano wakidai wameumia.
“Mheshimiwa tumeumia sana. Kule rumande kuna shida. Twataka tushtakiwe ama tuachiliwe tukajipange. Sisi ndio tunategemewa na familia zetu,” washukiwa hao waliwasihi mahakimu hao wapunguze muda wao wa kukaa rumande.
Bw Shikwe aliyesikiliza ombi la washukiwa hao 16 alisema afisi ya DPP yahitaji muda kusoma na kutoa mwelekeo wa mashtaka watakayofunguliwa.
“Naipa afisi ya DPP siku mbili kukamilisha kusoma na kutoa ushauri kuhusu kesi hii,” alisema Bw Shikwe.
Bw Ondieki aliyesikiliza ombi kumhusu mshukiwa mkuu Zachariah Nyaore Obadiah aliyekamatwa akijaribu kuvuka mpaka kuenda Tanzania alisema atamwachilia kwa dhamana endapo afisi ya DPP haitawasilisha mashtaka kufikia Machi 28, 2022.
Afisa huyo wa Ubalozi anawakilishwa na wakili mwenye tajriba ya juu Philip Murgor.
Bw Murgor hakupinga afisi ya DPP ikipewa muda zaidi kusoma na kutoa mwelekeo.
Wahudumu hao walikamatwa kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta kwamba msako mkali ufanywe kwa wahudumu wa bodaboda kote nchini.
Pia Rais Kenyatta alilaani kitendo cha kuporwa na kudhulumiwa kwa afisa huyo wa ubalozi wa Zimbabwe nchini Kenya mnamo Machi 4, 2022.
Washukiwa waliofikishwa kortini ni James Mutinda Muema, Samuel Wafula, Muswahili, Charles Omondi Were, Obano, Hassan Farah Forah, Wanjuki Lincoln Kinyanjui, Mbugu, Fundi, Maina, Ngure, Shitekha, Martin Kamau Maina, Shadrack Ambia Luyeku, Shadrack Kioko Nyamai,Cliff Gikobi Oyaro na Joseph Kibui Mukambi.
Washukiwa hao walirudishwa kuzuiliiwa katika kituo cha polisi cha Gigiri.