Wahudumu wa teksi mjini Thika watoa malalamishi ya kupokea malipo duni, uhalifu
NA LAWRENCE ONGARO
CHAMA cha wahudumu wa teksi cha Thika Online Cub Association, kinataka maslahi ya wanachama yaangaziwe upya.
Mwenyekiti wao Samuel Kariuki alisema kulingana na jinsi wanavyoendesha shughuli zao kupitia mitandao kwa kupata wateja wao, wametathmini na kugundua wanapoteza pakubwa.
Kwa mfano walisema iwapo mteja atamuita dereva kupitia programu ya simu, wanaelewana bei lakini baadaye mteja anakuwa mgumu wa kutoa pesa mwisho wa safari.
Wahudumu hao wanasema ya kwamba mahali ambapo pengine dereva alistahili kulipwa Sh500, analipwa Sh130 pekee.
“Sisi kama wahudumu wa magari ya teksi tunajipata katika njia panda kwa sababu hata stakabadhi zetu za magari – Log books – zimehifadhiwa kwenye benki, ili tuwe na nafasi ya kupata mikopo wakati tunapohitaji,” alifafanua Bw Kariuki.
Alisema baada ya bei ya petroli kupanda, kazi hiyo ya teksi imekuwa ngumu ajabu kwa sababu “hatupati pesa kamili tunayostahili na kwa hivyo tumebaki katika njia panda.”
Alisema wangetaka wateja wao wajaribu kuelewa masaibu wanayopitia kutokana na malipo ya safari kwa sababu pia wao wanaolipa madeni mengi ya magari hayo.
Bw Sammy Macharia, alisema biashara ya teksi imekuwa na changamoto tele kwani mara nyingi hata yeye mwenyewe hufutilia mbali makubaliano na mteja wake.
“Iwapo sielewani na mteja kuhusu bei kamili ninalazimika kufutilia mbali na kutafuta mteja mwingine,” alifafanua Bw Macharia.
Alihimiza wateja wao kuelewa kuwa kazi hiyo ni ya changamoto tele kwa hivyo ni vyema kulipa ada inayostahili bila kumkandamiza mwenye teksi.
Pia Macharia alisema ya kwamba mwenzao mmoja alivamiwa na wahuni alipokuwa akiwapeleka eneo la Kisii, Thika. Hao wahalifu walijifanya wateja.
Alisema ni vyema pia kuwa makini kujua hasa ni mteja yupi unayembeba kabla ya kuelewana.
Anthony Mugo ambaye amefanya kazi hiyo kwa miaka saba anaitaka serikali kuingilia kati kuona ya kwamba hawapunjwi kutokana na pesa wanazopokea ambazo haziambatani na huduma wanazotoa kwa wateja wao.
Alipendekeza kwa serikali kupitisha sheria maalum itakayowakinga wahudumu hao.
Next article
‘Jungle’ Wainaina ateuliwa kinara wa IPLF…