Wakazi mjini Moi’s Bridge sasa wapumua
Na HASSAN MUCHAI
ENDAPO matukio ya hapo awali kuhusu kuzorota kwa hali ya usalama katika mji wa Moi’s Bridge yasingezingatiwa kwa kina, basi huenda utulivu ambao umekuwa ukishuhudiwa kwa sasa ungekuwa ndoto kwa wakazi wake.
Kwa mujibu wa wakazi wa mji huo ulioko baina ya kaunti tatu za Trans Nzoia, Uasin Gishu na Kakamega, hali ya usalama ilikuwa mbaya sana baada ya kuripotiwa kwa mauaji ya watoto tangu mwaka juzi. Mauaji ya watoto hawa yalifikia kilele mnamo Juni 15, 2021 baada ya mwili wa mtoto Linda Jerono aliyeripotiwa kupotea siku tano zilizokuwa zimepita kupatikana kichakani karibu na makao ya Halmashauri ya Nafaka na Mazao (NCPB) ukiwa na majeraha.
Tayari mshukiwa mkuu Evans Wanjala aliyekuwa akifanya kazi ya uashi mjini humo, alikamatwa na kufichua habari ambazo zimekuwa zikiwasaidia wapelelezi wa jinai kufanya uchunguzi wao wa kina.Kabla ya visa hivyo vya mauaji kuanza kushuhudiwa katika mji wa Moi’s Bridge, eneo hili lilikuwa bustani ya amani na kitovu cha uwekezaji kwa wafanyabiashara wa jumla, rejareja na hata wachuuzi.
Uwekezaji huu umevutia wawekezaji kutoka sekta za benki, bima, ujasiriamali, wajenzi wa mitaa ya makao, mashirika yasiyo ya kiserikali, shule za kibnafsi na hata vituo vya matibabu.
Ghadhabu
Kilichowatia shaka na ghababu wakazi wa mji huo ni kuwa, ilichukua muda mrefu kwa idara husika serikalini kuwasaka wahalifu hao licha ya visa kama hivyo kuongezeka na kuripotiwa kila uchao.Ingawa wizi wa kawaida ulikua jambo la kawaida na wakazi kuiishi kwa hofu ya mashambulio wakati wowote, sasa hali imetulia na wakazi wanaishi bila hofu.
Mashamba makubwa ya mahindi na miti yalikuwa maficho mazuri kwa wahalifu hawa na wengi kukimbilia maeneo ya mbali na mji huo bila kujulikana.Kinachotia hofu zaidi ni kuwa, uhalifu unapotokea huwa ni vigumu sana kuwajua watekelezaji. Hii ni kwa sababu mji wa Moi’s Bridge uko katikati mwa tawala tatu;
Uasin Gishu, Trans Nzoia na Kakamega. Kwa sababu hiyo, maafisa wa usalama hukumbana na wakati mgumu kuwasaka wahalifu.Mji wa Moi’s Bridge umezungukwa na barabara nzuri. Kuna barabara mbili muhimu. Ile inayopitia ngome ya jeshi ya Moi, Nangili, Matunda hadi Kitale.
Nyingine ni ile inayozunguka eneo la nyuma kupitia chuo kikuu cha Moi, Ziwa, Moiben, Twiga Farm hadi Moi’s bridge. Barabara hizi mbili ni muhimu sana kwa uchukuzi wa abiria na usafirishaji wa mazao ya kilimo. Wahalifu wanapotekeleza uhalifu wao, hufaulu kuponyoka kwa haraka na kufanya kazi ya maafisa wa usalama kuwa ngumu kuwanasa.
Historia ya mji wa Moi’s Bridge ilianza nyakati za utawala wa kikoloni wakati daraja linalounganisha kaunti hizo tatu lilipokuwa likijulikana kama Hoey’s Bridge kutokana na mjenzi wake wa kwanza Cecil Hoey. Baadaye jina hilo lilibadilishwa na kuwa Moi’s Bridge kwa heshima ya aliyekuwa Rais wa pili wa Jamhuri ya Kenya hayati mzee Moi.
Eneo hili lina mandhari ya kupendeza na hali nzuri ya hewa, udongo mzuri uliojaa rotuba, maji ya kutosha na misitu mikubwa. Shughuli za kilimo cha mahindi, ngano, alizeti , maharagwe na hata ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyama pamoja na mifugo wengine zilinawiri na kuwapa mtaji mkubwa Wazungu na wakulima wengine.
Baadhi ya maduka ya mwanzo kufunguliwa hapa ni lile lililokuwa likimilikiwa na mhindi mmoja kwa jina Bismillahi na jingine kwa jina Sabugo Wholesalers. Mengine yaliyofuata ni Pakawa, Wa- Mumbi Supermarket, Variety Hadrware, Henna Hardware and Electricals na kadhalika.
Baada ya Wazungu kuondoka, kupitia usaidizi wa serikali, kuliibuka makundi makubwa ya ununuzi wa mashamba yaliyovamia kaunti za Trans Nzoia, Uasin Gishu na Kakakemga na kuwasaidia wanachama kujipatia vipande vya ardhi kwa bei nafuu.
Serikali ilianzisha taasisi za utoaji mafunzo ya kilimo kwa wakulima – Waafrika – na ikatenga ekari nyingi za ardhi kwa shughuli hiyo. Mfano mzuri ni shamba la Jabali ambalo lilikuwa kituo kikubwa cha mafunzo ya kilimo cha mifugo na upanzi wa mahindi, ngano na miti.
Cha kushangaza ni kuwa, kituo hicho kimesalia kaburi la sahau baada ya wanyakuzi kutwaa ardhi yake.Kubomolewa kwa majengo ya mabanda ya Kambisuswa iliyokuwa katika ardhi iliyotengewa halmashauri ya nafaka na mazao miaka kadhaa iliyopita, kuliupa mji huu sura mpya na kutoa nafasi mwafaka kwa utekelezaji wa shughuli za biashara.
Kambisuswa ilikuwa makao fiche ya uuzaji wa pombe haramu, maasi ya kijamii na hata uhalifu. Makazi haya yalikuwa duni sana hivi kwamba wakazi wengi tulioongea nao walifurahia kubomolewa kwake kwani yalichochea kuzorota kwa maadili katika mji wa Moi’s Bridge na viunga vyake.
Tangu kubomolewa kwa Kambisuswa, upikaji wa pombe haramu katika mashamba ya Mukunga, Chebarus, Karara, Moiben, Nzoia Scheme, Kapkoi na hata Jabali umepungua kwa kiasi kikubwa na wasafirishaji wake waliokuwa wakijulikana kama ‘kanderere’ kutokomea kabisa.
Kwa sasa, mji wa Moi’s Bridge umerejesha utulivu wake na wakazi wana imani kuwa visa vya ubakaji na mauaji ya watu ambavyo vimekua vikishuhudiwa vitaisha. Hata hivyo, hili litategemea sana uwajibikaji wa maafisa wa usalama ambao walilaumiwa sana na wakazi na kusababisha maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa mjini humo baada ya mauaji ya mtoto Jerono.
Mmoja wa wakazi, Bw John Kiptoo anatoa wito kwa serikali za kaunti za Uasin Gishu na Kakamega ambapo mji huo upo, zishughulikie kwa haraka mahitaji ya kimsingi ya wenyeji. Baadhi ya mahitaji hayo ni barabara zinazoingia mitaani, mabomba ya kupitisha maji taka, taa za barabarani na zile za usalama. Pia wakazi wanataka vituo vya kisasa vya masoko na maji safi.
Ushuru
“Haina maana kwa serikali zetu za kaunti kuendelea kutoza ada na malipo mengine bila kuzingatia suala la maendeleo. Tunataka soko la kisasa la wachuuzi, uwepo wa maji safi, mabomba ya kupitisha maji taka, taa za usalama na zile za barabarani, kuimarishwa kwa barabara zinazoingia mitaani na kadhalika,” anasema mkazi huyu.Hata hivyo, mgalla muue na haki yake umpe, Gavana wa Uasin Gishu anayeondoka Jackson Mandago amesifiwa kutokana na kazi yake kuimarisha sura ya Moi’s Bridge.