Wakenya wana imani na mfumo wa CBC – Ripoti
NA JURGEN NAMBEKA
IDADI kubwa ya Wakenya wanapendelea mtaala mpya wa elimu ya umilisi na utendaji (CBC) licha ya kupingwa na mrengo wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu wa Rais William Ruto.
Utafiti wa kura ya maoni uliofanywa na Idara ya Masomo ya Maendeleo (IDS) ya Chuo Kikuu cha Nairobi na kampuni ya Afro Barometer, unaonyesha asilimia 65 ya Wakenya wanahisi kuwa mtaala wa CBC utaboresha kiwango cha elimu nchini.
“CBC imekumbwa na changamoto sana ukiwa ni mfumo mpya ambao haujawahi kutumika nchini. Ni miaka mitano tangu mfumo huu uanzishwe na utafiti wetu un – aonyesha Wakenya wengi wanapenda CBC.
“Hatujafika tunakotaka ila tunaendelea vyema kama nchi,” akasema Dkt Laura Barasa, mtafiti wa Afro Barometer na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Theluthi moja ya Wakenya hawaamini kuwa CBC itaimarisha kiwango cha elimu nchini huku asilimia tisa wakisema hawana hakika ikiwa mfumo huo utaleta manufaa yoyote kwa wanafunzi, kwa mujibu wa ripoti ya utafiti.
Mtaala wa CBC ulioanzishwa 2017, unatarajia watoto kusoma kwa miaka miwili chekechea kabla ya kujiunga na shule za msingi ambapo wanasoma kwa miaka sita.
Baada ya kukamilisha elimu msingi, wanafunzi wanajiunga na sekondari ya chini kwa miaka miwili na sekondari ya juu kabla ya kujiunga na elimu ya chuo kikuu ambapo wanasoma kwa miaka mitatu.
Mkurugenzi msaidizi wa IDS, Prof Winnie Mitullah, aliwataka Wakenya na taasisi mbalimbali, vikiwemo vyombo vya habari na vyuo vikuu, kuchukulia kwa uzito matokeo ya utafiti huo.
Muungano wa Kenya Kwanza chi – ni ya Dkt Ruto, kinara wa ANC Musalia Mudavadi na Moses Wetangula wa Ford Kenya, mwezi uliopita, walisema watafutilia mbali mfumo wa CBC iwapo watashinda urais Agosti 9. Wakenya 2,400 kutoka kote nchini walihusishwa kwenye utafiti huo uliofany – wa kati ya Novemba 12 na 30, mwaka jana.