KINYUA BIN KING’ORI: Wakenya waongozwe na sifa bora za Kibaki kuchagua viongozi wao Agosti 9
NA KINYUA BIN KING’ORI
KENYA na ulimwengu kwa ujumla tunaendelea kuomboleza Rais mstaafu Mwai Kibaki aliyeaga dunia wiki jana, mipango ya mazishi yake imekamilika na atazikwa Jumamosi nyumbani kwake Othaya, Kaunti ya Nyeri.
Historia ya taifa hili, ikiandikwa jina la marehemu Kibaki litabakia katika dibaji kuelezea mchango wake mkubwa kama mwanauchumi aliyechangia uchumi wetu kuimarika akiwa Rais.
Aidha, alifufua miradi iliyokwama na kuanzisha mingine mingi ikiwemo kuboresha miundomsingi na sekta ya elimu katika kipindi chake cha miaka 10 akiwa rais.
Juhudi zake daima zilikuwa kuhakikisha wananchi wamepata mafanikio, haki ya elimu, uhuru wa kisiasa, uhuru wa kupata habari muhimu kutoka kwa serikali na kadhalika.
Ufanisi wake ndio uliohakikisha Kenya imepata matumaini ya kupigana na maradhi ya ujinga kabisa kwa kuleta elimu ya bure ambapo watoto wa maskini na matajiri waliweza kupata elimu kwa usawa bila usumbufu wa karo hasa katika elimu ya msingi.
Tusisahau pia ni katika uongozi wa Kibaki ambapo Wakenya walipitisha katiba mpya.
Ni kipindi chake tu tulishuhudia kiongozi wa taifa akiendesha shughuli za serikali bila kujihusisha na siasa za kikabila au kuonyesha upendeleo katika siasa za urithi mwaka wa 2013.
Tunapozika shujaa Kibaki kesho kutwa, wananchi watashiriki uchaguzi ujao mwaka huu ambapo itakuwa fursa yetu kuchagua viongozi kuanzia Rais hadi mwakilisihi wadi kijijini unamoishi.
Je, utatumia kura yako kuchagua Kibaki mwingine? Je, kura yako Agosti 9, 2022 itabadilisha uongozi mbaya na kuleta matumaini kwa Wakenya?
Je, ni kiongozi yupi kati ya wagombeaji Urais katika kundi la Azimio au Kenya Kwanza anayeweza kufanikisha maendeleo kwa manufaa ya taifa hili kama Mzee Kibaki?
Maswali hayo ndiyo yanayopaswa kuzingatiwa na kila mpigakura, ikiwa tuna nia ya kuchagua kiongozi mwenye sifa za Kibaki katika uchaguzi wa mwaka huu.
Tuanze kujadiliana sasa bila ushabiki wa mirengo ya kisiasa na kikabila tujue matatizo yetu yatasuluhishwa tu na viongozi waliojitolea kubadilisha taifa hili bila unafiki wa kisiasa. Mwai Kiba