Wakenya wawili wamiliki mali zaidi ya wananchi milioni 16
NA PETER MBURU
PENGO kati ya matajiri na maskini nchini limefikia viwango vya kutisha ikiibu – ka kuwa Wakenya wawili matajiri zaidi wako na mali nyingi kuliko jumla ya inayomilikiwa na wananchi maskini milioni 16.5.
Ripoti inayozinduliwa leo na mashirika ya kuheshimika kimataifa ya Oxfam na Development Finance International (DFI), inasema kuwa jinsi watu wachache matajiri wanavyoendelea kutajirika ndivyo idadi ya maskini inavyopanda, hali inayochangiwa na ukosefu wa usawa wa kiuchumi.
Kwa kutumia utajiri wa Wakenya wawili matajiri zaidi ambao mali yao ni jumla ya Sh174.5 bilioni, hii ni kumaanisha kuwa kwa wastani kila mmoja wa Wakenya maskini milioni 16.5 maskini anamiliki chini ya Sh10,575 kama utajiri wake.
Kulingana na ripoti ya Oxfam iliyoorodhesha Wakenya matajiri zaidi mwezi uliopita, Sameer Naushad Merali na Bhimji Depar Shah, ndio Wakenya matajiri zaidi, kwa pamoja wakimiliki mali ya Sh174.5 bilioni.
Bw Merali ni mwanawe aliyekuwa mfanyabiashara tajika nchini, Naushad Merali aliyeaga dunia Julai mwaka jana. Ripoti hiyo ilibaini kuwa utajiri wake ni Sh89.5 bilioni. Naye Bw Shah aliyebainika kuwa na utajiri wa Sh85 bilioni, ni mwanzilishi wa kampuni ya Bidco, inayotengeneza bidhaa mbalimbali za matumizi ya nyumbani.
Waliofuata Wakenya hawa kwa utajiri ni Jaswinder Singh Bedis aliyebainika kuwa na utajiri wa Sh77.1 bilioni na familia ya rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta, kwa utajiri wa Sh60.1 bilioni.
“Viwango vikubwa vya ukosefu wa usawa wakati kwa wengine utajiri unaongezeka na mamilioni ya Wakenya kuzama katika umaskini na ukosefu wa matumaini ni matokeo ya chaguo la kisiasa. Ni uchafu, ukosefu wa maadili na ukatili wa kijamii,” akasema Bw John Kitui, Mkurugenzi wa Oxfam Kenya.
Mabilionea 120 pekee
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa japo janga la Covid-19 limesukuma zaidi ya Wakenya milioni mbili katika umaskini, huku majanga mengine kama kiangazi, viwavi
jeshi na yanayohusiana na mabadiliko ya anga yakiwafanya takriban Wakenya milioni tatu kukosa chakula, idadi ya matajiri wakubwa nchini inazidi kuongezeka.
“Japo Kenya imeshuhudia ukuaji mkubwa wa kiuchumi miaka ya majuzi, ukosefu wa usawa wa kiuchumi unasalia kuwa juu, huku maendeleo yakiwa kwa wachache. Kati ya 2016 na 2021, idadi ya Wakenya wenye utajiri zaidi ya Sh5.6 bilioni iliongezeka kutoka 80 hadi 120.
Utajiri wao kwa pamoja ulipanda kutoka Sh1.4 trilioni hadi Sh1.9 trilioni,” mashirika hayo yakasema katika taarifa jana.
“Ukijumuisha utajiri wa watu wawili matajiri zaidi Kenya wanamiliki utajiri mkubwa zaidi ya asilimia 30 ya idadi ya watu maskini nchini, ama watu milioni 16.5,” ripoti hiyo inasema.
Mashirika hayo yanaitaka serikali kutopunguza bajeti ya baadhi ya sekta muhimu kama afya, elimu na ulinzi wa kijamii kama ilivyopanga, yakisema hatua hiyo itawatesa Wakenya wengi zaidi ambao hawana uwezo wa kifedha kulipia huduma hizo muhimu.
Badala yake, mashirika hayo yanapendekeza kuwa serikali ianze kuwatoza Wakenya matajiri ushuru kwa viwango vya asilimia 2 kwa Wakenya wenye utajiri
zaidi ya Sh550 milioni na asilimia 3 kwa wenye utajiri wa zaidi ya Sh5.6 bilioni, kwani ushuru huo utaipa serikali zaidi ya Sh900 bilioni kila mwaka za kugharamia shughuli zake za maendeleo na kuinua maskini kiuchumi.
Yakisema ushuru huo utasaidia kupunguza viwango vya ukosefu wa usawa kiuchumi nchini kwa kuhakikisha kuwa serikali inapata pesa zaidi za kufadhili sekta muhimu kiuchumi, mashirika hayo pia yanazitaka Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutambua viwango vya ukosefu wa usawa kiuchumi hapa Kenya na kuanza kufuatilia kuhakikisha kuwa vinapunguzwa.
“Mapendekezo ya kupunguza bajeti yatahatarisha uwezo wa serikali kufadhili afya, elimu, ulinzi wa kijamii na utoshelezaji wa chakula. Ili kulinda walioathirika na janga la Covid-19 na matatizo ya kiuchumi ni muhimu kuhakikisha pesa zaidi zinatengewa hudumu za kimsingi,” yakasema.
Mashirika hayo yanasema kuwa wakati wa utafiti, zaidi ya asilimia 75 ya Waken – ya waliunga mkono kutozwa ushuru kwa matajiri ili kufadhili mipango ya kuwanufaisha maskini.
Next article
Mawaziri, makatibu wajiuzulu kujaribu bahati katika siasa