Wakili bandia taabani kwa kumwakilisha mganga kutoka Ghana
NA RICHARD MUNGUTI
WAKILI bandia aliyejitokeza mahakamani kumtetea mganga wa dawa za kienyeji kutoka Afrika Magharibi ameshtakiwa kujifanya mwanasheria.
Mganga huyo Adoulaye Tamba Kouro aliye pia raia wa Ghana ameshtakiwa kumlaghai aliyekuwa waziri msaidizi Danson Mungatana Sh76 milioni akidai ataziekeza katika biashara ya mafuta.
Wakili huyo feki, Edwin Motari Ong’uti alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu Susan Shitubi katika mahakama ya Milimani.
Motari alidaiwa alifanya wakili mbele ya hakimu mkuu Wendy Kagendo mnamo Aprili 12,2022, Kouro alipofikishwa kortini.
Kouro alikuwa ametoroka kisha polisi wakamkamata na kumfikisha mahakamani.
Bi Kagendo alimwuliza Motari kama alikuwa amepata shahada ya digrii katika somo la Sheria na kuhitimu katika shule ya mawakili (KSL) na kuapishwa na Jaji Mkuu.
“Je, ulisuluhisha suala la masomo yako?” Bi Kagendo alimwuliza Motari.
“Bado sijakamilisha lakini ninaendelea na masomo ya uanasheria,” Motari alijibu.
Bi Kagendo aliamuru polisi wamkamate Motari na kumfungulia shtaka la kujifanya wakili na kujaribu kumtetea Kouro kortini.
Baada ya agizo hilo kutolewa Motari alikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi cha Capitol Hill kuhojiwa na kufunguliwa mashtaka.
Alipofikishwa mbele ya Bi Shitubi mshtakiwa alijaribu kujieleza kuwa anaendelea na masomo ya uanasheria lakini “akaambiwa bado kuhitimu kuwa wakili.”
Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu akisema “hana kazi inayomletea kipato.”
Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.
Kesi hiyo itatajwa Aprili 28,2022 kutengewa siku ya kusikizwa.
Motari alijipata pambaya alipoomba mahakama imrudishie dhamana Kouro baada ya kutoroka kisha akatiwa nguvuni
Kouro amekana alimkomoa Muungatana Sh76milioni miaka tisa iliyopita.
Akiomba arudishiwe dhamana tena Kouro alishangaza mahakama alipodai alikuwa mgonjwa lakini alikuwa akitumia dawa za kienyeji kutoka nchi jirani ya Tanzania kujitibu na wala hakuenda hospitali kutumia dawa za kimaabara.
Kouro alimsihi Bi Kagendo amwachilie kwa dhamana tena lakini ombi lake likagonga mwamba alipotakiwa awasilishe stakabadhi za hospitali kuthibitisha alikuwa mgonjwa.
“Je uko na rekodi zozote kutoka hospitali kuthibitisha ulikuwa mgonjwa,” Bi Kagendo alimwuliza Kouro.
“Mheshimiwa sina rekodi zozote kutoka hospitali kuonyesha nimekuwa nikipokea matibabu. Nimekuwa nikutumia dawa za kienyeji kujiganga kutoka Tanzania.Samahani,” Kouro alimweleza hakimu.
Bi Kagendo alimweleza mshtakiwa kwamba itabidi azuiliwe gerezani kwa vile alikaidi agizo la mahakama alipoachiliwa kwa dhamana.
Mahakama ilimweleza masharti ya dhamana ni kufika kortini kila alipohitajika kuendelea na kesi lakini alidharau na kutoroka.
Lakini Kouro alisema, “Naomba tu uniwie radhi na kufutilia kibali cha kunitia nguvuni kilichotolewa na hii mahakama nikamatwe na dhamana yangu kufutiliwa mbali.Nimeghairi makosa yangu.Nihurumie tu.”
Mshtakiwa huyo aliomba tu mahakama isimchukulie kuwa mbaya ni vile alikuwa sio buheri wa afya.
Kiongozi wa mashtaka Anderson Gikunda alieleza mahakama itilie maanani kipindi cha miezi zaidi ya sita mshtakiwa alichotoroka mahakama.
“Ilibidi polisi watumie kila mbinu kumtia nguvuni mshtakiwa. Naomba korti iamuru azuiliwe gerezani kwa vile amekaidi maagizo ya hii mahakama,” alisema Gikunda.
Kouro anakabiliwa na shtaka la kumlaghai Muungatana Dola za Marekani 1,000,000 (Sh76 milioni) kati ya Aprili 20-29, 2013 katika makazi ya Sandalwood Apartments ,Westlands Nairobi akidai ataziekeza katika biashara ya mafuta.
Mahakama iliamuru mshtakiwa azuiliwe hadi leo Aprili 19, 2022 korti itakapoamua ikiwa atarudishiwa dhamana au la.