Connect with us

General News

Wakulima wa parachichi watumie vyema fursa iliyoko ya ‘soko tayari’ nchini China – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wakulima wa parachichi watumie vyema fursa iliyoko ya ‘soko tayari’ nchini China – Taifa Leo

Wakulima wa parachichi watumie vyema fursa iliyoko ya ‘soko tayari’ nchini China

NA SAMMY WAWERU

FEBRUARI 2022, China ilifungua soko la maparachichi kutoka Kenya.

Hatua hiyo ilitokana na kuendelea kuimarika kwa uhusiano bora wa kibiashara kati ya Kenya na China.

Aprili 2019, Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa China, Xi Jinping, walitia saini mkataba wa makubaliano Kenya kuuza mazao yake ya maparachichi nchini humo.

Makubaliano hayo yaliwapa afueni wakulima, japo waliruhusiwa kuuza maparachichi ambayo yametolewa maganda na kugandishwa.

Mikakati na taratibu hizo za Beijing, zililemea wazalishaji wengi ikizingatiwa kuwa uwekezaji wa mashine ya shughuli hiyo ni bei ghali.

Ni kampuni moja pekee inayouza mazao mabichi ya shambani kimataifa ilimudu, licha ya kuwa na zaidi ya mashirika mengine 100.

Maparachichi aina ya Hass. PICHA | SAMMY WAWERU

Tangazo la wakulima kuruhusiwa kuuza maparachichi mabichi yaliyokomaa China, ni afueni.

Kutokana na vikwazo ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa, itakuwa busara ikiwa wakulima watajituma kuzalisha mazao yaliyoafikia ubora wa bidhaa – kwa mujibu wa soko la China.

Itakumbukwa kwamba, licha ya Rais Kenyatta na mwenzake Xi Jinping kutia saini mkataba, baadaye Kenya iliwekewa marufuku ya muda.

Hata ingawa yaliondolewa, China ililalamikia kusambaziwa maparachichi ambayo hayajakomaa.

Taasisi ya Mazao Mabichi na Mimea (HCD) kwa ushirikiano na ile ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis), ndizo zinajukumika kuhakikisha mazao yanayoingia masoko ya kimataifa yameafikia ubora.

Mashirika hayo, yamekuwa katika mstari wa mbele kuhamasisha wakulima na kampuni zinazowatafutia soko nje ya nchi kuafikia vigezo faafu.

“Kenya imepata kibali kuuza maparachichi mabichi yaliyokomaa nchini China,” akatangaza Prof Theophilus Mutui, Meneja Mkuu Kephis.

Afisa huyo alisema hatua hiyo iliafikiwa baada ya Kephis na China kutathmini suala la wadudu wanaoshambulia maparachichi, na jinsi ya kuwakabili.

Wazalishaji na wanaouza mazao mabichi ya kilimo masoko ya kimataifa, hawana budi ila kuafikia matakwa yaliyowekwa.

Aidha, yanajumuisha, kuhakikisha mashamba, maghala ya kupakia na vituo vya kutibia maparachichi yao, yamesajiliwa na Kephis.

Kulingana na shirika hilo la kiserikali, wakulima watahitajika kuzingatia mbinu faafu kuendeleza kilimo na kukabiliana na kero ya wadudu.

Masoko ya ughaibuni yamekuwa yakilalamikia mazao ya maparachichi ambayo hayajakomaa, kutoka humu nchini.

Mabroka walioteka nyara masoko ya mazao ya kilimo nchini, wametajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo, baadhi wakilaumiwa “kushinikiza wakulima kuvuna maparachichi kabla kukomaa”.

Kulingana na wataalamu, maparachichi yanayovunwa kabla ya kukomaa ni vigumu kuiva.

“Huishia kuharibika na hatimaye kuoza. Mazao ya aina hiyo huharibu soko,” aonya Daniel Mwenda, mtaalamu wa masuala ya matunda na miti.

“Kuna vigezo kadha wa kadha kutambua maparachichi yaliyokomaa. Mosi, matunda kubadili rangi kutoka kijani kibichi na kuwa kijani cheusi.

“Mengine, yanakuwa meusi. Vilevile, unapotikisa tunda na kusikia sauti ya mbegu ikicheza, ni ishara kuwa limekomaa,” mdau huyu ashauri.

Maparachichi aina ya Hass yanaendelea kuwa na ushindani mkuu katika masoko ya kimataifa.

Yale ya Fuerte, vilevile yanashika kasi.

Mzee Francis Njoroge, ni kati ya wakulima wanaopenda na kustawisha maparachichi aina ya Hass, Kenya.

Akiwa mkulima wa matunda hayo ya thamani katika Kaunti ya Murang’a, Njoroge anayakuza kwenye nusu ekari.

Ni mwanachama wa Kihoto-Kihumbuini Self Help Group, muungano wanaotumia kusambazia kampuni ya kuwatafutia soko.

Kulingana na takwimu za HCD mwaka uliopita, 2021, Kenya iliuza kilo milioni 84.5 ughaibuni kutoka kilo milioni 70.3 mwaka 2020.