WANTO WARUI: Walimu wana kibarua kuandaa watahiniwa kwa mitihani mitano ya kitaifa 2022
Na WANTO WARUI
WALIMU wana kibarua kigumu sana cha kuwatayarisha wanafunzi kufanya mitihani ya kitaifa mwaka 2022.
Mitihani hiyo ambayo yote mitano imenuiwa kufanywa hapo mwakani inajumlisha miwili ya Kidato cha Nne (KCSE), miwili ya Darasa la Nane (KCPE) na mmoja wa Gredi ya Sita (CBA).
Akitangaza kuhusu ratiba hiyo hapo wiki jana, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha alisema kuwa mtihani wa darasa la nane KCPE ndio utakaofungua ukurasa na utafanywa kati ya Machi 7-10 huku ukifuatiwa na ule wa kidato cha nne (KCSE). Hiyo mingine mitatu inayobakia imeratibiwa kufanywa mwezi wa Disemba 2022.
Kutokana na tangazo hilo, bila shaka walimu wana kibarua kigumu cha kutayarisha wanafunzi kwa mitihani ya kitaifa ndani ya mwaka mmoja.
Wale hasa walio na kazi ngumu zaidi ni wale wa shule za msingi kwani wanatarajiwa kuwa wakitayarisha madarasa matatu kwa pamoja sasa ambayo ni darasa la nane, darasa la saba na wale walio Gredi ya tano sasa.
Matayarisho kama haya ni changamoto kweli kwa walimu hasa katika zile shule ambazo zinakumbwa na uhaba wa walimu.
Jambo jingine ambalo linaweza kutatiza ni maandalizi ya wanafunzi wa Gredi ya Sita. Itakuwa ni mara ya kwanza kwa mfumo huu kujaribiwa katika matokeo ya mitihani ya CBA na walimu wengi hawana ujuzi wa kuwaelekeza wanafunzi katika mitihani hii licha ya kuwa wamekuwa wakifunzwa katika makongamano.
Wazazi wa wanafunzi wa Gredi ya sita nao wamechanganyiwa kwani hawaelewi masuala mengi yanayohusiana na mfumo huu wa CBC.
Walimu na wazazi waunde mikakati mwafaka ili kuhakikisha kuwa wanafunzi hawa wanafanya mitihani yao kama ilivyopangwa.
Tayari taasisi ya mitihani nchini (KNEC) imekuwa ikiwasilisha mitihani ya CBA kwa shule zote za msingi na kutoa maelekezo kuhusu kufanywa kwa mitihani na kujaza matokeo kupitia mtandaoni.
Huku matayarisho haya ya mitihani yakiendelea, bado kungali na maswali mengi kuhusu shule za sekondari ambako wanafunzi wa Gredi ya sita wanatarajiwa kusomea. Serikali imesikika mara kwa mara ikitoa taarifa tatanishi hivyo basi kuwaacha walimu, wanafunzi na wazazi wakiwa na maswali kuhusu mpito wa masomo ya CBC kutoka shule ya msingi hadi ile ya sekondari.
Bila shaka, tunapoingia mwaka wa 2022 ambao utakuwa na shughuli nyingi ikiwemo uchaguzi mkuu hapo mwezi wa Agosti, walimu watakuwa na hali ngumu ya kuwatayarisha wanafunzi. Ni sharti wajitayarishe vyema wao wenyewe wasije kuwachanganya wanafunzi.Wizara ya Elimu isikae pembeni kujitazamia walimu wakitaabika katika shughuli hii yote bali ifanikishe shughuli hii ya matayarisho ya wanafunzi.