Connect with us

General News

Waliojiunga na magaidi wanusuriwe – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Waliojiunga na magaidi wanusuriwe – Taifa Leo

TAHARIRI: Waliojiunga na magaidi wanusuriwe

Na MHARIRI

WITO wa Mshirikishi wa Shughuli za Serikali Kuu ukanda wa Pwani, John Elungata, kuwataka wazazi Kaunti ya Tana River kuwasalimisha kwa serikali watoto wao waliopewa mafunzo yenye itikadi kali – yanayochochea vijana kujiunga na makundi ya kigaidi – unastahili kuungwa mkono.

Wito sawa na huo unafaa kutolewa kote nchini kuwezesha vijana waliopata mafunzo hayo kusaidiwa kuachana na fikra hizo potovu.

Kulingana na Kituo cha Kupambana na Ugaidi nchini (NCTC), mafunzo hayo yameshika kasi katika Kaunti 12, yakiwemo maeneo yanayopakana na nchi jirani ya Somalia.

Mnamo Juni, kituo cha NCTC kilisema vijana 350 waliokuwa wamejiunga na Al-Shabaab, wamerejea nchini na kujisalimisha kwa serikali mwaka huu.

Kituo hicho kilisema wakati huo kilikuwa kinaendelea na mchakato wa kusaidia zaidi ya vijana 300 waliokuwa wapiganaji wa kundi la al-Shabaab kujumuka tena na jamii.

Takwimu hizo ni za kuogofya kwani idadi ya vijana Wakenya walioko Somalia wakipigania kundi la Al-Shabaab, haijulikani.

Aidha, idadi ya vijana waliopewa mafunzo yenye itikadi kali nchini wanaotafuta mwanya wa kuelekea Somalia kujiunga na al-Shabaab au makundi mengine ya kigaidi kama vile Islamic State, pia haijulikani.

Kulingana na Bw Elungata, vijana waliopewa mafunzo yenye itikadi kali wanaweza kusaidiwa kuondoa fikra hizo za kinyama kwa kupewa ushauri nasaha na wataalamu.

Kuna uwezekano wengi wa wazazi wa vijana hao, hawajui kwamba watoto wao wamepewa mafunzo kama hayo.

Hivyo, kuna haja ya serikali kuweka mikakati mwafaka itakayohakikisha vijana hao wanajisalimisha bila kupitia kwa wazazi wao.

Vilevile, wito huo hautoshi iwapo serikali haitawahakikishia wazazi hao kwamba, wanao hawataandamwa au kuhangaishwa na maafisa wa usalama endapo watajitokeza na kukiri kupokea mafunzo yenye itikadi kali.

Mbali na mafunzo yenye itikadi kali, serikali inastahili kufanya utafiti wa kina ili kubaini kiini cha idadi kubwa ya vijana kukimbilia kujiunga na makundi ya kigaidi.

Umaskini kupindukia ni miongoni mwa sababu kuu ambazo zimekuwa zikitolewa kusukuma vijana kujiunga na mitandao ya kigaidi.

Makundi hayo ya kigaidi yamekuwa yakitoa ahadi hewa za kuwapa fedha vijana wanaojiunga nao.Hivyo, kutoa ushauri nasaha tu kwa vijana waliopokea mafunzo hayo hakutoshi, mengi yastahili kufanywa.