Wamalwa atoa hakikisho la upatikanaji wa haki kwa familia ya Agnes Wanjiru aliyeuawa na mwanajeshi wa Uingereza
Na CHARLES WASONGA
WAZIRI wa Ulinzi Eugene Wamalwa, Jumanne aliwahakikishia wabunge kwamba serikali ya Uingereza imejitolea kushirikiana na Kenya katika juhudi za kuhakikisha kuwa mwanajeshi wake aliyemuua Agnes Wanjiru mjini Nanyuki, Kaunti ya Laikipia anaadhibiwa.
Akiongea alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni Bw Wamalwa alisema kuwa amepata hakikisho hilo kutoka kwa Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace na Balozi wa Uingereza nchini Jane Marriott.
“Ningependa kuwahakikishia kwamba tumefanya mashauriano na serikali ya Uingereza kuhusu suala hili lenye umuhimu wa kitaifa. Leo asubuhi nilikutana na balozi wa Uingereza na mwenzangu wa Uingereza na wamenihakikishia kuwa mwenajeshi huyo ataletwa nchini ili ashtakiwe kwa mujibu wa sheria za nchi hii,” akaambia kikao cha kamati hiyo kilichoongozwa na Mbunge wa Saku Dida Rasso.
“Hatimaye haki itatendekeka kuhusu suala hili la mauaji ya Agnes Wanjiru. Tunajua kwamba familia yake na Wakenya kwa ujumla wanalilia haki ambayo kwa kweli imecheleweshwa kwa kupindi cha miaka tisa,” Bw Wamalwa akaongeza.
Waziri alipuuzilia mbali madai kuwa maafisa wa serikali ya Kenya wanaendesha njama ya kuficha ukweli kuhusu mauaji ya mwanamke huyo ili kulinda uhusiano kati ya Kenya na Uingereza.
“Hakuna afisa wa serikali anayetaka kuficha ukweli kuhusu suala hilo muhimu. Ni kweli kwamba haki imecheleweshwa kuhusiana na mauaji ya Agnes Wanjiru lakini sharti tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kuwa inapatikana.
Hata hivyo, Mbunge wa Yatta Charles Kilonzo alitilia shaka hakikisho hilo, akisema miaka tisa ni kipindi kirefu mno ikizingatiwa kuwa marehemu Wanjiru aliuawa na mwanajeshi wa Uingereza mjini Nanyuki mnamo Machi 31, 2012.
“Kila mtu anataka kuona haki ikitendeka. Miaka tisa imepita huku hakikisho hilo likitolewa. Sasa wewe waziri Wamalwa unatuambia kwamba unataka sisi kama wabunge tuidhinishe mkataba wa ushirikiano na Uingereza ilhali serikali haina haraka ya kuadhibu mshukiwa,” akasema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mandera Kaskazini Bashir Abdullahi alitisha kuwa huenda wabunge wakakataa kuidhinisha mkataba mpya wa ushirikiano kati ya Kenya na Uingereza ambao unatarajiwa kuletwa bungeni hivi karibuni.
“Hatuwezi kupitisha mkataba huo hadi pale tutakapopata hakikisho na ushahidi tosha kwamba serikali ya Kenya inashughulikia suala hili kwa lengo la kumleta mshukiwa nchini ili ashtakiwe kwa mujibu wa sheria za humu nchini,” akaeleza.
Wanjiru, 21, alioenekana mara ya mwisho akiingia katika mkahawa wa Lions Court mjini Nanyuki akiandamana na wanajeshi wawili wa Uingereza. Miezi miwili baadaye mwili wake ulipatikana katika shimo la maji taka (septic tank) karibu na chumba ambacho alidaiwa alilala.
Uchunguzi kuhusu kifo chake ulifanywa na ikabainika kuwa Wanjiru ambaye alimwacha mtoto mwenye umri wa miaka mitano, aliuawa. Uchunguzi huo uliendeshwa na mahakama ya Nanyuki.
Mnamo Jumanne wananchi mjini Nanyuki waliungana na watu wa familia yako kufanya maandamano wakiitisha haki.
Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai kwa mara nyingine ameamuru kuwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ishughulikie kesi hiyo kwa lengo la kuhakikisha kuwa mshukiwa amehukumiwa kwa mujibu wa sheria.
Next article
Tottenham Hotspur waajiri Antonio Conte kuwa mrithi wa…