TAHARIRI: Wananchi wasaidie kukabili ugaidi
NA MHARIRI
USALAMA wa raia na mali yao ni muhimu na unafaa kuhakikishwa kila wakati.
Kufuatia onyo lililotolewa na mataifa ya Ulaya na Amerika kwa raia wake nchini kuepuka baadhi ya maeneo yanayoweza kulengwa na magaidi, Wakenya wameingiwa na hofu wakiwa katika shughuli zao za kila siku.
Serikali ya Kenya, imesema mataifa hayo hayakufaa kutoa onyo hilo kwa kuwa ina uwezo wa kukabiliana na tisho la ugaidi na kuwafahamisha raia kuchukua tahadhari.
Kulingana na serikali, imeimarisha usalama katika maeneo yaliyo kwenye hatari ya kukabiliwa na tisho la ugaidi na imewataka raia kuwa makini na kuripoti vitendo vyovyote vya watu wanaowashuku kuhusika na uhalifu ukiwemo ugaidi.
Tunakubaliana na serikali kuwa kila Mkenya ana jukumu la kuchangia kudumisha usalama wake na nchi kwa jumula.
Raia wakiwajibika na maafisa wa usalama watekeleze majukumu yao ipasavyo bila ubaguzi na kunyanyasa raia, magaidi hawatapata upenyo wa kuendeleza vitendo vyao vya uhayawani nchini.
Kama nchi, tumekuwa waathiriwa wa mashambulio ya kigaidi mara si moja na habari zozote za uwezekano wa kutokea kwa shambulio kunatia wengi tumbojoto.
Kumekuwa na ripoti za baadhi ya watu kusaidia na hata kupatia makao washukiwa wa ugaidi ili wapange na kutekeleza mashambulizi.
Kuna wanaofahamu kuwa watoto au jamaa zao ni washirika wa mitandao ya ugaidi na hawakuchukui hatua.
Watu kama hao huwa hawasaidii nchi yao.
Usalama hauwezi kuachiwa maafisa wa usalama pekee.
Raia wanafaa kusaidia maafisa hao kuwalinda na kwa kufanya hivi nchi inakuwa salama na kuvutia wawekezaji.
Lengo la magaidi ni kuzua taharuki na hofu ili kuwafukuza wawekezaji na kuvuruga uchumi.
Hili linapotendeka ni raia wanaoteseka. Ushirikiano wa raia na maafisa wa usalama unaweza kukomesha ugaidi na kufanya nchi kuwa salama.