TAHARIRI: Wanasiasa waache kuhadaa kwa spoti
KITENGO CHA UHARIRI
KATIKA kipindi hiki cha kampeni, bila shaka wanasiasa mbalimbali watajitokeza kwa hali na mali kubuni miradi ya kila aina ya kuwavutia wananchi, hasa vijana.
Wanasiasa wengi watarejea mashinani kusaka kura kwa ajili ya kuwapokonya wapinzani wao viti au kudumisha viti wanavyoshikilia kwa sasa.
Kwa sababu hiyo, watafanya kila juhudi kuhakikisha wanafanya vitu vinavyowashawishi wapigakura kwa namna moja au nyingine.
Wengi wa wapigakura ambao hulengwa katika njama hizi ni vijana. Utashuhudia mashindano mbalimbali hasa ya kandanda yakianzishwa kila mahali.
Vijana watashindania pesa na tuzo nyinginezo mzomzo ambazo kwa bahati mbaya zitaisha punde uchaguzi mkuu utakapokamilika.
Naam, japo tunaunga mkono mchango wa wanasiasa katika kukuza talanta za vijana, hisani hiyo haifai kuisha tu punde wanapochaguliwa katika nyadhifa za kisiasa.
Hasa kwa wanaoshinda uchaguzini, ipo haja ya kuendeleza mashindano ya mashinani ambayo bila shaka yatawashughulisha vijana, na hivyo basi, kuwaepusha na maovu yanayotokana na kukosa la kufanya.
Manufaa hayo ni mbali na kuwawezesha vijana kukuza talanta na kujipa pato, japo dogo.
Hatua ya wanasiasa hao kuanzisha mashindano mengi wakati wa kampeni kisha upigaji kura unapomalizika, wanatoweka, ni ishara ya wazi kuwa nia yao huwa ni ya kibinafsi wala si ya kuwanufaisha vijana jinsi ambavyo huwa wanajisawiri.
Nia zao zingekuwa nzuri, wangekuwa wanahakikisha kuwa mashindano hayo hayakomi.Hilo ndilo tatizo letu na vinyang’anyiro hivi vinavyoanzishwa na wanasiasa hao.
Sekta ya michezo ni mojawapo ya nguzo muhimu katika ukuzaji jamii yenye afya, wajibifu na jumuishi. Afya, kwa sababu ya kujiweka imara kimwili kutokana na mazoezi.
Wajibifu, kwa sababu vijana hao wanahusishwa katika shughuli za kukuza nchi, na jumuishi kwa sababu kila raia wa taifa hili anahusika katika shughuli za maendeleo za nchi yake bila kuacha nyuma yeyote.
Kwa hivyo, ni bora wapigakura wahakikishe wamepata hakikisho kutoka kwa wanasiasa hao kuhusu mustakabali wa mashindano hayo.
Wakikosa kuyaendeleza baada ya uchaguzi, basi wasichaguliwe katika kipindi kijacho au wale wanaorejea ulingoni kuwania wasichaguliwe asiliani.
Next article
Washukiwa saba wa wizi wa simu za rununu wanaswa Thika