Connect with us

General News

Wanasiasa wanawahadaa wanaoishi ughaibuni – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wanasiasa wanawahadaa wanaoishi ughaibuni – Taifa Leo

DOUGLAS MUTUA: Wanasiasa wanawahadaa wanaoishi ughaibuni

Na DOUGLAS MUTUA

SI siri kamwe kwamba wanasiasa nchini Kenya wamezoea kuwachezea Wakenya, lakini sasa wamevuka mipaka na kuwafuata hata na waliohamia nchi za watu.

Yapata miezi saba pekee hadi uchaguzi mkuu ujao ufanyike, washindani wakuu katika ulingo wa siasa wamezuka na ahadi za ajabu zinazowasawiri kama wasiojua kitu.

Kinara wa Orange Democratic Party (ODM) Bw Raila Odinga amewaahidi wanaoishi ughaibuni kuwa haki yao ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu itatimizwa mwaka ujao 2022.

Labda kwa kujua Wakenya hao hukerwa na kutozwa ushuru tu na kuchangia makuzi ya uchumi wa taifa lao bila manufaa yoyote, Bw Odinga amewahimiza wawanie vyeo.

Amedai hakuna sheria inayowanyima haki ya kuwania vyeo hata wakiwa na uraia wa nchi mbili, eti wakifanya hivyo kisha wakumbwe na matatizo ya kisheria wamjulishe. Kituko!

Naye Naibu Rais, Dkt William Ruto, ameahidi kuwa akichaguliwa rais mwakani, serikali yake itatenga wizara mahsusi ya kuyashughulikia masuala ya wanaoishi nje ya nchi.

Dkt Ruto aliongeza kuwa watu wanaotuma nchini takriban Sh400 bilioni kila mwaka hawapaswi kupuuzwa; pesa zao zinahitaji kutafutiwa utaratibu bora wa kutumika.

Ni mengi waliyoahidi wawili hao, lakini hayo ya haki ya kupiga kura na kubuniwa wizara maalum yalinigusa mimi binafsi kama mmoja wa hao wanaoishi ughaibuni.

Mwanzo tukubaliane: Hizo zote ni ahadi hewa; wajanja hao wawili wamekuwa kwenye siasa kwa miongo mingi, lakini wanayavalia njuga maslahi ya walio ng’ambo sasa hivi tu.

Si sadfa, wanafanya kampeni kwa kuwa wanaamini uchaguzi mkuu utakuwa na ushindani mkali hivi kwamba hata kura chache tu zinaweza kuathiri matokeo.

Mathalan, Bw Odinga amekuwa katika siasa tangu akiwa kijana hadi akakonga, mwenyewe aliishi ughaibuni, lakini hajawahi kuona haja ya kuwatetea Wakenya hao.

Mbona sasa anajituma sana kana kwamba Wakenya wameanza kuishi ng’ambo mwaka huu? Hivi huku si kuzichezea akili razini za Wakenya?

Mbona Bw Odinga hajatamka neno kuwahusu hao wanaoishi nje tangu awe mshirika wa kupanga katika serikali hii ya wagombanao? Amesubiri muda huo wote akitaka nini?

Naye Dkt Ruto ana lipi la kutwambia ispokuwa kufirikia jinsi pesa zetu zitakavyotumika ilhali amekuwa katika siasa tangu miaka ya 1990?

Alifanya nini cha kukumbukwa na Wakenya hao alipokuwa mdau na msiri wa Rais Uhuru Kenyatta wakati wa kipindi cha kwanza?

Ni kitu gani kinachomsadikisha kuwa, ili Wakenya walio ng’ambo wapate haki zao, ni lazima ibuniwe wizara maalum ya kuwashughulikia? Anatupumbaza!

Watu si wapumbavu; tunajua uchaguzi umekaribia, hivyo kila aina ya propaganda, hata uongo wa wazi kabisa, ni miongoni mwa mbinu za kutafuta mamlaka makuu zaidi nchini.

Tunaoishi nje tunajua fika kwamba udanganyifu, utapeli na uhalifu ni baadhi ya mbinu maarufu zaidi miongoni mwa wanasiasa wakuu wanapotia nia kutawala.

Hatuna chochote maalum cha kuwafanya wasitumie mbinu hizo kupata kura zetu, hivyo wanapotuahidi mambo yasiyoaminika tunafahamu mara moja.

Ikiwa wamekataa kuwabadilishia maisha mamilioni ya Wakenya walio nchini, wana msukumo gani kutufaa sisi tunaozuru Kenya mara moja-moja?

Mambo yatasalia vilevile hata baada ya miaka mitano ijayo, na nakuhakikishia ahadi zinazotolewa zitakaririwa tena kama mashairi hapo 2027.

Kwa mwanasiasa, Mkenya anayeishi ughaibuni ni chombo cha kulipa ushuru na kutoa fedha ili kuchangia uchumi, hakina haki zozote. Upigaji kuwa wetu utawafaidi wao, si sisi.

Mataifa yanayojua umuhimu wa wanaoishi ng’ambo hayaweki vizuizi vya kuwakwaza bali huwawezesha kujihisi nyumbani kote kuwili.

Ndiyo sababu hakuna Mwingereza anayelalamika kwamba Waziri Mkuu Boris Johnson ni raia wa Marekani.

Wanasiasa wetu wakiendelea kufikiria kishamba watasalia washamba daima, nayo Kenya itakuwa taifa la washamba.

[email protected]

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending