Connect with us

General News

Wanawe 19 wamletea faraja ingawa alikosa ushauri bora kuhusu upangaji wa uzazi – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wanawe 19 wamletea faraja ingawa alikosa ushauri bora kuhusu upangaji wa uzazi – Taifa Leo

Wanawe 19 wamletea faraja ingawa alikosa ushauri bora kuhusu upangaji wa uzazi

Na FATUMA BUGU

WAKATI mwingine huwa vigumu kwa mzazi kulea mtoto mmoja au wawili. Lakini je, ushawahi kujiuliza kuhusu kazi ya kulea watoto 19?

Kutana na Bi Mbodze Munga, ambaye ni mama aliyejaliwa watoto 19 ambao wana umri kuanzia miaka 32 hadi miwili.Safari yake kufikia hapo haikuwa ya kujitakia, bali kwa kukosa ushauri mwafaka mapema kutoka kwa wahudumu wa afya kuhusu upangaji uzazi wakati alipowaendea.

Tulifika nyumbani kwa Bi Mbodze katika kijiji cha Chasimba, Kaunti ya Kilifi na kupata picha halisi ya jinsi maisha yanavyomwendea segemnege.Wanawe wadogo walikuwa wakicheza huku wengine wakifua.Jikoni kwao kulikuwa kukavu jivu likiwa limetapakaa na vyombo vikiwa visafi tu, ishara kwamba hakukuwa na matayarisho yoyote ya chakula mchana huo.

Anakiri kuwa, kuwalisha watoto hao wote kila siku inavyostahili si rahisi hata akijikakamua kivipi.“Wote niliwazaa kwa njia ya kawaida bila kufanyiwa upasuaji. Wakati mwingi sisi hushinda na hata kulala njaa. Hatuna chakula cha kupika kila siku.

Tukipika sima mifuko miwili na vile wameshinda njaa, wanakula yote kwa vile ni riziki imepatikana lakini hawashibi,” anasema.Nyumba yao si nadhifu, ina paa la makuti ya mnazi yaliyochanika ambayo yamefunikwa kwa karatasi angalau kuikinga mvua kupenya ndani ya nyumba pindi kunaponyesha.

Kulingana naye, wao hulazimika kulala katika chumba kimoja, hali ambayo kwake ni ngumu lakini lisilo budi hubidi. Baadhi yao hulazimika kulala wakiwa wamekaa angalau wengine wapate nafasi.“Tunabanana yani hata nyumba haitoshi lakini nitafanyaje?

Huwezi kumwambia jirani akusaidie. Kweli utapeleka watoto walale kwa jirani? Nani atakubali? Inabidi wale wakubwa wanawapa nafasi wadogo walale,” anaeleza.Bi Mbodze, 57, anasema kwamba maisha yake yalichukua mkondo mpya baada ya kuolewa akiwa na umri wa miaka 19.Jambo hilo ni kinaya kwake kwani idadi ya watoto wake pia ni 19.

“Sisi huwataja majina kulingana na tukio ama mtu tunayempenda. Kuna Bruce Lee, kuna Hussein, kuna Shaban…na siwezi kuyasahau majina yao, ni watoto wangu,” anasema.Ijapokuwa anakiri kwamba hakutarajia wala kupanga kuwa na watoto wengi kiasi hicho, anasema hayo ni majaliwa ya Mungu.

“Namshurukuru Mungu kwani kuna wale ambao hawajajaliwa kupata watoto na wanahangaika kila siku kuwapata na mimi nimejaliwa wengi. Natoa tu shukrani.”Kulingana naye, alipozaa mtoto wake wa sita ndipo marafiki wakamshauri kwenda hospitalini ili apate usaidizi kuhusu upangaji uzazi.Safari zake nyingi kwa vituo vya afya vilimkatisha tamaa ya kupanga uzazi kwani aliambiwa ana tatizo la shinikizo la damu na uzani mkubwa, kwa hivyo si vyema akitumia mbinu zozote za kupanga uzazi.

“Waliniambia wanaweza kunipa ila zikinidhuru nisirudi kwao, nikaona basi haina haja nijiweke hatarini” anaeleza.Hali hii ndiyo ilimfanya aendelee kushika mimba na kuzaa mara kwa mara.Wakati alipopata mtoto wake wa 19 ambaye sasa ana umri wa miaka miwili, aliamua kutafuta tena usaidizi.

“Nilienda hospitalini wakanifanyia upasuaji na kunitoa mayai ya uzazi. Walinionyesha wakasema ‘hii ndiyo ilikuwa shida yako kubwa lakini sasa hautazaa tena,” akasema huku akitabasamu.Hata hivyo, mtaalamu wa upangaji uzazi, Bw Solomon Mwenda, anasema kuwa kuna mbinu mbalimbali ambazo mama huyo angeweza kufanyiwa bila yeye kulazimika kufanyiwa upasuaji kama njia ya kupanga uzazi.

Kulingana naye, mbinu za upangaji uzazi ni nyingi na kunazo ambazo kina mama wenye matatizo ya kiafya kama vile shinikizo la damu wanaeza kupewa bila kudhuru afya yao wala kuwahitaji kutolewa mayai ya uzazi.“Wizara ya Afya ina mwongozo mahususi unaotoa mwelekeo kuhusu aina za upangaji uzazi kwa watu tofauti.

Kusingekuwepo matatizo yoyote ya afya na haikuwa lazima yeye kufanyiwa upasuaji wa kutoa mayai yake ya uzazi,” asema mtaalamu huyo.Hata hivyo, kwa Bi Mbodze, kilichobaki kwake ni kujitahidi na maisha ya kuwalea wanawe 19.Baadhi yao wameshindwa kuendeleza elimu kwa sababu ya umaskini unaowakumba, kando na kuwa ni vigumu kwao kumakinika kimasomo ilhali wana njaa karibu kila siku.

Mume wake hutegemea vibarua vya ujenzi, na ikizingatiwa kuwa wanaishi kijijini, kazi hizo hazipatikani kwa urahisi. Mama huyo naye hutegemea vibarua vya kulimia watu mashamba, lakini eneo hilo wakati mwingi hukumbwa na kiangazi.Ijapokuwa halalamiki kuhusu kujaliwa watoto hao, anaamini matatizo yanayomkumba hivi sasa yangeepukika kama wahudumu wa afya wangemshughulikia ipasavyo mapema wakati alihitaji msaada wa upangaji uzazi.

“Ninapowaona napata faraja. Wajua kuna wale ambao hutamani kuwatupa watoto wao, mimi hakuna hata siku moja nishawahi kuwa na fikra kama hizi. Namshukuru Mungu sana, bora ni uzima na afya yao,” asema Bi Mbodze.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending