Wandani wa Ruto wamtaka Rais atoe agizo kuachiliwa kwa pikipiki 40,000 zilizonaswa
NA MWANGI MUIRURI
WANDANI wa Naibu Rais Dkt William Ruto sasa wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta atoe agizo pikipiki zote zilizokuwa zimenaswa katika msako wa kitaifa ziachiliwe bila masharti.
Mnamo Machi 8, 2022 Rais Kenyatta aliamrisha vitengo vya usalama nchini kuzindua msako huo baada ya genge lililoonekana kujumuisha baadhi ya wahudumu wa bodaboda kumdhulumu kingono mwanadiplomasia wa asili ya Zimbabwe.
Katika kisa hicho cha Machi 4, 2022, mwanadiplomasia huyo wa kike aliripotiwa kuhusika katika ajali ya barabara ambapo alimgonga na kumjeruhi mhudumu wa bodaboda katika barabara ya Forest Road.
Aliposimama ili kusaidia mwathiriwa, genge lilimwandama na katika ukanda wa video uliopachikwa mitandaoni, genge hilo linaonekana likimvuta kiasi cha kumvua nguo huku mkanda wa usalama wa kiti cha dereva ukimnusuru kuvutwa hadi nje ya gari lake.
Raia wengi na watumiaji mitandao ya kijamii walilaani kitendo hicho na Rais alitoa amri kutekelezwe msako wa kitaifa huku nao wanasiasa na miungano ya wahudumu wa bodaboda kwa pamoja walisema msako huo unaumiza vijana wengi wasio na hatia. Hatimaye operesheni hiyo kali ilisitishwa.
Sasa, Seneta wa Murang’a Dkt Irungu Kang’ata anamtaka Rais atangaze pia kuwa “pikipiki zilizokuwa zimenaswa ziachiliwe bila masharti yoyote.”
Alisema kuwa takwimu za idara ya polisi hadi Machi 12 zilionyesha kwamba pikipiki 40,136 zilinaswa katika msako huo wa siku nne.
Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi (DIG) Bw Edward Mbugua alikuwa ametoa mwongozo kwamba wanabodaboda wasakwe kijumla na kila siku maafisa nyanjani wawe wakimtumia ripoti kuhusu idadi ya waliokamatwa, waliozuiliwa, walioshtakiwa, waliopigwa faini na kiwango gani na pia idadi ya pikipiki zitakazonaswa.
Bw Kang’ata alisema kuwa kwa sasa “hakuna haja ya kubagua wahudumu hao kisheria kwa kuwa ikiwa amri ya kusakwa iliwalenga wote, basi hata afueni inafaa kuwalenga wote.”
Mwenyekiti wa vuguvugu la vijana wa United Democratic Alliance (UDA) katika Kaunti ya Murang’a Bw Mixson Warui alisema kuwa “kila pikipiki iliyonaswa katika msako huo inadaiwa hongo ya kati ya Sh20,000 na Sh50,000.”
Alisema kuwa wengi wa wahudumu ambao pikipiki zao zimenaswa walikuwa wamezinunua kwa mikopo na kwa sasa kuzuiliwa kwazo kunawazamisha katika hatari ya kupigwa mnada na hatimaye kuhukumiwa kuwa muflisi.
Mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua aliteta kwa Taifa Leo kuwa “sasa inaonekana Rais Kenyatta amechanganyikiwa kisiasa na kazi yake imegeuka kuwa ya malumbano.”
Alisema kuwa rais alinoa kwa kuhukumu wanabodaboda wote nchini kama walioteua kundi la kufika Nairobi ili kumdhulumu mwanadiplomasia huyo.
“Sio suala la kuhitaji utafiti kujua kwamba serikali ya Rais Kenyatta iko katika vita na masikini wake. Sera za serikali ya Rais Kenyatta haswa katika awamu hii ya pili mamlakani imekuwa ya kupiga masikini vita kupitia kuwafungia uchumi, kuwaimbia madawa ya kutibi Covid-19, kuchoma bidhaa kwa msingi wa kupambana na biashara za magendo na pia kuwabomolea vibanda vya kibiashara sambamba na makao,” akasema.
Alimtaka Rais sasa kutangaza kwamba “pikipiki zote zilizokuwa zimenaswa katika msako huo haramu ziachiliwe bila masharti na maafisa wa polisi wakumbushwe kuwa wao ni idara ya kikatiba ambayo haifai kushinikizwa kwa miongozo haramu kupiga masikini wa nchi vita vya kisiasa na kiuchumi.”
Seneta wa Nakuru Bi Susan Kihika alisema kwamba “kwa sasa serikali imejipa nembo ya uhaini dhidi ya sheria na wananchi.”
Alisema kwamba wandani wa Dkt Ruto watazindua harakati za kuwashinikiza maafisa wa polisi kuachilia pikipiki zote zilizo mikononi mwao.
“Hii ni serikali ambayo itakumbukwa kwa ujasiri wake wa kukaidi sheria. Isipokuwa ni ujasiri sawa wa mahakama ambao umekuwa ukitukinga kutokana na ukaidi huo, tungekuwa na taifa la utundu unaonezwa na serikali,” akasema.
Katika hali hiyo, Bi Kihika alisema kwamba ikibidi, wandani wa Dkt Ruto watatafuta ilani ya mahakama ya kushurutisha kuachiliwa kwa pikipiki hizo.
Hata hivyo, Mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi alilalamika kuwa “suala hili halifai kupewa sura ya kisiasa.”
Alisema kwamba kunafaa kuwe na uwiano wa kitaifa wa kuzima uhuni uliokita mizizi katika sekta ya bodaboda.
“Maovu yaliyo ndani ya sekta hii ni mengi mno kiasi kwamba wengi wa Wakenya wanawaona baadhi yao kama magaidi. Kuna wengi wao wazuri na kuna wachache waovu. Hao wachache ndio tunafaa tutafute mbinu ya kuwaandama kisheria pasipo kulumbana kisiasa,” akasema.
Hata hivyo, aliyekuwa gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu aliteta kuwa kazi ya kuwasaka wahalifu sio ya Rais Kenyatta.
“Rais anafaa tu kutoa mwongozo rasmi kupitia kikao na vyombo vya kiusalama kwamba usalama udumishwe. Lakini Rais aliamka, akakimbia kwa vyombo vya habari na akatangaza kwamba anehukumu sekta yote ya bodaboda kuwa ya ujambazi. Akaamrisha wote wanaswe. Kwa kawaida, polisi wakipewa amri za aina hiyo, huwa wanazindua misururu ya udhalimu wa kujipa hongo,” akasema.
Bw Waititu alisema kwamba sio ajabu kuona hali ambapo Rais alitengwa na wadau wote na akabakia kwa aibu ya kujaribu kurekebisha hali wakati mambo yashaenda mrama.