Connect with us

General News

Wandani wakaidi Raila – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wandani wakaidi Raila – Taifa Leo

AZIMIO: Wandani wakaidi Raila

Na WAANDISHI WETU

MIZOZO na mivutano ya ndani kwa ndani katika vuguvugu la Azimio la Umoja inatishia kuvuruga mikakati ya kumpigia debe kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti.

Mizozo hiyo inahusu ubabe wa kisiasa baina ya wanasiasa washirika wa Odinga, hali ya kutoaminiana baina ya baadni ya viongozi na utata kuhusu maandalizi ya shughuli za mchujo miongoni mwa vyama washirika.

Hii ni licha ya Bw Odinga kuonya dhidi ya kampeni za wanasiasa binafsi kabla mchujo rasmi kuanza. Wadadisi wasema, kiongozi huyo wa ODM alihofia kwamba, huenda baadhi ya wawaniaji wakatumia jina lake visivyo kujivumisha wanaposaka viti tofauti kabla ya kuidhinishwa rasmi na vyama washirika katika Azimio. Katika eneo la Ukambani, kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, yuko kwenye njiapanda ya kisiasa kufuatia juhudi za washirika wa Bw Odinga kumsukuma kutoka vuguvugu hilo.

Washirika wa Bw Odinga wanaoonekana kumpiga vita ni magavana Charity Ngilu (Kitui), Dkt Alfred Mutua (Machakos) na Prof Kivutha Kibwana (Makueni).

Jumatano, magavana hao watatu walianza kampeni za pamoja kumvumisha Bw Odinga katika Kaunti ya Makueni, wakimtaja kama kiongozi atakayeifaa jamii ya Akamba kimaendeleo.

Ingawa watatu hao walimrai Bw Musyoka kujiunga na vuguvugu hilo, wadadisi wanasema mwamko mpya wa magavana hao ni pigo kubwa kwa Bw Musyoka, kwani hilo linamnyima usemi na ushawishi wa kisiasa aliokuwa nao katika eneo hilo mbeleni.

“Ni wazi kuwa muungano wa magavana hao watatu umefifisha ushawishi wa Bw Musyoka kisiasa,” asema Bw Mutie Musau, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Katika Kaunti ya Kilifi, mizozano kati ya Chama cha ODM na Pamoja African Alliance (PAA) ilizidi wiki hii huku wandani wa Bw Odinga wakijiandaa kwa mikutano ya Azimio La Umoja ukanda wa Pwani. Wanachama wa ODM katika Kaunti ya Kilifi walishikilia kuwa, wenzao wa PAA hawatakikani kuhudhuria mikutano hiyo.

Kulingana nao, chama hicho kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kinataka kudandia umaarufu wa Bw Odinga kwa kumuunga mkono kwa urais ilhali kitashindana na wagombeaji viti vingine vya kisiasa na ODM.

Wafuasi wa PAA walikuwa tayari wameandaa mabango ya kumkaribisha Bw Odinga Kilifi. Bw Kingi alisema alishtushwa na misimamo mikali ya wafuasi wa ODM dhidi yao, akidai alikutana na kinara wa chama hicho Dubai akahakikishiwa kwamba PAA wamealikwa kuhudhuria mkutano huo. Katika eneo la Kisii, afisi ya Kampeni za Bw Odinga jana ilitangaza kufutilia mbali mikutano ya kisiasa iliyokuwa imepangwa kufanyika katika kaunti za Kisii na Nyamira jana na leo.

Ni hatua iliyothibitishwa na Mkuu wa Mawasiliano katika Sekretariati hiyo, Bw Dennis Onsarigo kwenye mahojiano.

Mwekahazina wa Kitaifa wa chama hicho, Bw Timothy Bosire alisema mikutano hiyo imefutiliwa mbali kutokana na sababu zisizoepukika.

Hata hivyo, duru ziliiambia ‘Taifa Leo’ kuwa hatua hiyo ilichangiwa na mivutano baina ya Gavana James Ongwae wa Kisii na mbunge Simba Arati (Dagoretti Kaskazini), anayelenga kuwania ugavana katika kaunti hiyo kwa tiketi ya ODM.

Ripoti za Wanderi Kamau, Pius Maundu, Maureen Ongala,Ruth Mbula na Rushdie Oudia