Wanjigi atimuliwa katika OKA akishukiwa kuwa fuko wa Ruto
Na JUSTUS OCHIENG
MFANYABIASHARA Jimi Wanjigi ameondolewa katika mazungumzo ya vinara wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kufuatia madai kwamba ni fuko wa Naibu Rais William Ruto.
Bw Wanjigi amekuwa akimshambulia Kiongozi wa ODM Raila Odinga katika mikutano ya kisiasa ya OKA iliyofanyika majuzi katika kaunti tatu za Ukambani akimtaja kama msaliti.
Bwanyenye huyo alisaidia kampeni za uliokuwa muungano wa NASA katika uchaguzi mkuu wa 2017 ambao Bw Odinga alikuwa mgombeaji urais huku kiongozi wa Wiper, ambaye ni mmoja wa vinara wa OKA Kalonzo Musyoka akiwa mgombea mwenza.
Alitofautiana na Bw Odinga baada ya handisheki ya waziri mkuu huyo wa zamani na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, 2018.
Jana Jumatano, Taifa Leo ilibaini kwamba mfanyabiashara huyo aliondolewa kutoka mazungumzo ya OKA baada ya baadhi ya wanachama kuelezea wasiwasi wao kuhusiana na matamshi yake ya kumshambulia Bw Odinga.
Vinara wa OKA, Jumatano walitia saini rasmi mkataba wa kushirikiana na kujipatia fursa ya kuzungumza na washirika wengine walio na msimamo sawa na wao kwa lengo la kuunda muungano mpana kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Vinara hao Bw Musyoka (Wiper), Gideon Moi (Kanu), Cyrus Jirongo (UDP) na Martha Karua (Narc-Kenya) walitia saini mkataba huo katika hafla iliyoshuhudiwa na maafisa wa vyama vyao iliyofanyika Stephen Kalonzo Musyoka (SKM) Command Centre, Karen, Nairobi.
Bw Wanjigi hakuhudhuria hafla hiyo.
Alipoulizwa kwa nini Bw Wanjigi hakuwa kwenye hafla hiyo, Bw Musyoka alisema kwamba, mfanyabiashara huyo ni mwanachama wa chama cha ODM cha Bw Odinga na hivyo hakuwa kinara wa OKA.
“Wanjiigi hayuko hapa hadi wasuluhishe masuala yao katika ODM,” Bw Musyoka alisema.
Lakini Bw Wanjigi alipoulizwa kuhusiana na madai ya kuwa fuko wa Dkt Ruto katika OKA alishangaa na kusema hakuwa mwanachama wa muungano huo.
“Nimewahi kuwa katika OKA kweli?” alihoji.