Wapinzani wadai Nassir ni Joho mpya
NA WINNIE ATIENO
SIKU chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga kumwidhinisha Mbunge wa Mvita Bw Abdulswamad Nassir kugombea ugavana wa Mombasa, wapinzani wake wameanza kumpiga wakisema hafai.
Wiki iliyopita, Bw Kenyatta na Bw Odinga waliingilia mzozo wa kumsaka mrithi wa Bw Hassan Joho baada ya juhudi za ODM kushurutisha Bw Nassir na mpinzani wake mfanyabiashara Suleiman Shahbal kuafikiana kugonga mwamba.
Wawili hao walikuwa wanazozania tikiti ya ODM ili kugombania nayo ugavana.
Hata hivyo, Bw Nassir na Bw Shahbal wakaitwa kwenye mkutano na kinara wao wa ODM ambapo mfanyabiashara huyo alikubali kumwachia mpinzani wake baada ya maafikiano ambayo yalimhusisha Rais Kenyatta na Bw Odinga ili kuleta mapatano.
“Tulikuwa tumejitayarisha kumenyana na Bw Shahbal ambaye hata hivyo tungembwaga kwenye debe. Lakini sasa Bw Nassir ameidhinishwa na Rais na Bw Odinga tutapambana naye. Lakini tunawasihi wakazi wasikubali kutawaliwa na familia ya kina Hassan Joho utawala wa Bw Nassir utakuwa uendelezaji wa serikali ya Bw Joho,” alisema Bw Hassan Omar.
Bw Mbogo ambaye ni mbunge wa Kisauni anayegombea ugavana kupitia tikiti ya Wiper alisema kuidhinishwa kwa Bw Nassir sio tishio kwake.
Alisema atakutana na Bw Nassir kwenye debe akiongeza kuwa ana imani atashinda.
Hata hivyo, kwenye kikao na wanahabari katika eneo la Treasury Square, wawakilishi wa wadi za Mombasa walimshutumu Bw Omar kwa kutomheshimu Bw Nassir.
“Kama Bw Nassir ni kikaragosi cha Bw Joho, si wewe ni kikaragosi cha Naibu wa Rais, William Ruto? Bw Omar hutojibiwa na Gavana Joho wala Bw Nassir. Sababu hawawezi kushuka hadhi yako sisi tutakujibu, lakini sababu ni Ramadhan hatutaki matusi, tuwe na heshima,” alisema diwani maalum Bi Fatma Kushe.
Walisema watampigia debe Bw Nassir mpaka atangazwe mshindi kwenye uchaguzi wa Agosti 9.
“Bw Nassir ni gavana mtarajiwa, heri uanze kujitayarisha na mapema. Tutakuonyesha kivumbi kama kile ulikiona 2013 na 2017 wakati wa Bw Joho. Kwanza unamdanganya Bw Ruto utamzolea kura na hufanyi kampeni, Mombasa ni ngome ya ODM,” alisema Bi Kushe.
Walimsifu Bw Nassir wakisema uongozi wake umejaribiwa. Walimpa changamoto Bw Omar kuwaeleza wakazi alichokifanya alipokuwa seneta.
“Mshukuru Bw Ruto kwa kukufufua kisiasa manake ulikuwa umekwisha hata wakazi wa Mombasa walisahau uliwahi kuwa seneta. Badala ya kukampeni na kuuza sera, unazungumza kuhusu mwanamume mwenzako, hivyo ndio unamsaidia Bw Ruto?” aliuliza Bi Kushe.
Mwakilishi wa wadi ya Tudor Bw Tobias Samba alimwambia Bw Omar kuacha kulia mapema huku mwenzake wa Likoni Bw Athman Mwamiri akimsihi kuheshimu mwezi wa Ramadhan.
Next article
Wingi wa washindani wa ugavana Vihiga wavurugia ANC hesabu