Connect with us

General News

Wasaka kazi ya uzeeni 2022 – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

WANDERI KAMAU na LEONARD ONYANGO

HUKU mashindano ya kuingia Ikulu baadaye mwaka ujao yakionekana kuwa baina ya ‘farasi’ wawili, orodha ya wawaniaji wanaoaminika kuwa wasindikizaji inazidi kuwa ndefu.

Kulingana na Naibu wa Rais William Ruto, yeye na kinara wa ODM Raila Odinga ndio wana nafasi bora ya kuibuka washindi katika kinyang’anyiro cha urais mwaka ujao.

“Tayari mwelekeo wa kinyang’anyiro cha urais 2022 umejulikana. Ushindani utakuwa baina yangu na ‘mradi wa Rais Kenyatta’,” akasema Dkt Ruto alipokutana na wafanyabiashara kutoka eneo la Githurai nyumbani kwake mtaani Karen, Nairobi, Alhamisi.

Jana Ijumaa, Dkt Ruto aliyekuwa akizungumza katika msururu wa mikutano ya kisiasa katika Kaunti ya Kakamega, alielezea imani yake kwamba atambwaga Bw Odinga.

Alisema kuwa ataweka mikakati ya kutosha kuhakikisha kuwa serikali ‘haiibi’ kura zake.

Mbali na kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka walio na angalau ushawishi wa kisiasa katika ngome zao na maeneo kadhaa nchini, zaidi ya watu 10 wametangaza kuwania urais mwaka ujao licha ya kukosa uungwaji mkono nchini.

Maswali yameibuka kuhusu lengo la wawaniaji hao, ikizingatiwa wengi wao hawana uungwaji mkono hata katika maeneo wanakotoka.

Miongoni mwao ni Maseneta Gideon Moi (Baringo) na Moses Wetang’ula (Bungoma), Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi wa Bunge la Kitafa, Gavana wa Machakos Alfred Mutua (Machakos) na aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo.

Wengine ni mfanyabiashara Jimi Wanjigi, waziri wa zamani Dkt Mukhisa Kituyi, Gavana wa Migori Okoth Obado, mwanamuziki wa Injili Reuben Kigame, Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria, aliyekuwa kiongozi wa Kanisa la PCEA Dkt David Githii, Gavana wa Makueni Prof Kivutha Kibwana na mwanasheria Prof George Wajackoya.

Kiongozi wa Kanu Bw Moi alizindua rasmi azma yake kuwania urais Septemba 30, mwaka huu.

Bw Moi ambaye ni mmoja kati ya vigogo wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA), aliahidi kuboresha uchumi na kukabiliana na ufisadi. Bw Moi amekuwa akionekana kuegemea mrengo wa Bw Odinga.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanatabiri kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwamba Seneta Moi hatawania urais mwaka ujao na badala yake ataunga mkono Bw Odinga.

Japo kiongozi wa Ford Kenya Bw Wetang’ula ametangaza kuwania urais mwaka ujao, ameanza harakati za kutetea kiti chake cha useneta wa Kaunti ya Bungoma.

Bw Wetang’ula amehudumu kama mbunge tangu 1992 na kama waziri wa Mashauri ya Kigeni katika serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki. Amekuwa Seneta wa Bungoma tangu 2013.

Wasaka kazi ya uzeeni 2022 – Taifa Leo
Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula. Picha/ Maktaba

Spika Muturi ambaye jana alikuwa katika eneobunge la Ugenya nyumbani kwa aliyekuwa msemaji wa polisi Charles Owino, ametangaza kuwania urais kupitia chama cha Democratic Party (DP).

Lakini uwepo wa mbunge wa eneo hilo, David Ochieng, na aliyekuwa Nicholas Gumbo – ambao wote ni mwasi wa ODM – kunaashiria kwamba huenda Bw Muturi ameanza harakati za kusaka viongozi atakaoshirikiana nao mwaka ujao.

Alihudumu kama mbunge wa Siakago, Kaunti ya Embu, kati ya 1999 na 2007. Amekuwa Spika tangu 2013.

Wadadisi wanasema Bw Muturi ametangaza kuwania urais ili kuongeza nafasi yake ya kuteuliwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga au Dkt Ruto.

Gavana wa Machakos Dkt Mutua analenga kuwania urais kwa tiketi ya chama chake cha Maendeleo Chap Chap (MCC). Alihudumu kama Msemaji wa Serikali wakati wa Serikali ya Muungano kati ya Bw Kibaki na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Dkt Mutua ambaye ana uungwaji mkono katika Kaunti ya Machakos pekee, amekuwa gavana wa Machakos tangu 2013.

Dkt Mutua anaunga mkono Bw Odinga na amekuwa akimshambulia Bw Musyoka ambaye ametangaza kuwa hataunga mkono kiongozi wa ODM kwa mara ya tatu.

Bw Kabogo ambaye ni kiongozi wa chama cha Tujibebe Wakenya Party (TWP), alihudumu kama mbunge wa eneo la Juja kati ya 2002-2007 na 2010-2013 na gavana wa Kiambu kati ya 2013-2017.

Alhamisi, Bw Kabogo alikuwa miongoni mwa viongozi waliomkaribisha Bw Odinga katika Kaunti ya Kiambu. Bw Kabogo aliahidi kuhakikisha Bw Odinga amepata uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya.

Bw Wanjigi ambaye ametangaza kuwania urais kupitia tiketi ya ODM, amewaacha wadadisi wa masuala ya kisiasa wakijikuna kichwa kung’amua anacholenga.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna hivi majuzi alisema wanashuku hatua ya Bw Wanjigi kufungua afisi za chama katika maeneo mbalimbali bila kuhusisha viongozi.

Baadhi ya wadadisi wanaamini kuwa Bw Wanjigi anatumiwa na ODM kupenyeza chama hicho katika eneo la Mlima Kenya ambapo amefungua afisi kadhaa.

Dkt Kituyi alikuwa akihudumu kama Katibu Mkuu wa Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) kabla ya kujiuzulu mwanzoni mwa mwaka huu ili kuwania urais.

Bw Obado ametangaza kuwania urais lakini mapema mwezi huu, alikuwa mwenyeji wa Dkt Ruto – hali ambayo imefanya wengi kuamini ameingia katika kambi ya Naibu wa Rais.

Kwa upande wake, Bw Kigame atatumia chama cha Federal Party of Kenya (FPK) na hajakuwa akiendesha kampeni.

Gavana wa Iria atatumia chama cha Usawa kwa Wote Party (UKWP) humu Prof Kibwana akitumia chama chake cha Muungano.

Dkt Githii bado hajatangaza chama atakachotumia kuwania.

Wadadisi wanasema baadhi ya wawaniaji hao hawana haja ya kushinda urais bali wanajitafutia umaarufu kisiasa na wanalenga kuteuliwa kwenye nyadhifa kuu serikalini baada ya uchaguzi wa 2022.

“Baadhi ya wawaniaji wanafahamu kwamba hawana hata uungwaji mkono wa kisiasa katika maeneo wanakotoka. Wengine waliwahi kuwania nyadhifa kama ubunge na wakashindwa. Ni wazi wana malengo fiche wanapotangaza azma za kuwania urais,” asema Bw Mark Bichachi, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Bw Martin Andati, mdadisi wa siasa, anasema kuwa baadhi yao wanalenga kuteuliwa kuwa wawaniaji wenza.

“Wawaniji wengi wanafanya kila wawezalo kuhakikisha hawapo nje ya ulingo wa kisiasa, hata kama hatataibuka washindi kwenye uchaguzi huo,” asema mdadisi wa wa siasa Martin Andati.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending