Connect with us

General News

Washukiwa 3 walivyohepa gereza Kamiti – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Washukiwa 3 walivyohepa gereza Kamiti – Taifa Leo

Washukiwa 3 walivyohepa gereza Kamiti

Na MARY WAMBUI

WAFUNGWA watatu waliotoroka kutoka gereza lenye ulinzi mkali la Kamiti, Kaunti ya Kiambu walisaidiwa kuhepa kupitia lango kuu, uchunguzi umeonyesha.

Kulingana na upelelezi wa Taifa Leo, shimo linalodaiwa watoro hao walitumia kutoroka jela ni dogo na haliwezi kutoshea kichwa au mwili wa binadamu.

Taifa Leo imebaini kwamba, mwanya ulioko katika Jengo A6 ambapo watatu hao walikuwa wakizuiliwa ni mwembamba mno na haiwezekani kwamba, wafungwa hao waliutumia kuhepa.

Hiyo inamaanisha kwamba, mahabusu hao, Musharaf Abdalla Akhulunga, 34, maarufu Zarkawi au Alex au Shukri, Mohamed Ali Abikar, 22, na Joseph Juma Odhiambo maarufu Yusuf, 30, walihepa kupitia lango kuu la gereza hilo.

Watatu hao walikuwa wamefungwa katika jela moja na Egilva Bwire aliyeachiliwa huru Oktoba baada ya kukamilisha kifungo chake cha miaka 10.

Bwire alitoweka saa chache baada ya kuachiliwa huru kutoka Gereza la Kamiti.

Bwire ni miongoni mwa washukiwa watano wa ugaidi ambao serikali imetangaza zawadi ya Sh60 milioni kwa yeyote atakayetoa habari za kusaidia kuwanasa.

Uchunguzi wa Taifa Leo pia umebaini kuwa, mfungwa wa nne aliyekuwa na watatu hao waliotoweka, alikataa kutoroka na wenzake.

Taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa Magereza nchini Wycliffe Ogallo, Jumatatu, ilisema kuwa, watatu hao walipitia kwenye mwanya ulio kwenye Jengo A6.

Lakini mahojiano yaliyofanywa na maafisa mbalimbali gerezani humo, yamebaini kwamba njama ya kutoroka kwa watatu hao ilipangwa kwa muda mrefu.

Gereza la Kamiti ni kati ya taasisi zilizo na ulinzi mkali nchini.

Vile vile, ndio makao ya wahalifu sugu, wakiwemo magaidi na wauaji.

Majengo yanayotumika kuzuilia wafungwa yamezingirwa na ukuta mrefu kuzuia wafungwa kuruka.

Gereza hilo pia limewekewa kamera za CCTV katika kila kona na liko chini ya ulinzi mkali wa maafisa waliojihami usiku na mchana.

Hiyo inamaana kuwa haingewezekana kwa mahabusu hao kutoroka bila usaidizi wa walinzi gerezani humo.

Jumanne, serikali ilisema walinzi saba wa gereza la Kamiti wamekamatwa kwa madai ya kusaidia wafungwa hao kutoroka.

Baadhi ya walinzi walidai wafungwa hao walisokota kamba ndefu kwa kutumia blanketi zao na kisha kuitumia kupanda ukuta.

Ripoti zinaonyesha kuwa kamera za CCTV zinazomulika eneo linalodaiwa kutumiwa na mahabusu hao kuhepa, zilipatikana Jumatatu zikiwa zimeharibiwa.

Waziri wa Usalama Fred Matiang’i Jumatatu usiku alisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kwamba taarifa zilizotolewa kuhusu namna mahabusu hao walitoroka, zilikuwa za kupotosha.

“Tumezuru eneo ambapo mahabusu hao wanadaiwa kupitia lakini hatujaridhika. Sitaki kufichua mengi ili nisije nikatatiza uchunguzi unaoendeshwa na maafisa wa DCI,” akasema Dkt Matiang’i alipozuru gereza hilo.

Waziri Matiang’i ambaye alikuwa ameandamana na Katibu wa Wizara ya Usalama Karanja Kibicho, Katibu wa Huduma za Kubadili Tabia Zeinab Hussein, Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai na Mkurugenzi wa DCI George Kinoti, alisema maafisa wa usalama wameimarisha ulinzi katika maeneo ya mpakani kuhakikisha maabusu hao hawatorokei nchi jirani.

Maafisa wa magereza waliokuwa likizoni wameagizwa kurejea kazi mara moja.

“Tutahakikisha wahalifu hao wanasakwa kwa nguvu zote. Tutawapata,” akasema Dkt Matiang’i.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending