Connect with us

General News

Wasiwasi wakongwe wakitakiwa kuhama – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wasiwasi wakongwe wakitakiwa kuhama – Taifa Leo

Wasiwasi wakongwe wakitakiwa kuhama

NA MAUREEN ONGALA

WAZEE waliookolewa kutokana na mauaji wakidaiwa kuwa wachawi katika Kaunti ya Kilifi, sasa wanaishi kwa hofu baada ya kubainika makao ambayo walipewa hifadhi salama yamepangiwa kuuzwa.

Kwa zaidi ya miaka 13, wazee walipata usalama katika kituo cha Kaya Godhoma katika kijiji cha Forodhoyo, eneobunge la Ganze.

Huku visa vya mauji ya wazee kwa tuhuma za uchawi vikiendelea kushuhudiwa katika Kaunti ya Kilifi, imefichuka familia ya mmoja wa wahisani waliojitolea kuwapa makao hapo, inataka kuuza shamba hilo.

Wazee hao wamepewa makataa ya hadi mwisho wa juma hili kutafuta sehemu mbadala ya kuishi.

Akizungumza na Taifa Leo, mwenyekiti wa kituo cha Kaya Godhoma, Bw Emmanuel Katana, alisema juhudi za kuisihi familia hiyo kuwapa muda zaidi wa kutafuta pesa ziligonga mwamba.

Kituo hicho kilijengwa katika ekari 12 ya shamba ambalo lilikuwa kichaka awali.

“Mwenye shamba anahitaji kuuza na hatuna pesa. Tunatoa wito kwa mashirika na serikali ili tupate msaada kununua ile sehemu ili kuendelea na shughuli zetu za kuwaokoa wazee. Tulitazamia kutafuta pesa na kununua takriban ekari tatu lakini familia hiyo imedinda na kusema kuwa iwapo tungetaka kubaki hapo tununue shamba lote ekari 12,” akasema.

Kulingana na Bw Katana, shamba hilo linauzwa kwa sh175,000 kwa ekari moja kwa hivyo watahitaji Sh2.1 milioni kununua ekari zote 12.

“Tushapewa ilani tuwaondoe wazee wetu na pia tusitishe shughuli zote tunazofanya katika kituo hicho,” akasema.

Bw Katana alisema kuwa wamewasilisha maombi katika serikali ya kaunti na ya kitaifa kupitia kwa ofisi ya Mbunge wa Ganze, Bw Teddy Mwambire, ambaye aliahidi kulishughulikia suala hilo.

“Kituo hicho ndicho usalama wetu na pia wa wazee wetu. Tukiondolewa leo tutaenda wapi?”akauliza.

Bw Katana alisema kuwa iwapo wazee hao watafurushwa kutoka kituo hicho watakuwa hatarini.

Hata hivyo, Bw Katana alisema wanaendeleza mazungumzo na familia za wazee waliookolewa na kituo hicho ili jamaa zao wakubali warudi nyumbani na kuwatunza.

Alisema kuwa licha ya kuwa idadi ya wazee wanaoishi kwa muda imepungua, wazee wengi hukimbilia kituo hicho na huishi kwa muda majadiliano yakiendelea na mwishowe familia zao huwakubali tena.

Katika visa vya hivi majuzi, baadhi ya wazee wa kike wanaoshukiwa kuwa wachawi kutoka maeneo ya Tezo na Ngerenya, walitoroka nyumbani kwao na kutafuta usalama kwa jamaa wao wengine baada ya kutishiwa kuuawa.

Kamanda wa Kaunti ya Kilifi, Bw Nelson Taliti, alisema kuwa wazee 145 wenye umri wa miaka 50 kuendelea waliuawa kutoka mwaka wa 2019 hadi 2021.