Watawanywa kwa vitoa machozi huku wakidai haki
ANTHONY KITIMO na CECIL ODONGO
POLISI JANA walitumia vitoa machozi kuwatawanya baadhi ya Waislamu waliokuwa wamekusanyika katika uga wa Makadara kwa swala maalum, ya kuombea na kulalamikia kutoweka kwa watu wanaoshukiwa kuhusika na ugaidi.
Waumini hao waliokuwa wakiimba Allahu Akhbar (Mungu ni Mkuu) walizua vurugu polisi walipojaribu kuzuia ibada hiyo isiendelee.Ililazimu mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir pamoja na Mkurugenzi wa Haki Afrika, Hussein Khalid, kuingilia kati kudhibiti hali.
Baada ya majadiliano ya kina kati ya MaBw Nassir na Khalid kwa upande moja na Mkuu wa Polisi Joseph Ongaya upande mwingine, iliamuliwa kwamba maombi yaendelee nje ya msikiti wa Baluchi ndipo maandamano yasifanyike.
Kundi hilo la waumini lilitimuliwa mara tu baada ya maombi hayo kutamatika, huku maafisa wa usalama wakizingira uwanja huo ili kuzuia yeyote asiingie ndani.Baada ya ibada Bw Abdulrahaman Said, nduguye Muhamad Abubakar, 22, maarufu kama Minshawary, aliwalaumu maafisa wa polisi kwa kuhusika na kutoweka kwa ndugu yake.
Bw Abubakar amehusishwa na kundi la kigaidi la Al-Shabaab huku polisi wakiahidi kumtunuku Sh10 milioni raia yeyote anayefahamu aliko. “Naomba maafisa wa polisi wawaachilie huru wale wote ambao wamekuwa wakiwazuilia akiwemo ndungu yangu.
“Tuna orodha ya zaidi ya watu 43 na kuna hofu kwamba idadi hiyo imekuwa ikiendelea kupanda,” akasema Bw Said.Bw Abubakar, ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu, anasemekana kutekwa nyara na watu wanaodaiwa kuwa maafisa wa polisi, ambao walikuwa na bunduki mnamo Oktoba 14.
Alichukuliwa juu juu katika mtaa wa Majengo baada ya kuhudhuria maombi ya jioni (Ishaa) katika msikiti wa Masjid Ashar saa mbili unusu usiku.Tangu wakati huo, mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Umma hajaonekana hadharani.
Wiki hii familia yake ilishangaa kufahamu kwamba alikuwa mshukiwa wa ugaidi, ambaye alirejelewa na Idara ya Polisi kama aliyejihami vikali. Bw Muhamad ni kati ya washukiwa wengine wanne ambao Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) Bw George Kinoti ametoa ahadi, ya kumpa mtu yeyote atakayetoa habari kuhusu mahali alipo, zawadi ya Sh10 milioni.
Washukiwa wengine ambao idara ya polisi inawaandama ni Elgiva Bwire Oliacha alias Seif Deen, Barigi Abdikadir Haila, Trevor Ndwiga alias Idriss Jamal na Salim Rashid Mohamed.Bw Nassir naye alikashifu maafisa wanaohusika na utekajinyara huo wa washukiwa wa ugaidi badala ya kuwapeleka kortini.
Bw Khalid aliunga mkono wito huo na kusema maandamano yao ni moja ya njia zitakazosukuma serikali kusikiza kilio chao, na kuchukua hatua dhidi ya maafisa wanaohusika na kutoweka kwa watu hao.Wakati huo huo, Shirika la Kiislamu la Hizb UT Tahrir limeungana na mashirika mengine ya Waislamu kukashifu vyombo vya uslama kwa kuendeleza visa vya kuwateka Waislamu wanaotuhumiwa kuwa na uhusiano na magaidi.
Next article
NIS yapewa Sh169m kwa siku, Uhuru aagiza vyombo vya usalama…