Connect with us

General News

Watimkaji wa Kenya walivyotamalaki fainali za Diamond League 2021 – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Watimkaji wa Kenya walivyotamalaki fainali za Diamond League 2021 – Taifa Leo

Watimkaji wa Kenya walivyotamalaki fainali za Diamond League 2021

Na CHRIS ADUNGO

MWAKA wa 2021 ulikuwa wa tija na fahari tele kwa wanariadha wazoefu wa Kenya baada ya kutawala vitengo vyote vitano walivyovishiriki katika siku ya pili na ya mwisho ya fainali za mbio za Wanda Diamond League jijini Zurich, Uswisi mnamo Septemba 9, 2021.

Bingwa mara mbili wa Olimpiki katika mbio za 1,500m, Faith Kipyegon, aliendeleza ubabe wake katika fani hiyo kwa kusajili muda wa dakika 3:58.33 na kumpiku Mholanzi Sifan Hassan (3:58.55) aliyeshinda dhahabu za Olimpiki katika 5,000m na 10,000m.

Sawa na washindi wa vitengo vyote vingine, Kipyegon, 27, alituzwa taji la Diamond Trophy na akatia mfukoni Sh3 milioni. Nambari mbili aliridhika na Sh1.2 milioni huku nambari tatu na nne wakijizolea Sh700,000 na Sh400,000 mtawalia.

“Nilijivunia msimu wa kuridhisha sana mwaka huu wa 2021. Kubwa zaidi lililofaulu kufanya ni kumbwaga Sifan. Hilo halikuwa jambo rahisi,” akasema Kipyegon kwa kufichua azma ya kuanza kunogesha pia mbio za 5,000m – fani ambayo imekuwa ikitawaliwa sana na Hellen Obiri aliyestaafu mwaka huu na kuhamia mbio za masafa marefu za marathon na nusu-marathon.

“Nikiwa mdogo, nilikuwa nikimtazama sana Vivian Cheruiyot. Nilivutiwa na jinsi alivyofaulu kutamba katika fani mbili tofauti za riadha – 5,000m na 10,000m. Nami nina kiu ya kudhihirisha ukubwa wa uwezo wangu katika ngazi nyingine – 5,000m ambapo ninatarajia makuu zaidi mnamo 2022,” akaongeza Kipyegon.

Japo Hassan alitamalaki duru ya Florence Diamond League (Italia) mnamo Juni 10, Kipyegon alilipiza kisasi katika duru ya Monaco (Ufaransa) mnamo Julai 4 kabla ya kuzoa dhahabu kwenye Olimpiki za Tokyo, Japan.

Bingwa wa dunia katika 1,500m, Timothy Cheruiyot, naye alitawala kivumbi hicho kwa upande wa wanaume kwa dakika 3:31.37 na kulipiza kisasi dhidi ya Jakob Ingebrigtsen wa Norway (3:31.45) aliyemzidi ujanja kwenye Olimpiki za Tokyo, Japan.

Hadi walipomenyana kwenye Olimpiki za Tokyo mnamo Agosti, Cheruiyot alikuwa amemshinda Ingebrigtsen mara 12 mfululizo.

Wakenya wengine Ronald Kwemoi (3:33.34), Charles Simotwo (3:34.24) na Bethwell Birgen (3:46.01) waliambulia nafasi za sita, saba na tisa mtawalia.

“Ushindi niliojivunia 2021 ulikuwa wa kimuujiza. Sikuwa nimepona kabisa baada ya kusumbuliwa na jeraha la paja kwa kipindi kirefu msimu huu. Sasa nimeanza kuzamia mazoezi kabambe ili nihifadhi taji la dunia jijini Oregon, Amerika mwaka ujao wa 2022 kwenye Riadha za Dunia,” akasema Cheruiyot.

Mambo yalikuwa shwari pia kwa Wakenya katika mbio za 800m wanaume zilizotawaliwa na bingwa wa Olimpiki, Emmanuel Korir (1:44.56).

Mshindi wa fedha katika Olimpiki, Ferguson Rotich alimaliza wa pili (1:44.96) huku bingwa wa Jumuiya ya Madola, Wycliffe Kinyamal akitupwa hadi nafasi ya nane (1:46.52).

Wakenya walidhihirisha pia ugwiji wao katika mbio za 3,000m kuruka viunzi na maji kwenye fainali hizo za Diamond League. Norah Jeruto na Hyvin Kiyeng aliyeibuka bingwa wa dunia mnamo 2015 walitamalaki kivumbi hicho kwa upande wa wanawake kwa muda wa dakika 9:07.33 na 9:08.55 mtawalia.

Celliphine Chespol (9:10.26), Rosefline Chepngetich (9:21.67) na Purity Kirui (9:38.56) waliambulia nafasi za tano, nane na 10 mtawalia. Fancy Cherono anayejivunia muda bora wa dakika 9:27.20 hakumaliza mbio hizo.

Kwa upande wa wanaume, Benjamin Kigen aliyeshinda medali ya shaba kwenye Olimpiki, alilipiza kisasi dhidi ya Soufiane El Bakkali wa Morocco aliyezoa dhahabu jijini Tokyo. Kigen alisajili muda wa dakika 8:17.45 huku El Bakkali akiridhika na nafasi ya pili (8:17.70).

Abraham Kibiwott alimaliza wa tatu (8:18.16) mbele ya Leonard Bett (8:20.20). Mwakilishi mwingine wa Kenya, Wilberforce Kones anayejivunia muda bora wa dakika 8:21.42 hakukamilisha mbio hizo.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending