Watu wanane waangamia kwenye ajali mbaya Narok
STANLEY NGOTHO Na ROBERT KIPLAGAT
WATU wanane wamefariki na watano kujeruhiwa katika ajali mbaya eneo la TM, kwenye barabara kuu ya Narok-Bomet baada ya trela na matatu kugongana ana kwa ana.
Kamanda wa Polisi eneo hilo, Bw Frederick Shiundu, alisema ajali ilitokea saa sita adhuhuri.
“Dereva wa trela alipofika eneo la tukio tairi ya mbele ya kulia ilipasuka akapoteza usukani,” alisema Bw Shiundu.
Baada ya kushindwa kudhibiti, trela iligongana na matatu ya kampuni ya Ena Coach iliyokuwa ikielekea upande wake.
Watu watano waliangamia papo hapo huku dereva wa matatu aliyejeruhiwa vibaya akifariki dunia alipokuwa akipelekwa hospitalini na wengine watatu wakaaga dunia katika Hospitali ya Rufaa Kaunti ya Narok walipokimbizwa kupokea matibabu.
Wakati huo vilevile Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ameziomba msamaha jamii za Wamaasai na Wakamba kwa mauaji yaliyotekelezwa na polisi eneo la Masimba kwenye barabara kuu ya Mombasa, Alhamisi.
Waziri alisema inahuzunisha kuwa watu wanne walipigwa risasi na kuuawa na polisi katika maandamano ya kulalamikia visa vya wanyamapori kushambulia binadamu na kuahidi kuwa maafisa hao watachukuliwa hatua.
Kikosi maalum cha wapelelezi kutoka Mamlaka ya Kuangazia Utendakazi wa Polisi (IPOA) kilitua Kajiado, Ijumaa asubuhi na kuanzisha uchunguzi unaolenga kubaini ni jinsi gani maafisa wa GSU waliwamiminia risasi waandamanaji ambao hawakuwa wamejihami.
Waandamanaji wanne waliuawa huku wengine watano wakilazwa hospitalini wakiwa na majeraha ya risasi.Walioaga dunia ni Ntidu Tereu, Letomir Topoika, Dennis Matheka na Duncan Kanari Mungei.
Katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Gavana Joseph Ole Lenku pamoja na viongozi katika eneo la Masimba uliohudhuriwa na Katibu wa Wizara Zeinab Hussein, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai na Msimamizi wa Bonde la Ufa Maalim Mohammed, Waziri alisema Rais ameamuru malipo yote ya fidia yaliyosalia kulipwa.
“Fidia iliyosalia ni karibu Sh1.5 bilioni. Rais Kenyatta amenipigia simu kutoka Sweden na kuniagiza tulipe fidia hizi. Kajiado ni moja kati ya kaunti zenye idadi kubwa zaidi ya madai ya fidia kutoka kwa wahasiriwa wa wanyamapori,” alisema Dkt Matiang’i.
Maandamano kutoka kwa wanajamii yalitokana na kuongezeka kwa visa vya mauaji yanayotekelezwa na wanyamapori bila kufidiwa kwa miaka mingi.
Wiki iliyopita, mwalimu katika shule moja ya msingi eneo hilo aliuawa na ndovu.
Dkt Matiang’i vilevile alitangaza kuwa shule zote saba zilizokuwa zimefungwa kwa kuhofia mashambulizi ya wanyamapori zitawekwa ua na kufunguliwa mara moja.
Next article
Madai wizi wa kura yanavyotishia Ruto