Wawaniaji roho mkononi mchujo wa ODM ukianza
CHARLES WASONGA na KENYA NEWS AGENCY
CHAMA cha ODM kinaanza kura ya mchujo Ijumaa huku hofu ikiwa imetanda miongoni mwa wawaniaji kwamba baadhi ya wawaniaji tayari wamepewa tiketi za moja kwa moja.
Kulingana na ratiba iliyotolewa wiki jana na Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya chama hicho, shughuli hiyo itaanza katika kaunti za Nakuru, Turkana, Narok na Kajiado.
Shughuli hiyo itafanyika katika kaunti za Kilifi na Tana River mnamo Jumatatu (Aprili 4), Taita Taveta na Kwale (Aprili 5), Mombasa (Aprili 6), Kisii na Nyamira (Aprili 7), Vihiga na Busia (Aprili 12), Kisumu (Aprili 13) na Siaya (Aprili 14).
Kura hiyo ya mchujo itafanyika katika kaunti za Bungoma na Trans Nzoia mnamo Aprili 15, Migori (AprilI 16), Homa Bay (AprilI 18) na Kakamega (Aprili 19).
Hata hivyo, wagombeaji viti vya udiwani ndio watateuliwa kwa njia ya upigaji kura wa moja kwa moja baada ya mwenyekiti wa NEB Bi Catherine Mumma kutangaza kuwa chama hicho kinapendelea njia za maelewano na kura za maoni.
“Tayari tumegundua kuwa wawaniaji wa viti vya ugavana na ubunge katika maeneo mbalimbali wamekubaliana. Kwa hivyo, upigaji kura hautaendeshwa katika maeneo kama hayo,” Bi Mumma akawaambia wanahabari katika makao makuu ya ODM, Nairobi, Jumanne wiki hii.
Alitoa mfano wa kaunti ya Turkana ambako mfumo wa maelewano umetumika kuamua wagombeaji wa viti vya ugavana, useneta na ubunge.
“Katika kaunti hiyo, ODM itaendesha kura ya mchujo kuamua wagombeaji wa viti vya udiwani pekee kwa sababu wawaniaji wa viti vingine wamekubaliana,” Bi Mumma akaeleza.
Mwishoni mwa wiki jana, chama cha ODM kilitoa tiketi za moja kwa moja kwa baadhi ya wawaniaji wa viti mbalimbali haswa katika ngome zake za Pwani, Magharibi na Nyanza.
Hatua hiyo iliwakera baadhi ya wawaniaji ambao walitishia kukihama chama hicho na kuwania viti husika kama wagombeaji wa kujitegemea.
Kwa mfano, katika Kaunti ya Kwale, chama hicho kimempa tiketi ya moja kwa moja aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Kilimo Hamadi Boga kuwania ugavana wa kaunti hiyo.
Aidha, ODM ilifutilia mbali kura ya mchujo ya ugavana katika Kaunti ya Kakamega na kuamua kumteua aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Ketraco Fernandes Barasa kuwania ugavana katika kaunti hiyo.
Wengine waliopokezwa tiketi za moja kwa moja kutetea viti kwa tiketi ya ODM ni wabunge Tindi Mwale (Butere), Titus Khamala (Lurambi), Christopher Aseka (Khwisero), Emmanuel Wangwe (Navakholo) na Benard Shinali (Ikolomani).
Wakati huo huo, Chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) tawi la Siaya, limetoa wito kwa muungano wa Azimio la Umoja kuondoa pendekezo la kutenga maeneo fulani kwa vyama fulani.
Mwenyekiti wa tawi hilo, Bw Andrew Aduda, alisema chama hicho kitamdhamini Bw Oscar Tony Omondi kuwania useneta wa Siaya , licha ya kaunti hiyo kuwa ngome ya ODM.
Kakake, Kiongozi wa ODM Raila Odinga, Oburu Odinga anapigiwa upatu kupewa tiketi ya ODM kuwania wadhifa huo wa useneta wa Siaya.