CHARLES WASONGA: Wazazi wakumbatie shule nyingine za upili watakazoingia wana wao, si kitaifa tu!
NA CHARLES WASONGA
HUKU uteuzi wa wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Kwanza ukitarajiwa kuanza juma lijalo, kuna hofu kuwa wengine wao watakosa nafasi katika shule za upili walizochagua.
Kutokana na nafasi finyu katika shule za upili za kitaifa zinazochukuliwa kama za kifahari, baadhi ya jumla ya watahiniwa 11,857 waliopata alama 400 na zaidi, bila shaka watajipata wameitwa katika shule nyingine.
Kulingana na mwongozo wa Wizara ya Elimu kuhusu uteuzi wa wanafunzi kujiunga na kidato wale waliopata alama 380 kwenda juu katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) huwa wamehitimu kujiunga na shule za kitaifa.
Japo, Waziri wa Elimu George Magoha wiki alitoa hakikisho kuwa haki na usawa utazingatiwa katika shughuli hiyo, wazazi wengine watavunjika moyo endapo watoto wao watakosa nafasi katika shule walizochagua.
Wazazi kama hao hawafai kuvunjika moyo endapo, kwa mfano, watoto wao watakosa nafasi katika shule za kitaifa zenye majina makubwa kama vile, shule za upili za Kenya High, Alliance, Mang’u, Pangani miongoni mwa nyingine ambazo huandikisha matokeo mazuri katika mitihani ya kidato cha nne (KCSE).
Kuna baadhi ya shule za ngazi za “exta county” au kaunti ambazo huandikisha matokeo mazuri katika KCSE kila mwaka. Mifano shule ya upili ya Orero iliyoko Kaunti ya Homa Bay, Shule ya Upili ya Wavulana ya Ortum iliyoko kaunti ya Pokot Magharibi miongoni mwa shule zingine nyingi.
Wazazi ambao watoto wao walipata alama 400 zaidi waondoe kasumba kwamba mustakabali wa watoto wao kimasomo utavurugika endapo hawatajinga na shule za kitaifa zenuye majina makubwa.
Waelewe kwamba uteuzi wa wanafunzi katika shule za upili, haswa zile za kitaifa, haufanywi kwa kuzingatia idadi ya alama pekee. Kuna vigezo vingine ambavyo Wizara ya Elimu imeweka ili kufikia kanuni ya usawa, haswa wa kimaeneo.
Kwa mfano, juzi Waziri Magoha alifafanua kuwa Wizara yake itahakikisha kuwa imewatendea haki watahiniwa waliofanya KCPE katika maeneo kame nchini, mitaa ya mabanda na katika maeneo mengine yenye changamoto.
Aidha, alisema kuwa uteuzi wa wanafunzi haswa katika shule za upili za kitaifa utazingatia uwakilisha sawa wa kimaeneo nchini.
Kwa mfano, kulingana na Profesa Magoha mtahiniwa aliyepata alama 360 kutoka kaunti kama vile Marsabit, Baringo au Isiolo wataitwa katika shule ya upili ya Kenya na baadhi ya waliopata alama 400 na zaidi wakakosa nafasi hiyo.
Vile vile, ningependa kuwashauri wamiliki wa shule za kibinafsi kwamba wasilaumu Wizara ya Elimu endapo watahiniwa wa shule zao waliopata alama 400 na zaidi wataitwa katika shule za kitaifa zinazochukuliwa kuwa za hadhi ya chini.
Tayari naibu mwenyekiti wa muungano wamiliki wa shule za kibinafsi (KPSA) Solomon Munene umeonya kuhusu kile alichokitaja kama “kupendelewa” kwa watahiniwa kutoka shule za umma na “kubaguliwa” kwa wenzao waliosomea katika shule za kibinafsi.
Ni kweli kwamba wanafunzi wanaosomea katika shule za kibinafsi na wale wanaosomea shule za umma wote ni watoto wa Wakenya, wanavyodai wamiliki wa shule za kibinafsi.
Lakini ukweli mwingine ni kwamba Wizara ya Elimu ina wajibu wa kuhakikisha kuwa shule za kitaifa zina sura ya kitaifa; kwamba wanafunzi wanateuliwa kujiunga nazo wanatoka pembe zote za nchini.