SHINA LA UHAI: Mwaka mpya 2022 kauli mbiu: Wekeza katika afya
Na PAULINE ONGAJI
KUUNDA mfumo mpya thabiti wa kiafya ndio ujumbe uliotawala kongamano la kwanza la kimataifa kuhusu afya ya umma (CPHIA 2021) juma lililopita.
Hafla hiyo iliyoandaliwa na Muungano wa Afrika (AU) na kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia maradhi barani Afrika (Africa CDC), kati ya Desemba 14 na Desemba 16 2021, ilihusisha mawasilisho kutoka marais wa Afrika, viongozi wakuu na wataalamu wa kiafya, waliozungumzia jinsi ya kukabiliana na maradhi ya COVID 19 na mkondo mpya wa kufuata ili kuimarisha afya ya umma barani.
Jambo kuu lililoibuka kwenye kongamano hilo lilikuwa kwamba kiwango cha huduma ya afya barani kingali chini, na hiyo sharti kuwe na utaratibu mpya wa kuhakikisha kwamba sekta ya afya imeimarishwa.
Lakini ingawa waandalizi wa kongamano hilo waliridhishwa na maandalizi, vile vile kiwango cha juu cha ushiriki kwenye kongamano hilo, lazima itiliwe mkazo kwamba suala la mikutano kuandaliwa ili kujadili hali ya huduma ya afya hapa barani Afrika, sio geni.
Kwa mfano, kabla ya hapa kulikuwa na Azimio la Abuja (Abuja Declaration (2001), Mkakati wa huduma ya Afya barani (the Africa Health Strategy 2007-2015, 2016-2030) na mwito wa Addis Ababa wa kuchukua hatua kuhakikisha huduma ya afya kwa wote (Addis Ababa Call to Action on UHC 2019).
Katika Azimio la Abuja kwa mfano, viongozi wa nchi wanachama wa Muungano wa Afrika walipokutana jijjini Abuja, Nigeria, Aprili 2001, walikubaliana kutenga asilimia 15 ya bajeti ya serikali zao kwa afya.
Hii ilikuwa kwa sababu rasilimali zaidi zilihitajika kuangazia changamoto za kiafya wakati huo kama vile virusi vya HIV na Ukimwi, maradhi ya Malaria na Kifua kikuu.
Lakini japo katika kipindi cha hivi majuzi baadhi ya mataifa ya Afrika yameongeza kiwango cha fedha zilizotengewa afya, ni nchi chache ambazo zimetimiza shabaha katika mwaka wowote ule. Kufikia mwaka wa 2018 ni nchi mbili pekee zilizofikia shabaha hiyo.
Kwa sasa mataifa ya Afrika hutumia kati ya $8 na $129 kwa kila mtu kwa afya, ikilinganishwa na mataifa tajiri ambayo hutumia zaidi ya $4,000. Hii ni kwa kutokana na masuala mbali mbali kama vile kiwango cha chini cha jumla ya pato la taifa (GDP) na kiwango cha chini cha ukusanyaji thabiti wa ushuru.
Na japo katika miaka ya hivi majuzi bara la Afrika limeshuhudia ongezeko la kiwango cha ukauaji wa kiuchumi, hii haijamaanisha kwamba fedha zilizotengewa afya ziliongezeka.
Kwa mfano, kati ya mwaka wa 2001 na 2015 fedha zilizotengewa afya katika mataifa 21 barani zilipungua, na wataalamu wanahoji kwamba huenda hali ikazidi kuwa mbaya wakati huu wa mkurupuko wa maradhi ya Covid 19.
Kwa mfano, katika bajeti katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022, Kenya wizara ya fedha ilitenga Sh121.1 bilioni kwa afya katika bajeti iliyofikia Sh3.64 trilioni pekee kwa afya. Kiwango hiki kinawakilisha chini ya asilimia 3.5.
Kuna masuala kadha wa kadha ambayo yamesababisha sekta ya afya kupuuzwa barani inapowadia wakati wa kuitengea fedha. Kulingana na Prof Francis Omaswa, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afya ulimwenguni barani Afrika (ACHEST) na mwenyekiti wa taasisi ya usimamizi wa mifumo ya afya barani (Ashgovnet), Afrika imekumbwa na changamoto ya uongozi mbaya, suala ambalo limetatiza tu sio sekta ya afya, bali maendeleo kwa ujumla.
Aidha, umaskini umekuwa changamoto katika bara hili huku idadi ya watu ikiendelea kuongezeka.
“Pia, mataifa mengi ya Afrika, Kenya ikiwa miongoni mwao, hutegemea ufadhili kutoka nje ili kuendesha asilimia kubwa ya bajeti ya huduma za afya. Hii imesababisha mataifa mengi kushindwa kujitegemea katika sekta hii,” aeleza Prof Omaswa.
Na haya yamekuwa na athari kubwa katika sekta hii hapa barani. Mapema mwaka huu kwenye kongamano la kimataifa la Tume huru kuhusu ajenda ya afya barani Afrika (AHAIC), ripoti kuhusu hali ya huduma nafuu ya afya kwa wote barani iliyotolewa.
Ripoti hiyo kwa jina State of Universal Health Coverage (UHC) in Africa Report iliyokusanywa kati ya Novemba 2020 na Machi 2021, lionyesha kwamba ni asilimia 48 pekee ya idadi ya watu barani wanapokea huduma za afya wanazohitaji. Takwimu hizi ziliashiria kwamba takriban huenda watu milioni 615 barani Afrika wasipokee huduma za afya.
Kwa hivyo swali kuu ni je, matatizo haya yatatatuliwa vipi?
Kulingana na Rais Paul Kagame wa Rwanda, sharti bara hili lijifadhili katika masuala ya afya, na utafiti.
Rais wa Rwanda Paul Kagame. PICHA | MAKTABA
“Viongozi wa Afrika wanapaswa kuwekeza katika mifumo ya afya, uwezo wa kuzalisha bidhaa za kimatibabu, vile vile kuimarisha imani miongoni mwa raia wao,” alisema kwenye kongamano la CPHIA 2021.
Kulingana na Prof Agnes Binagwaho, mwenyekiti msaidizi wa CPHIA, kuna haja ya kuunda vituo vya utafiti barani.
Mwenyekiti msaidizi wa CPHIA, Prof Agnes Binagwaho. PICHA | MAKTABA
“Afrika haipaswi kukaa kitako na kusubiri kushughulikwa na maeneo mengine katika masuala haya.”
“Ikiwa mataifa ya Afrika yananuia kutimizi ndoto ya kuimarisha mfumo thabiti wa afya, basi yanapaswa kuendelea kuwekeza katika watu wake, vituo vya elimu na kuendelea kuhimili wanasayansi na wavumbuzi, miongoni mwa wataalamu wengine wa Kiafya,” alisema Prof Senait Fisseha mwenyekiti msaidizi wa CPHIA na mkurugenzi wa miradi ya kimataifa katika hazina ya The Susan Thompson Buffet Foundation.
Kwa upande mwingine, Prof Omaswa asema Muungano wa AU unapaswa kuchukua hatua dhidi ya viongozi na serikali zisizotekeleza demokrasia.
“Aidha, suluhisho ni kuzungumza na viongozi wa nchi za Afrika na kuwarai kuwekeza zaidi sio tu katika afya, bali pia utafiti. Tatizo ni kwamba viongozi wengi barani huchukulia huduma ya afya kuwa mzigo, ilhali yaweza kuwa uwekezaji mkubwa. Sharti ujumbe huu ufikie viongozi wetu wa kisiasa na hili litafanyika kupitia uhamasishaji.”