Connect with us

General News

Wenye ardhi waitwa serikali ikipanua barabara ya Nyali-Malindi – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wenye ardhi waitwa serikali ikipanua barabara ya Nyali-Malindi – Taifa Leo

Wenye ardhi waitwa serikali ikipanua barabara ya Nyali-Malindi

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI imeanza harakati za kupanua barabara inayoanzia Nyali, Kaunti ya Mombasa hadi Kaunti ya Kilifi kwa lengo la kumaliza msongamano katika barabara kuu ya Mombasa-Malindi.

Kupitia taarifa iliyochapishwa jana katika Gazeti Rasmi la Serikali, mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi Nchini (NLC) Gershon Omanwa, aliwataka wamiliki wa ardhi itakayoathiriwa na upanuzi huo kujitokeza ili walipwe fidia.

Vikao hivyo vitafanyika kati ya Februari 1 na Februari 23 mwaka huu katika afisi za chifu za Takaungu, Mtwapa, Shanzu, Maweni na Kongowea.

Katika Afisi ya Chifu ya Kongowea, Kaunti ya Mombasa, mikutano hiyo itafanyika kati ya Februari 1 na 4.

Katika Afisi ya Chifu ya Maweni, maafisa wa NLC watakutana na wamiliki wa ardhi kati ya Februari 8 na Februari 16.

“Tume ya NLC kwa niaba ya Halmashauri ya Kitaifa ya Barabara nchini (KeNHA) ingependa kutoa ilani ya mazungumzo ya fidia kwa ardhi inayotakikana kwa upanuzi wa barabara ya daraja la Nyali-Mtwapa –Kwa Kadzengo-Kilifi (A107) katika kaunti za Kilifi na Mombasa,” alisema mwenyekiti huyo.

Kwa miaka kadhaa sasa serikali imekuwa ikitumia maelfu ya pesa kuwafurusha zaidi ya wachuuzi 500 waliojenga vibanda nje ya soko la Kongowea ambapo barabara hiyo inatarajiwa kupita wakijitayarisha kwa upanuzi huo.

Hata hivyo, baada ya muda wachuuzi hao wamekuwa wakirudi kujenga vibanda vyao kwenye sehemu hiyo ambapo wizara ya barabara inapania kutumia.

Barabara hiyo kilomita 14 itapanuliwa na kuunganika na ile kuu ya kilomita 460 ya Malindi-Tanga-Bagamoyo ili kuimarisha uchukuzi na biashara hasa kati ya Kenya na Tanzania.

Wiki iliyopita, Waziri wa Uchukuzi James Macharia alizuru Mombasa kudadisi mradi huo.

Benki kuu ya Afrika ilikubali kugharamia ujenzi huo kwa Sh38.4 bilioni wiki chache baada ya Bara la Uropa kutoa Sh3.3 bilioni.