Wimbi la uhalifu Pwani
NA WAANDISHI WETU
ULANGUZI wa mihadarati, magenge ya vijana yanayohangaisha wakazi mitaani, na wahalifu wanaolenga matajiri yamezidi kuibuka Pwani na kutishia utulivu ukanda huo.
Matukio haya yanashuhudiwa katika kipindi cha uchaguzi ambacho hushuhudia visa tele vya uhalifu.
Katika siku chache zilizopita, wapelelezi katika eneo la Pwani wamenasa mihadarati inayokadiriwa kugharimu mamilioni ya pesa.
Mnamo Alhamisi, washukiwa saba wakiwemo wanawake wanne, walifikishwa katika Mahakama ya Shanzu wakidaiwa kupatikana na mihadarati inayokadiriwa kugharimu Sh15 milioni.
Saba hao, walinaswa katika Kaunti ya Kilifi, siku chache baada ya mwanamke kukamatwa mtaa wa Utange, Kaunti jirani ya Mombasa, akidaiwa kuhifadhi heroin zilizokadiriwa kugharimu Sh110 milioni nyumbani kwake.
Polisi walisema kulikuwa pia na raia wa Nigeria ambaye serikali iliagiza afurushwe nchini mara moja.
Wiki iliyopita, Bi Nuru Murshid Mahfudh, alifikishwa mahakamani kwa madai ya kupatikana na heroin katika mtaa wa Utange, Mombasa.
Iliripotiwa kuwa pakiti tisa za mihadarati zilipatikana zimefichwa ndani ya boksi la runinga huku nyingine sita zikiwa ndani ya boksi tofauti. Kulikuwa pia na ratili, paspoti mbili za watu wasiojulikana, na simu mbili ambazo zinachunguzwa kubainisha kama ana washirika.
“Ni muhimu tuzingatie kuwa janga la mihadarati ni sugu Pwani. Kunahitajika uchunguzi wa kina kuhusu suala hili,” kiongozi wa mashtaka, Bw Anthony Musyoka, alisema alipokuwa akiomba agizo la mahakama mshukiwa aendelee kuzuiliwa seli.
Katika Kaunti ya Lamu, polisi Alhamisi walikamata wanaume wawili na wanawake watatu wakisafirisha misokoto 250 ya bangi eneo la Koreni, barabara ya Lamu-Witu-Garsen.
Wiki chache zilizopita, katika kaunti iyo hiyo, polisi walimkamata mshukiwa kwa kusafirisha bangi yenye thamani ya Sh500,000 kwa boti katika Bahari Hindi. Wenzake walitoroka kwa kujirusha baharini na kuogelea.
WIZARA YA USALAMA
Hivi majuzi, serikali ilitaka wananchi wawe macho kuhusu majaribio ya wanasiasa kutumia pesa walizopata kwa njia haramu kufadhili kampeni zao.
Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i, alisema viongozi aina hiyo wakichaguliwa mamlakani, watatatiza juhudi zozote za kuzima uhalifu wao.Ingawa kufikia sasa hapajakuwa na ushahidi wa kuhusisha ulanguzi wa mihadarati Pwani na ufadhili wa siasa za uchaguzi ujao, baadhi ya wakazi hulaumu dawa za kulevya kwa madhila mengine yanayokumba eneo hilo.
Msemaji wa vijana waliojinasua kutoka kwa uraibu wa mihadarati Lamu, Bw Salim Athman, alisema baadhi ya wanasiasa huwatumia waraibu wa dawa za kulevya kuzua fujo katika mikutano ya hadhara.
WARAIBU WA MIHADARATI
Watumizi wengi wa mihadarati mitaani wanaofahamika kama mateja, huwa hawana namna ya kupata fedha.
“Tumeamua tusaidie wenzetu kwa njia moja au nyingine, ikiwemo kuhakikisha hawatumiwi vibaya na wanasiasa,” akasema.
Hatari zaidi hutokea kuwa, vijana hao hutembea na silaha na kuvamia wapitanjia wanapotoka katika mikutano ya kisiasa.Haya huzidisha utovu wa usalama unaosabishwa na magenge mengine ya vijana mitaani. Mwezi Aprili, kikosi kipya cha polisi kiliundwa kukabiliana na magenge hayo.
Mbali na haya, kumeibuka pia wahalifu wanaoonekana kulenga mabwanyenye.
Mnamo Aprili, mwanasiasa aliyepanga kuwania kiti cha ubunge Mvita kupitia kwa UDA, Bw Ali Mwatsahu, aliponea chupuchupu alipomiminiwa risasi 22 usiku alipokuwa ndani ya gari lake barabarani.
Jumapili usiku, mwili wa mfanyabiashara Giddy Mukugi ulipatikana kando ya barabara takriban kilomita tatu kutoka Kituo cha Polisi cha Nyali.
Polisi walisema kuwa, mashahidi waliwaarifu kwamba mfanyabiashara huyo alikuwa kwenye gari lake huku lingine likimfuata nyuma kwa kasi mwendo wa saa tano asubuhi Jumapili.
“Gari hilo lilimpita na kumfungia njia. Watu waliokuwa kwenye gari la pili walimtoa nje marehemu na kuanza kumpiga kwa jiwe kichwani. Dereva wake alitoroka walipovamiwa,” ripoti ya polisi ikaeleza.
Mwanamume huyo alikuwa na bunduki aliyofyatua mara kadha lakini haikuwapata washambuliaji wake. Bunduki yake, kitambulisho na leseni ya kuendesha gari zilipatikana katika eneo la tukio.