Wito vijana wa Kiislamu wapewe vitambulisho bila ubaguzi Kiambu
Na LAWRENCE ONGARO
WAISLAMU zaidi ya 1,000 kutoka kaunti ya Kiambu, walikongamana kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya, Landless, mjini Thika, huku wakidai kuwa wametengwa na serikali kuu.
Waislamu hao walikongamana pamoja kwa lengo la kuungana ili kuongea katika ukumbi huo kuhusu maslahi yao kama Waislamu.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na mbunge wa Thika Patrick ‘Jungle’ Wainaina.
Waislamu hao walilalamika kuwa wengi wao ambao wanaishi Thika na Kiambu, hawapati huduma sawa kama jamii nyingine.
Walisema hata ingawa wenzao Waislamu kutoka maeneo ya Kaskazini Mashariki hupata nanasi ya kujitetea kuhusu shida zao, lakini wale Waislamu walio maeneo mengine mashinani wanatelekezwa hasa wakati wa kutoa vitambulisho.
Wanadai kuwa wao hupitia vikwazo vingi kwa kuagizwa kufika na msimamizi wa kutambua uhalisia wao kama ni raia wa Kenya.
Waislamu hao walipitisha ‘Azimio’ lao kuwa watamchagua Bw Wainaina ambaye ni mbunge wa Thika, awe kama gavana wa kaunti ya Kiambu.
Walisema huyo ndiye wamewekea matumaini kwake kama mgombeaji halisi wa kiti hicho cha ugavana.
Bw Wainaina kwa upande wake aliitetea serikali akisema tayari imetoa nafasi kadha za ajira kwa Waislamu, lakini aliwahakikishia atatetea matakwa yao mashinani.
“Iwapo nitapata nafasi kama gavana wa Kiambu, nitafanya juhudi kuona ya kwamba Waislamu wanapokea fedha za maendeleo NG-CDF bila ubaguzi pamoja na vitambulisho vya kitaifa,” alifafanua mbunge huyo.
Alisema akiwa kinara wa kaunti ya Kiambu atahakikisha kuna usawa kwa kila mkazi wa Kiambu.
Mwenyekiti wa Waislamu aliyeongoza ujumbe huo Bw Hassan Kinyua alipendekeza serikali ifanye hima ili vijana Waislamu wapate vitambulisho ili waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.
Mwaniaji wa kiti cha ubunge Thika Bw Juma Hamedi, alidai kuwa vijana wengi Waislamu wana hamu kubwa ya kupiga kura ili kutekeleza haki yao ya kupiga kura na kwa hivyo wanastahili kupokea vitambulisho hivyo haraka iwezekanavyo.
Alieleza kuna vijana wengi Waislamu wasio na vitambulisho na kwa hivyo ni vyema kupewa nafasi ya kupata haki hiyo.
“Nimezunguka katika mji wa Thika na vitongoji vyake na nimepata ya kwamba vijana wengi hasa Waislamu wanahitaji vitambulisho haraka iwezekanavyo,” alifafanua Bw Hamedi.