Connect with us

General News

Chama cha PAA chataka wazee wateue wagombeaji – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Chama cha PAA chataka wazee wateue wagombeaji – Taifa Leo

Chama cha PAA chataka wazee wateue wagombeaji

NA MAUREEN ONGALA

CHAMA cha Pamoja African Alliance (PAA), kinazingatia kutumia mbinu ya mashauriano baina ya wanasiasa ili kuamua watakaopewa tikiti ya chama hicho kuwania viti mbalimbali katika uchaguzi ujao.

Gavana wa Kilifi, Bw Amson Kingi anayeongoza chama hicho, amewatwika jukumu wazee katika jamii tofauti kuendeleza mazungumzo kati ya wanasiasa wanaopigania kiti kimoja ili kuwe na maelewano.

Bw Kingi alisema kuwa hali hii itarahisisha maamuzi na kuhakikisha kuna haki na usawa.

Akizungumza katika wadi ya Kambe Ribe wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika eneo bunge la Rabai, Bw Kingi aliwaahidi wanachama wa PAA kuwa endapo watalazimika kufanya kura za mchujo, itakuwa kwa njia ya haki.

“Kuna wagombea viti wengi wa viti mbalimbali na hawa wote ni familia ya PAA. Ningekuwa na uwezo ningewapa vyeti hao wote lakini sina uwezo huo. Ninataka wazee wanisaidie kwa sababu penye wazee hapaharibiki kitu. Mjipange na muwe na vikao na wagombea viti hao na kushauriana nao ili wakubaliane kwa hiari yao,” akasema.

Hata hivyo, Bw Kingi aliwaonya wazee hao dhidi ya kuwashurutisha baadhi ya wagombea viti hao kutupilia mbali azma yao ya kuwania viti vya kisiasa ili kuwapisha wapinzani wao.

Alisema kuwa atakubaliana na uamuzi wa wazee hao iwapo tu utakuwa wa haki.

“Nitasalimu amri ya wazee na nitampa atakayechaguliwa cheti cha kupeperusha bendera ya chama cha PAA katika uchaguzi mkuu,” akasema.

Wakati uo huo, aliwaonya wananasiasa wanaojigamba kuwa tayari wamechaguliwa kupeperusha bendera ya PAA kwa sababu wako karibu naye kuwa wana kibarua kigumu cha kutafuta kuungwa mkono kutoka kwa wananchi ili kuungwa mkono na chama.

Alizidi kusema kuwa, wanasiasa wajiepushe na vurugu kwani wananchi wanahitaji viongozi wenye hekima na maarifa ya kuwatatulia changamoto zinazowakumba.

Kauli hii ya gavana inajiri baada ya makundi ya vijana waliokuwa wakishabikia wanasiasa mbalimbali katika eneo bunge la Rabai kuleta fujo.