Daktari asema hakupata sumu katika mwili wa Tecra
Na RICHARD MUNGUTI
MTALAAMU KATIKA maabara ya serikali aliambia mahakama kuwa hakupata sumu wala pombe mwilini mwa Tecra Patricia Muigai, katika kesi inayochunguza kilichosababisha kifo cha mwanadada huyo mrithi wa kampuni ya kutengeneza pombe ya Keroche Industries.
Bw James Matinde ambaye alipima sampuli sita kutoka kwa mwili wa Tecra, alisema hakupata sumu yoyote ambayo ingechangia katika kifo chake.Vilevile, mtaalamu huyo alisema hakupata kileo chochote katika sampuli iliyotolewa kwenye jicho la Tecra.
Usiku ambao Tecra alianguka, mpenziwe Omar Lali aliambia polisi kwamba, walikuwa wametafuna miraa na kubugia pombe aina ya Smirnoff.Chupa mbili kubwa za pombe na ya Soda ya Fanta ziliwasilishwa kortini kama ushahidi.
Mahakama pia ilielezwa kuwa polisi hawakupewa mabaki ya miraa ambayo Lali alikuwa akichana wakiwa na Tecra.“Sikupata hata chembe za pombe katika Vitreous Humor (sampuli kutoka kwa jicho la Tecra),” Bw Matinde alisema alipohojiwa na wakili maarufu wa Mombasa, Bw Yusuf Abubakar.
“Je katika sampuli zote sita ulizopokezwa na afisa wa polisi Bw Isaack Thiaka, ulipata sumu yoyote ambayo ingechangia kifo cha Tecra?” wakili Abubakar alimuuliza Bw Matinde.Akajibu mtaalamu: “Sikupata sumu yoyote katika sampuli nilizoletewa na Bw Thiaka.
Wala sikupata chembe za kileo katika sampuli ya jicho la Tecra. Jicho huhifadhi maji kwa muda mrefu na kungelikuwa na kileo ningetambua.”Shahidi huyo aliongeza kuwa pombe inaweza kupatikana katika chembechembe za mwili saa nane tu baada ya mtu kuaga dunia.
Bw Matinde alisema jinsi mwili unavyozidi kukaa ndivyo pombe inazidi kuyeyuka kwenye damu na sehemu zingine mwilini.Mtaalamu mwingine Henry Kiptoo Sang, aliyefanya ukaguzi wa kisayansi wa DNA, alithibitisha sampuli alizopokea zilikuwa za Tecra Muigai aliyeaga mnamo Mei 2, 2020.
Afisa wa polisi anayechunguza kifo hicho Inspekta Mkuu Evans Chea, alieleza korti kwamba meneja wa hoteli ya Jaha Guest House iliyoko eneo la Shela ambapo Tecra alianguka Aprili 24, 2020, hakuwafahamisha polisi kuhusu tukio hilo.Aidha, Inspekta Chea alisema meneja huyo aliamuru damu iliyokuwa mahali ambapo Tecra alianguka, isafishwe kabla ya polisi kuwasili.
“Meneja wa hoteli ya Jaha Guest House hakupiga ripoti kwa polisi,” afisa huyo wa polisi alieleza.kuhusu kuanguka na kuumia kwa Tecra,” afisa huyo wa polisi alieleza.Insp Chea alisimulia hayo katika uchunguzi wa kifo cha Tecra, aliyekuwa mpenziwe Omar Lali, anayefanya kazi ya utalii kaunti ya Kilifi.
Afisa huyo alisema yeye na Lali ni marafiki na hata wao hunywa chai naye.Alisema Lali alimweleza kwamba Tecra alianguka na kuumia.Lali aliwaita nduguzake na kumpeleka hospitali ya King Fahad na hatimaye akasafirishwa kwa ndege hadi Nairobi Hospital alipofia.
Next article
PETER NGARE: Wakenya waache kasumba ya ‘Mtu…