BAHARI YA MAPENZI: Huwezi kuepuka, pesa ni muhimu katika penzi
SIZARINA HAMISI na BENSON MATHEKA
TUMESIKIA wakisema, pesa sabuni ya roho.
Pesa ni kichocheo cha furaha. Ukiwa na pesa unajiamimi. Unaweza kufanya unalotaka wakati wowote. Ndiyo maana wengi wanadiriki kusema tafuta pesa ili uwe kama mfalme.
Wanaosema pesa ndiyo kila kitu wana hoja. Pesa inaweza kukufanya umfurahishe mpenzi wako kwa kumnunulia zawadi. Kumnunulia mapambo ambayo yatamfanya awe na amani kwa wakati husika.
Kuna dada mmoja hapo awali aliwahi kutaka nimshauri afanyeje, kwani ameingia kwenye uhusiano na mwanaume ambaye hana hisia naye, hampendi, isipokuwa anampatia pesa nyingi na kila anachotaka.
Akaniambia hata anapokuwa faragha, anashindwa kumuangalia usoni inabidi ajifunike blanketi ili asione sura yake.
Wapo wanaodai kwamba katika mapenzi, pesa ni muhimu kuambatanisha, lakini pia wapo wanaosema kwamba anayetanguliza pesa katika mapenzi hana upendo wa kweli.
Nao wengine wanasema bila pesa mapenzi hayaendi kwani wanawake wana mahitaji ambayo hutegemea kutimiziwa na wenzao kutokana na utamaduni uliozoeleka wa mwanaume kuwa ndiyo muhudumiaji wa familia.
Ndiposa swali kubwa ni kwamba ni maumivu au raha gani unapata kuishi na mtu mwenye pesa nyingi, tajiri anayekupa kila unachohitaji lakini huna hisia nae au hana hisia na wewe.
Pesa ni sehemu ya mahusiano tena huja bila hata hoja, isipokuwa mapenzi ni hisia. Mapenzi na pesa vinahusiana na vinaingiliana, lakini kukiwa na msingi wa mapenzi na halafu hiyo pesa ifuatie kwa juu.
Unaweza kuwa na mtu mwenye pesa nyingi lakini mahusiano yakawa yanakutoa machozi kila siku. Unaweza kuwa na mapenzi kupita kiasi kwa mwenzako, lakini pia pesa ikawa ni kikwazo cha kuweza kuwaletea uhusiano wenye amani na furaha.
Kwa maana hata kama pesa itakosekana kwenye uhusiano na mapenzi yawepo, uhusiano unaweza kuendelea kulingana na mtizamo wa wahusika.
Lakini msingi wa uhusiano ukiwa ni pesa, pale inapokosekana tu kuna uhakika mkubwa wa kuvunjika kwa uhusiano uliopo.
Mapenzi pia ni hisia. Kwani unaweza kuishi na mtu ambaye hana chochote ila ana mapenzi yote kwako, mapenzi yanayoshibisha moyo wako. Pale mwenzako anapokuonyesha mapenzi ya dhati, anakuwa tayari kukutendea lolote sababu anakupenda na mnapendana. Hili linapokuwepo, nafasi ya pesa huchukua sehemu ndogo na haiwezi kuwa chanzo cha mvurugano baina yenu.
Hata hivyo, hali halisi ya hivi sasa ni kwamba pesa imekuwa kipaumbele kwenye mahusiano, na ndio maana vijana wengi wanatendwa. Hapa ndipo unakuta mtu anakwambia naishi na fulani kwakua ana pesa tu nimchune lakini sina hisia naye.
Siku zote kwenye upendo, maeleweno na mapenzi ya dhati, kunakuwa na mazingira na nafasi ya kutafuta pesa ama kujenga maisha mazuri kwa pamoja.
Na mara nyingi wale wenye pesa, huwatumia vibaya wale wanaowataka kimapenzi. Kwani katika mtizamo wao hiyo ni biashara ya nipe nikupe.
Unaweza kupata msichana anadhalilishwa na mwanaume sababu ya pesa alizotafuna na sababu huyo mwanaume hana mapenzi ya dhati, sio taabu kwake kukejeli, kudharau na hata kudhalilisha bila kujali hisia za mhusika.
Unavyoona, bora penzi ama hiyo pesa?
HAKUNA asiyetaka kuwa na mpenzi mkwasi wa pesa. Hii ni kwa wanawake na wanaume. Na sio siri kwamba watu walio na pesa nyingi au wanaojua kutumia pesa, huwa wanajishindia wapenzi, tena warembo wa kufanya watu kuvunjika shingo wakiwatazama.
Kauli mbiu ya wengi siku hizi ni kuwa, penzi halitafunwi likajaza tumbo. Asiye na pesa au asiyejua kutafuta pesa na kuzitumia kwa watu wa jinsia tofauti, hawezi kupata mpenzi.
Ndio maana watu wamekuwa wakiachwa na wapenzi wanaowaendea wanaowapa pesa. Kadiri vizazi vipya vinavyojiri, ndivyo pesa zinavyobadilika kuwa kigezo muhimu kwa mtu kujishindia mpenzi. Mwanamume aliye na pesa hupiganiwa na wanawake kadhaa, kila mmoja akitaka kutambuliwa kama mtu wake halali. Mwanamume anaweza kuwa na sura mbaya, lakini akiwa na pesa, wanawake watampigania.
Visa kama hivi vimekuwa vikiripotiwa kila wakati, kila mahali na vinaendelea kuongezeka. Hakuna mwanamke anayeweza kukwamilia kwa mwanamume mkono gamu, sahau!
Ukweli utabaki kuwa, utamu wa mapenzi, ni pesa na jinsi ya kuzitumia. Vile vile, enzi za wanaume kuwafuata wanawake wasio na pesa zinaendelea kupita kwa kasi.
Vijana barobaro, wamekuwa wakiwamezea mate wanawake waliofanikiwa wawe wapenzi wao kiasi cha kutekwa na mama sukari.
Lakini yote tisa, kumi ni kuwa linalopuuzwa na wengi ni kuwa penzi lililojengwa kwa pesa, huwa limefunika dhiki. Kuna watu wanaovumilia wapenzi katili kwa kuwa wanawapa pesa na hawakosi chochote.
Kwa kuwa mahusiano ya mapenzi siku hizi yanajengwa kwa pesa, hayadumu. Ni wengi ambao wamezuru ulimwengu, wakajenga maghorofa na kuishi kama wafalme kwa sababu ya pesa lakini moyoni wanakosa furaha na amani.
Mapenzi ya pesa hukatika na kunyauka wakati wowote na kuacha mtu akisononeka. Kama pesa zingetumiwa kama nguzo ya mapenzi ya kudumu hadi kifo kitenganishe wanandoa, basi mabwanyenye kama vile Bill Gates na Melinda Gates, ambao utajiri wao sio wa kubahatisha, ukiwa umetokana na elimu na bidii ya miaka mingi, hawangetalikiana.
Ni rahisi pia kwa mwanamume mwenye pesa kuchepuka kuliko asiye na pesa na hii sio siri pia. Siri ambayo pengine baadhi ya wanawake hawafahamu ni kuwa wanaume wanachukia warembo wanaobana pesa zao. Naam, mwanamke asiyeweza kutumia pesa kuchangia katika masuala ya mahusiano, hasa katika ndoa, ni rahisi kukosa mume. Kigezo kikuu ambacho mwanamume wa kisasa anazingatia kutafuta mke, ni ikiwa demu anaweza kutoa pesa zake kusaidia majukumu ya kifamilia au atamwachia kila kitu wakioana.
Thamani ya mapenzi ni zaidi ya pesa anazomiliki mtu, lakini sivyo ilivyo kwa wengi, wanaotaka fasheni, marashi, magari, vipondozi na kutalii ulimwengu. Hakuna asiyetaka kuonekana nadhifu na mrembo na haya ni mambo yasiyowezekana bila pesa. Kama pesa hazingekuwa muhimu kwa kupata mpenzi, hali ingekuwa tofauti kwa watu wangwana wasio na viosha roho kwa kukosa ngweje. Ukweli ndio huu, pesa ni sabuni ya roho lakini hazioshi roho.
[email protected]
[email protected]