ZARAA: Kilimo cha matunda kinahitaji maji ya kutosha
Na SAMMY WAWERU
JOSPHAT Kiarie amekuwa katika kilimo cha matundadamu kipindi cha muda wa miaka mitatu sasa.
Aliingilia shughuli hiyo mapema 2020 baada ya kufanya vibarua vya hapa na pale.
Mwanzo, alichapa gange jijini baada ya kuhitimu kwa Stashada ya Uhandisi katika Masuala ya Maji 2017.
Baadaye, Kiarie alihamia Murang’a anakotoka akafanya kibarua cha uuzaji wa kuni kwa taasisi mbalimbali.
“Ni kupitia uuzaji wa kuni nilikutana na mfanyabiashara wa miche aliyekuwa anaikuzia Nairobi nilishawishika kuingilia kilimo,” asema.
Kando na kustawisha matundadamu, maarufu kama tree tomato, Kiarie pia amepanda miembe, miparachichi, migomba ya ndizi, michungwa, midimu, mikarakara kati ya mitunda mingineyo.
Kulingana na mkulima huyu, hatua ya kwanza kufanikisha jitihada zake ilikuwa kuhakikisha ana chanzo cha maji ya kutosha.
Josphat Kiarie, mkulima wa matunda Kaunti ya Murang’a. PICHA | SAMMY WAWERU
Aidha, ana bwawa linalositiri zaidi ya lita 50,000.
Anasema iwe msimu wa kiangazi au ukame halikauki. Maji yake, hutoka ardhini.
“Kwa siku, hutumia karibu lita 2,000 kunyunyizia mimea,” adokeza.
Kwa ushirikiano na baba na ndugu zake wote wakiwa wakulima, wamewekeza katika mfumo wa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa mifereji.
Aidha, wana tangi la kuyahifadhi. Isitoshe, wana jenerta kuyapampu.
Wakati wa mahojiano na Kiarie, 28 shambani mwake eneo la Gacharage, Murang’a alisema mradi wa maji umewagharimu zaidi ya Sh400,000.
Daniel Mwenda, mtaalamu wa masuala kilimo hasa upanzi wa matunda na miti, anasema ukuzaji wa matunda unafanikishwa na kuwepo kwa maji ya kutosha.
“Nchi kama Israili na Misri ambazo ni jangwa, zinazalisha matunda kwa wingi kwa sababu ya kukumbatia mifumo ya uvunaji maji,” Mwenda aelezea.
Mataifa hayo ni tajika katika ukuzaji wa zabibu, matufaha na machungwa.
Kenya ni miongoni mwa nchi zinazotegemea Israili na Misri katika matunda hayo ambayo ni adimu.
“Siri kufanikisha kilimo cha matunda ni kuwepo na maji ya kutosha,” Mwenda asisitiza, akihimiza wakulima kukumbatia mifumo ya mifereji kunyunyizia mimea na mashamba maji.
Huku matunda yakiwa miongoni mwa kiungo muhimu mwilini, serikali inahimizwa kuwekeza pakubwa katika uvunaji maji.
Wanazaraa wengi Kenya wana ari kuzalisha matunda, ila upungufu na ukosefu wa maji unakwamisha jitihada zao.
Inaposoma makadirio yake ya bajeti kila mwaka, serikali inapaswa kuipa kipau mbele miradi ya maji hasa uvunaji.
Si lazima ichimbe mabwawa yanayogharimu mabilioni ya pesa. Mkulima Kiarie anaithibitishia kima cha Sh500,000 ni tosha kuhami wakulima kadhaa. Kiwango hicho cha fedha ni mithili ya tone baharini kwa serikali.
Ni muhimu ifahamu, wakulima wanapopata maji ya kutosha kuendeleza zaraa ndivyo kapu lake la ushuru linaongezeka.
Hii ina maana kuwa idadi ya wakulima hususan wa matunda itaongezeka.
Matunda ni kati ya mazao yenye soko lenye ushindani mkuu nchi za nje.