KUMBUKUMBU ZA SPOTI: Kiungo mahiri Kadir aliyewika Afrika Mashariki
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
JINA la Kadir Farah liliwika miaka ya 1960 na 1970 kwani alikuwa kiungo bora sio nchini Kenya pekee bali kote Afrika Mashariki.
Mwanasoka huyo ambaye aliaga dunia miaka ya 1990 alifanikiwa kuwa mwanasoka wa kutambulikana 1970 alipochezea klabu ya Feisal FC, ambako aliitwa kwa timu ya taifa Harambee Stars na aliyekuwa kocha Mjerumani Ekhardt Krautzun.
Mwaka 1971, Farah alikuwa mmoja wa wachezaji waliotambulika zaidi Stars iliposhinda kwa mara ya tano kombe la East African Challenge Cup jijini Nairobi.
Alifunga bao lililowezesha Kenya kufuzu kwa mara ya kwanza dimba la Mataifa Bingwa Afrika (AFCON) zilizofanyika 1972 nchini Cameroon.
Mbali na kuwa katika timu ya taifa, Farah alikuwa kiungo muhimu katika timu ya Mombasa Combined akiisaidia kubeba mataji kadhaa ya Remington Cup, ambalo lilikuwa likipiganiwa na timu za mikoa nchini.
Wakati mmoja Farah alipotaka kugombania kiti cha udiwani wadi ya Bondeni, alilazimika kuwachezea mahasimu wao wakubwa, Liverpool (waliobadilisha jina baadaye kuwa Mwenge) ili apate kura za mashabiki wa timu hiyo.
Aliyekuwa meneja wa Feisal FC, Abdillahi Bashasha, asema hakujatokea kiungo aliye mzuri zaidi ya Farah.
“Kadir Farah alikuwa shupavu katika safu hiyo, na tangu miaka hiyo sijaona mfano wake,” asisitiza Bashasha.
Mwanasoka huyo aliyeanza kuonyesha kipaji chake tangu alipokuwa katika klabu ya Wananyuki FC ni mmoja ambaye hategemei kusahaulika kwani aliacha historia ya kuwa kiungo bora zaidi Afrika Mashariki.
Akiichezea timu ya Mombasa Combined, Farah alikuwa akishirikiana vyema na wanasoka wa klabu pinzani ya Mwenge kina Nassir Omar, Jabir Riziki, Ahmed Breik, Ali Kombo, Badi Ali na wengineo ambao waliing’arisha timu hiyo ya Mombasa kuchukua ubingwa wa mkoa wa Pwani miaka kadhaa.
Aliyekuwa meneja wa Feisal FC, Abdillahi Bashasha alisema kuwa hadhani kama kutawahi kutokea mchezaji wa safu ya kiungo aliye mzuri zaidi ya Farah.
“Ni Kadir Farah ndiye aliyekuwa nyota na tangu miaka hiyo, sijaona mfano wake,” akasema Bashasha.