Kocha Klopp kukosa gozi la EPL kati ya Liverpool na Chelsea baada ya kuugua Covid-19
Na MASHIRIKA
KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool atakosa gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) litakalowakutanisha na Chelsea uwanjani Stamford Bridge mnamo Januari 2, 2021.
Hii ni baada ya mkufunzi huyo raia wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 54 kuonyesha dalili za corona na kulazimika kujitenga.
Kutokuwepo kwake kutampa msaidizi wake Pep Lijnders fursa ya kuongoza Liverpool dhidi ya Chelsea katika mchuano unaotarajiwa kutawaliwa na hisia kali.
Mnamo Disemba 31, 2021, Klopp alisema kwamba wanasoka watatu wa Liverpool walikuwa wamepatikana na virusi vya corona.
Mabingwa hao mara 19 wa EPL baadaye walitoa taarifa kulikuwa na visa zaidi vya maambukizi ya corona kambini mwao huku maafisa watatu wa benchi ya kiufundi wakiugua Covid-19.
Sawa na Liverpool waliopokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Leicester katika mchuano uliopita ligini, Chelsea nao watakuwa na kiu ya kujinyanyua baada ya Brighton kuwalazimishia sare ya 1-1 katika mechi ya awali.
Kujikwaa zaidi kwa Chelsea au Liverpool kutadidimiza matumaini yao ya kufukuzana na viongozi Manchester City wanaopigiwa upatu wa kuhifadhi ufalme wa EPL muhula huu chini ya mkufunzi Pep Guardiola baada ya kutandika Arsenal 2-0 mnamo Januari 1, 2022.
Mechi nne kati ya tano zilizopita ambazo Chelsea wametandaza katika EPL ugani Stamford Bridge zimekamilika kwa sare za 1-1 huku The Blues wakikosa kukamilisha mchuano wowote bila ya kufungwa.
Japo kocha Thomas Tuchel amepuuza uwezekano wa Chelsea kutawazwa wafalme wa EPL msimu huu baada ya uthabiti wa kikosi chake kulemazwa na majeraha na virusi vya corona, mkufunzi Jurgen Klopp amewataka masogora wake wa Liverpool kujituma maradufu.
“Kampeni za EPL zimefikia katikati na chochote kinaweza kutokea katika mchezo wa soka. Kabla ya kukutana na Leicester katika gozi lililopita ligini, mashabiki walipigia Liverpool upatu wa kushinda. Tulikuwa tumewadengua kwenye Carabao Cup na walikuwa na maruerue ya kichapo kinono cha 6-3 kutoka kwa Man-City,” akasema Klopp.
Kichapo ugani King Power kilikuwa cha pili kwa Liverpool kupokea katika mashindano yote ya msimu huu wa 2021-22. Mabingwa hao wa 2019-20 sasa wanakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 41, moja pekee nyuma ya Chelsea walioshinda EPL mara ya mwisho mnamo 2016-17 chini ya kocha Antonio Conte wa Tottenham Hotspur. Man-City wanaselelea kileleni kwa alama 53 baada ya mechi 21.
Kinachotarajiwa kuwapa Chelsea motisha zaidi ni rekodi duni ya Liverpool jijini London. Kufikia sasa, mabingwa hao mara 19 wa EPL wameshindwa kuangusha Brentford, West Ham United na Tottenham Hotspur wanaotokea London katika mechi za ugenini muhula huu. Hata hivyo, Liverpool wamepoteza mechi mbili pekee kati ya 11 zilizopita dhidi ya Chelsea ugani Stamford Bridge.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO