Connect with us

General News

Kongamano kuuamsha mji kibiashara – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kongamano kuuamsha mji kibiashara – Taifa Leo

Kongamano kuuamsha mji kibiashara

PIUS MAUNDU na WANDERI KAMAU

KONGAMANO la Ugatuzi ambalo linatarajiwa kuanza leo Kaunti ya Makueni, limeuamsha kibiashara mji mdogo wa Wote, ambao kwa kawaida huwa hauna shughuli nyingi.

Uchunguzi wa ‘Taifa Leo’ jana, ulibaini kwamba karibu majumba yote ya malazi yamejaa katika mji huo na viungani mwake, hali waliyotaja kuwa dalili ya kuimarika kwa mapato. Vyumba vingi vya malazi pia vimeongeza ada zake maradufu.

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kufungua rasmi kongamano hilo, ambalo litadumu kwa siku nne. “Vyumba vyetu vyote 25 vimejaa. Vyumba ambavyo tulikuwa tukikodisha kwa Sh5,000 sasa vimefikia Sh10,000. Tumewaajiri wafanyakazi zaidi kukidhi ongezeko la shughuli za kibiashara,” akasema Bw Alex Ndetei, ambaye ndiye meneja wa Fort Hotel.

Wafanyabiashara wameeleza kufurahishwa na hatua ya kamishna wa kaunti hiyo, Mohammed Maalim, kuondoa baadhi ya masharti yaliyokuwa yamewekwa kukabili maambukizi wa corona kwa wakati ambapo kongamano hilo litakuwa likiendelea.

Hata hivyo, idara za usalama zimewarai wenyeji kuchukua tahadhari, hasa wakati huu nchi inapokabiliwa na tishio za janga la corona na ugaidi. Waandalizi wa kongamano wanasema wanachukua kila tahadhari kuhakikisha washiriki wamezingatia masharti yaliyowekwa na serikali kuzuia maambukizi ya virusi hivyo.

“Kila mtu atakayehudhuria kongamano hili ni lazima awe amepokea chanjo dhidi ya virusi hivyo. Huwezi kujua wakati wimbi jingine la maambukizi litakapotokea,” akasema Gavana James Ongwae (Kisii), ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati kuu andalizi ya konganano hilo.

Wiki iliyopita, Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, alitangaza hali ya tahadhari nchini kuhusiana na tishio la mashambulio ya kigaidi. Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Makueni, Bw Joseph Ole Napeiyan, amewahakikishia washiriki wote usalama wa kutosha.

Aliwaomba kuripoti kisa chochote cha mtu wanayemshuku kwa polisi. Kongamano hilo lilipangiwa kufanyika mwaka uliopita lakini likaahirishwa kutokana na tishio la corona. Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, anatarajiwa kuhutubu Alhamisi huku Naibu Rais William Ruto akilifunga rasmi mnamo Ijumaa.

Wakati huo huo, Bw Odinga jana alisisitiza kuhusu haja ya nchi wanachama wa Muungano wa Kikanda wa Maendeleo (IGAD) kuharakisha utekelezaji wa miundomsingi yake ili kuimarisha ushindani wa kibiashara na maeneo mengine duniani.

Alisema hayo kwenye kikao kuhusu ustawishaji wa miundomsingi katika mataifa hayo kilichofanyika jana jijini Nairobi.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending