Connect with us

General News

Kutumia utafiti kutoa tiketi kwaibua migawanyiko UDA – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kutumia utafiti kutoa tiketi kwaibua migawanyiko UDA – Taifa Leo

Kutumia utafiti kutoa tiketi kwaibua migawanyiko UDA

NA ONYANGO K’ONYANGO

MVUTANO umeibuka ndani ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu wa Rais William Ruto, kuhusu pendekezo la kutaka kutumia utafiti wa kura za maoni kutoa tiketi kwa wanasiasa watakaoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Chama cha UDA kinalenga kuendesha kura ya mchujo kati ya Aprili 9 na 16, mwaka huu.

“Kura za mchujo zitafanyika katika kaunti zote nchini kati ya Aprili 9 na 16,” ikasema taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi ya UDA, Anthony Mwaura.

Huku tarehe hiyo ikikaribia, Taifa Leo imebaini kuwa viongozi wa UDA wamegawanyika ikiwa chama hicho kitatumia utafiti wa kura ya maoni kubaini wawaniaji walio na ushawishi wa kisiasa na kuwapa tiketi.

Mbunge wa zamani wa Mugirango Kusini Omingo Magara alipojiuzulu wadhifa wa mwekahazina wa UDA, mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alidai kuwa aliogopa kushiriki kura za mchujo.

Bw Magara hakutaka kushindana na mbunge wa Nyaribari Masaba Ezekiel Machogu ambaye anataka kutumia tiketi ya UDA kuwania ugavana wa Kisii.

Bw Machogu aligura muungano wa Azimio la Umoja na viongozi wa UDA walihisi kuwa ni maarufu kuliko Bw Magara.

“Ulihama UDA ukidai kuwa hakuna demokrasia. Lakini ukweli ni kwamba ulitaka kupewa tiketi ya moja kwa moja ya UDA na haukutaka kushiriki mchujo,” akasema Bw Sudi.

Mwenyekiti wa UDA Johnstone Muthama alisema kuwa chama hicho kitatumia utafi – ti wa kura ya maoni kuwapa tiketi wawaniaji katika baadhi ya maeneo.

Kulingana na Bw Muthama, shughuli ya kutoa tiketi za UDA kwa kuzingatia utafiti wa wataalamu haijaanza na inatarajiwa kutumiwa katika maeneo ambapo wawaniaji wanakosa kuelewana.

“Tutatumia njia tatu kupata wawaniaji wa UDA. Njia ya kwanza, wafuasi wa UDA watapewa fursa ya kuteua wawaniaji kwa njia ya kura za siri. Njia ya pili, tutatumia utafiti wa wataalamu kutambua mwaniaji aliye na uungwaji mkono mkubwa. Njia ya tatu, tutawapa fursa wawaniaji wanaoshindana kuelewana,” akaelezea Bw Muthama.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa anasema kuwa chama cha UDA kimekuwa kikifanya utafiti wa kura za maoni kisiri kutafuta wawaniaji maarufu kila baada ya wiki mbili.

“Katika baadhi ya maeneo tutatumia ripoti ya utafiti wa siri kutoa tiketi kwa mwaniaji maarufu. Tumekuwa tukifanya utafiti kisiri kila baada ya wiki mbili kwa sababu huwezi kufanya mara moja na kutumia matokeo yake,” akasema Bw Barasa.

Lakini Katibu Mkuu wa UDA Veronica Maina jana aliambia Taifa Leo kuwa ripoti za utafiti wa wataalamu hazitatuiwa kutoa tiketi kwa wawaniaji.

“Hatuwezi kutumia ripoti ya utafiti kutathmini umaarufu wa wawaniaji wetu.

Itakuwa vigumu kwa wawaniaji kuthibitisha kuwa utafiti huo umefanywa kwa njia huru na haki,” akasema Bi Maina.