Chekecha unga kwa kutumia chungio kwenye chombo utakachotumia wakati utakanda unga wako na punguza nusu kikombe cha unga uweke pembeni.
Chukua kikombe weka hamira, sukari vijiko viwili, unga vijiko viwili na tui vijiko vinne na uache kwa dakika tano mpaka mchanganyiko ufure.
Chukua unga ulioweka kwenye chombo chako, weka baking powder na chumvi.
Twanga hiliki baada ya kuzimenya kisha weka kwenye unga unaotaka kuukanda.
Chukua hamira iliyoumuka, changanya na unga wako kwa mkono vizuri.
Malizia kwa kumimina tui lako kidogokidogo na uanze kuukanda utakapokuwa donge moja.
Weka samli kwa unga wako na uendelee kuukanda.
Kanda unga kwa dakika 10 mpaka ulainike kisha ufunike vizuri au uweke kwenye chombo na uufunike ili usipitishe hewa. Uache kwa dakika 15 kwenye sehemu ya joto. Ukishaumuka, kata madonge na uyasukume kwa kutumia unga mkavu upate duara ila lisiwe nene sana wala jembamba sana. Ukishafanya hivyo, kata mandazi yako kwa shepu ya pembe tatu au shepu uipendayo.
Vipande vya mandazi kabla ya kutumbukizwa kwenye mafuta. PICHA | MARGARET MAINA
Yaache mandazi yako yaumuke kwa dakika 30.
Weka mafuta kwenye sufuria, yaache yapate moto kiasi kisha weka mandazi yako.
Hakikisha mandazi hayawi mengi ili yaachane na uweze kuyageuza vizuri.
Ili andazi liumuke wakati wa kukaanga, basi fanya kama unalimwagia mafuta juu kwa kutumia kijiko halafu ndipo uligeuze baada ya kuumuka.
Andazi likiiva, litoe kwenye mafuta halafu uweke kwenye chujio kulichuja mafuta. Fanya hivyo hadi mandazi yote unayopika yaive.