PDP: Obado asalia mpweke wawaniaji wakikwepa chama
NA IAN BYRON
GAVANA wa Migori Okoth Obado, anayekabiliwa na kashfa kadha, anajikuna kichwa kuhusu mwelekeo wa kisiasa anaofaa kuchukua, baada ya washirika wake wa karibu kukwepa chama chake cha People Democratic Party (PDP) na kujiunga na vyama vingine kwenye mchujo wa vyama unaoendelea.
Katika mahojiano, gavana huyo anayehudumu muhula wa mwisho , alisisitiza kuwa PDP, chama ambacho alikitumia kuingia ofisini katika muhula wa kwanza, bado kinashiriki katika siasa za eneo hilo linalothibitiwa na chama cha ODM.
Bw Obado alijitenga na ODM na kuanza kuvumisha chama chake katika ngome ya Nyanza ya kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Wakati mmoja alitangaza kuwa angegombea urais kwa tikiti ya chama cha PDP kabla ya kuacha azma hiyo baada ya miezi michache. Alitajwa kuwa fuko aliposhirikiana kwa karibu na Naibu Rais William Ruto na tangu wakati huo, amekuwa pweke na anaonekana kutengwa kisiasa huku washirika wake wa karibu wakijitenga naye wakiwemo wa nyumbani anakotoka North Kanyamkago.
Huku chama chake kikionekana kufifia na kukosa mwaniaji kwenye mchujo unaoendelea, Bw Obado amekuwa akisaka wagombeaji na kuwapa tiketi za moja kwa moja katika maeneo mengine nchini.
“Hakuna wasiwasi wowote kwa kuwa siku ya mwisho ya mchujo haijapita. Bado tuko na wakati wa kuteua wagombeaji katika viti vyote,” Bw Obado alisema Jumapili. Alisisitiza kwamba ingawa hakuna mwaniaji aliyechagua PDP katika kaunti hiyo, maeneo mengine kama Kisii na Nyamira yametoa zaidi ya madiwani 50, wabunge kadhaa na viti vingine ambao tayari wamekabidhiwa vyeti.
Tangu alipojitenga na ODM, gavana huyo amekuwa akikwepa kujiunga na Azimio la Umoja One Kenya au Kenya Kwanza Alliance licha ya hatua yake ya awali ya kuunga azma ya urais ya Dkt Ruto.
“PDP ni chama huru sana. Hatujajiunga na muungano wowote kwa kuwa hatuelewi mielekeo yao ya kisiasa. Tunalinda maslahi ya mwananchi wa kawaida,” alisema.
Anapoendelea kuonekana mpweke kisiasa, kumekuwa na minong’ono kwamba atagombea useneta au kiti cha ubunge cha Uriri.
“Ningali nafikiria hatua ya kisiasa nitakayochukua na nitatoa taarifa nikifanya uamuzi,” alisema.
Alipofikiwa kwa simu kutoa maoni, Bw Obado alisema alikuwa akitulia nyumbani kwake mashambani Rapogi na alitaka kwenda mahali kufanya kazi ya juakali. “Kwa hivyo, nitakubali mahojiano kwa simu,” alisema akionyesha kuwa mwanasiasa aliyetulia wakati joto linaendelea kupanda.
Kimya chake kimezua maswali kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa kwa kuwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Dkt Ruto kimesimamisha wagombeaji 33 wa udiwani kati ya wadi 40 za Migori.
Mshirikishi wa UDA katika kaunti hiyo, Bw Paul Siengo alisema kwamba washirika wa Bw Obado pia wamejiunga na chama hicho wakiwemo waliokuwa mawaziri katika serikali yake Rebecca Maroa ( maji) na Scholarstica Obeiro( Fedha), ambao watagombea ugavana na kiti cha ubunge cha Nyatike mtawalia.