Connect with us

General News

Ruto kusimamia mchujo wa UDA – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Ruto kusimamia mchujo wa UDA – Taifa Leo

Ruto kusimamia mchujo wa UDA

NA ONYANGO K’ONYANGO

BODI ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu Rais William Ruto imeanzisha mchakato wa kujenga imani ya wawaniaji viti mbalimbali kuelekea kura ya mchujo ulioratibiwa kufanyika Aprili 2022.

Ili kuondoa matukio ambapo maafisa fulani huenda wakashawishiwa na baadhi ya wawaniaji, mwenyekiti wa bodi hiyo Anthony Mwaura alisema shughuli zote za kura ya mchujo zitaendeshwa na yeye pamoja na wanachama wengine wa NEB kama vile Salome Beaco, Aurelia Rono, Ummi Bashir, Matika Chacha, Raphael Chimera na Halake Dida.

“Chama cha UDA hakitabuni bodi za uchaguzi katika kaunti kote nchini ili kuzuia uwezekano wa afisa yeyote kushawishiwa,” Bw Mwaura akasema.

Mwenyekiti huyo wa NEB alikariri kuwa Dkt Ruto atasimamia shughuli zote za kura za mchujo za UDA.

“Wanachama wa bodi ya uchaguzi watamjulisha (Ruto) kila mara kuhusu maandalizi ya kura za mchujo. Anafahamu kuwa uthabiti wa chama unategemea jinsi kinavyoendesha kura zake za mchujo na yule anayezisimamia,” akasema Bw Mwaura.

Ili kujenga imani ya wawaniaji kuhusu shughuli hiyo, mwenyekiti huyo wa NEB alifichua kuwa afisi yake imetuma mwaliko kwa wanadiplomasia ili watume waangalizi wakati wa mchujo wa UDA kuanzia Aprili.

“Wiki ijayo tutaandikia maafisa wote wa kidiplomasia tukiwaalika kushiriki katika safari yetu ya kihistoria kwa kuangalia kura zetu za mchujo. Tuna imani kwamba shughuli hiyo itaendeshwa kwa njia huru na haki,” akaambia Taifa Jumapili.

Chama cha UDA pia kinapanga kuchapisha karatasi za uteuzi zenye picha za wawaniaji kwa nyadhifa zote sita. Chama hicho pia kitanunua masanduku yake ya kutumika wakati wa kupiga kura na wala hakitaazima masanduku kutoka kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Tutanunua masanduku yetu, hatutakodisha kutoka kwa IEBC. UDA itakuwa na masanduku ya kuakisi mwangaza. Yenye vifuniko. Karatasi za kura zitakuwa na picha za wawaniaji,” akaeleza Bw Mwaura.

Haya yanajiri wakati ambapo bodi hiyo imefutilia mbali uwezekano wa UDA kuandaa mchujo wa pamoja na vyama tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza (KKA). Vyama hivyo ni chake Musalia Mudavadi (ANC) na chake Moses Wetang’ula (Ford Kenya).

“Hakuna mpango wa kuandaliwa kwa kura ya mchujo ya pamoja katika vyama vya UDA, Ford Kenya,” akasema mwenyekiti huyo wa NEB.

Bw Mwaura alisema kuwa UDA haitaki kurudia makosa ambayo yalitendeka katika mchujo wa chama cha Jubilee ambapo baadhi ya wawaniaji waliokuwa maarufu walipokonywa ushindi.

Ili kufikia lengo hilo, bodi hiyo imekuwa ikiendesha kampeni ya kutoa uhamasisho kwa wawaniaji kuhusu yale ambayo wanapaswa kufanya kabla ya kushiriki katika mchujo ujao.

“Tumekuwa tukiendesha mafunzo kuhusu yale ambayo wawaniaji wanafaa kufanya wanapojiandaa kwa mchujo. Kanuni hizo ni zile ambazo zinafungamana na sheria mpya ya vyama vya kisiasa. Kwa mfano, watakaoshiriki mchujo ni wale ambao wamejiandisha rasmi kuwa wanachama cha UDA,” Bw Mwaura akasema.