Serikali yaimarisha upimaji wa mahindi mipakani
NA STANLEY KIMUGE
KENYA imeimarisha ufuatiliaji katika mipaka yake ili kuhakikisha usalama wa mahindi, huku wakulima kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki wakianza kuuza zao lao kuanzia msimu huu.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukadiriaji Ubora wa Bidhaa Kenya (KEBS) Luteni Kanali Mstaafu Bernard Njiraini, mnamo Jumatatu alisema shirika hilo limeimarisha upimaji katika vituo vya mipakani ili kuhakikisha kwamba mahindi yote kutoka nchi jirani yanatimiza viwango vya ubora.
“Tunachopatia kipaumbele ni kulinda afya na usalama wa watumiaji bidhaa. Katika vituo vya mpakani, tumeweka maabara zetu kupima kuhakikisha na kuthibitisha ubora wa mahindi na bidhaa zingine zote. Tumeimarisha ufuatiliaji, upimaji na tunaweza kuhakikishia Wakenya kwamba mahindi yanayoingizwa nchini yanatimiza viwango vya ubora,”alisema.
Mkuu huyo wa Kebs, aliyesema hayo akiwa mjini Eldoret wakati wa ziara ya eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa akiwa na Bodi ya Taifa ya
Ubora ikiongozwa na mwenyekiti wake Bernard Ngore, alisema kwamba ni lazima nafaka yoyote itimize viwango vya kuvu vinavyoruhusiwa katika soko nchini Kenya.
Alisema kwamba nchi katika eneo hili zimebuni na kuwianisha viwango vyake ili kulinda watumiaji bidhaa katika nchi wanachama.
“Tuko na alama za kutambua ubora na tumewianisha viwango pamoja na nchi jirani. Tuko na maelewano na nchi hizi kwamba bidhaa zinazotoka kwao kuja nchi yetu, zinafaa kukaguliwa, kuidhinishwa na kupatiwa cheti cha kuonyesha zimetimiza viwango vya ubora,” alisema Luteni Kanali Mstaafu Njiraini.
Katika wiki mbili zilizopita, ongezeko la mahindi kutoka nchi wanachama wa EAC limesababisha bei kushuka nchini Kenya kwa Sh400 hadi Sh2800 kwa gunia la kilo 90 ya mahindi.
Mnamo Februari 4, shirika hilo lilizungumza na chama cha kampuni za kusaga unga katika juhudi za kuimarisha ubora wa unga unaouzwa nchini.
Sumu ya kuvu imekuwa tatizo katika sekta ya nafaka. Mwaka jana, shirika hilo liliondoa unga wa mahindi madukani kwa kukosa kutimiza viwango vya matumizi ya binadamu.
Bw Njiraini alihimiza serikali za kaunti kuweka mifumo kama vile kuwa na mitambo ya kisasa ya kukausha nafaka ili kuhakikisha inashughulikiwa vyema. “Tumeona viwango vya unyevu vikisababisha sumu ya kuvu katika mahindi. Tunataka kushauri kaunti kununua mitambo ya kukausha mahindi kuzuia kuvu katika nafaka,” aliongeza.
Naibu Gavana wa Uasin Gishu Daniel Chemno aliomba serikali kuongeza ufuatiliaji ili kuhakikisha ubora wa chakula kinachouzwa katika masoko nchini.
“Tunahofia kwamba baadhi ya wafanyabiashara walaghai wanauza chakula hatari kama vile maziwa, mboga na bidhaa zingine kwa wateja wasio na habari na hii inaweza kusababisha madhara ya afya. Kwa mfano, kuna ripoti kwamba baadhi ya wafanyabiashara na kampuni zinatumia kemikali kwa maziwa yasiharibike jambo ambalo linahatarisha afya za wanaoyatumia,” alisema Chemno.
Next article
NCPB yadumisha bei ya mahindi licha ya zao kujaa kutoka nje