Connect with us

General News

Sierra Leone walazimishia Ivory Coast sare ya 2-2 katika Kundi E – Taifa Leo

Published

on


AFCON: Sierra Leone walazimishia Ivory Coast sare ya 2-2 katika Kundi E

Na MASHIRIKA

SIERRA Leone walisawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili na kulazimishia Ivory Coast sare ya 2-2 katika mchuano wa Kundi E uliowakutanisha jijini Douala kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Cameroon.

Masihara ya kipa Badra Sangare sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa yalimpa fowadi Alhadji Kamara nafasi ya kufungia Sierra Leone bao la pili katika mechi hiyo na hivyo kuvuna sare ya pili mfululizo kwenye Kundi E. Sierra Leone walishuka dimbani wakijivunia motisha ya kulazimishia mabingwa watetezi Algeria sare tasa katika mchuano wa kwanza kundini.

Sierra Leone kwa sasa wanajivunia alama mbili kutokana na mechi mbili huku Ivory Coast wakiwa na pointi nne. Ivory Coast waliotawazwa mabingwa wa AFCON mnamo 2015 baada ya kupiga Ghana kwa penalti 9-8 kwenye fainali nchini Equatoria Guinea, sasa wana kibarua kizito dhidi ya Algeria katika mchuano wa mwisho wa Kundi E mnamo Januari 20, 2022.

Ivory Coast walipoteza penalti mwanzoni mwa kipindi cha kwanza baada ya fowadi Wilfried Zaha kuangushwa ndani ya kijisanduku na nahodha wa Sierra Leone, Umary Bangura, katika dakika ya 12. Hata hivyo, walijiweka kifua mbele kupitia kwa Sebastien Haller kabla ya Musa Noah Kamara kusawazishia Sierra Leone katika dakika ya 55.

Kipa Mohamed Nbalie Kamara wa Sierra Leone alipangua na kudhibiti makombora mazito aliyoelekezewa na wanasoka wa Ivory Coast akiwemo Franck Kessie wa AC Milan na akatawazwa mchezaji bora wa mechi.

Nicolas Pepe wa Arsenal alifungia Ivory Coast bao la pili katika dakika ya 65 kabla ya juhudi zake kufutwa na Kamara mwishoni mwa kipindi cha pili.

Sierra Leone watatandaza mchuano wao wa mwisho wa Kundi E dhidi ya Equatorial Guinea mjini Limbe mnamo Januari 20, 2022 huku Ivory Coast wakipimana ubabe na Algeria waliotandika Senegal 1-0 kwenye fainali ya AFCON 2019 nchini Misri.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGOSource link

Comments

comments

Facebook

Trending