Simanzi tele baada ya kifo cha Tutu, 90
Na PETER DUBE
JOHANNESBURG, Afrika Kusini
ASKOFU Desmond Tutu wa Afrika Kusini amefariki Jumapili akiwa na umri wa miaka 90, rais wa taifa hilo, Cyril Ramaphosa, ametangaza kwenye taarifa.
Tutu, ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobeli, alifariki jijini Cape Town.
Alikuwa kiongozi wa Kanisa la Anglikana akishikilia nyadhifa tofauti.
“Desmond Tutu alikuwa mzalendo wa kuigwa na wengi; kiongozi mwenye msimamo thabiti aliyeonyesha maana halisi ya mafundisho ya Biblia kupitia imani yake,” akasema Rais Ramaphosa, Jumapili asubuhi.
Akaongeza: “Alikuwa kiongozi mwenye ujuzi wa hali ya juu aliotumia kuukabili utawala wa ubaguzi wa rangi. Alikuwa mtetezi wa wanyonge na waliodhulumiwa katika jamii kote duniani.”
Tutu alibuni msemo wa ‘The Rainbow Nation’ (Nchi ya Upinde wa Mvua) kurejelea hali ilivyokuwa nchini humo wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi.Amekuwa akiugua saratani ya kibovu kwa karibu miaka 20.
Tutu alizaliwa katika eneo la Klerksdorp, Transvaal Magharibi, mnamo 1931.
Babake alitoka katika jamii ya Waxhosa huku mamake akiwa mzaliwa wa nchi ya Botswana.
Hata hivyo, wote walizungumza lugha ya Kixhosa.
Inadaiwa Tutu aliamua kuwa kasisi ukubwani mwake alipokutana na Kasisi Trevor Huddlestone alipokuwa na umri wa miaka tisa.
Inaelezwa mazungumzo kati yao yalimfurahisha sana Tutu. Baadaye maishani mwake, Tutu alibaini kwamba, Huddlestone alikuwa mmoja wa wanaharakati waliopinga utawala wa ubaguzi wa rangi.
Sifa na ushawishi wa Tutu kama mpiganiaji haki zilianza kuenea baada ya kuhudumu kama mwalimu katika vyuo vikuu vya Botswana, eSwatini (zamani ikiitwa Swaziland) na Lesotho.
Hilo lilimfanya kuwa mtu wa kwanza mweusi kuhudumu kama askofu wa Lesotho, Johannesburg na Cape Town mtawalia.
Alitumia nafasi hizo kukabiliana na utawala wa ubaguzi wa rangi.
Tutu alianza kupinga ubaguzi dhidi ya watu weusi mnamo 1957, alipojiuzulu kazi ya ualimu akilalamikia kupitishwa kwa sheria iliyobuni mfumo wa chini wa elimu kwa weusi ikilinganishwa na weupe.
Baada ya kumaliza diploma katika Taasisi ya Pretoria Bantu Normal College, alisomea shahada katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini, ambapo alihitimu pamoja na aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, marehemu Robert Mugabe.
Baada ya kuacha ualimu mnamo 1957, Tutu alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Dini cha St Peter’s, Rosettenville, jijini Johannesburg. Kwenye chuo hicho, alisomea masuala ya Kanisa la Anglikana kama historia yake.
Alihitimu kwa shahada ya masuala ya kidini mnamo 1960.
Aliteuliwa kiongozi wa kanisa na baadaye kama kasisi mwaka ulliofuata.
Ili kuboresha ujuzi wake kama kasisi, alijiunga na Chuo cha King’s, jijini London mnamo 1962, alikopata Shahada ya Uzamili katika Masuala ya Dini mnamo 1966.
Akiomboleza kifo chake Jumapili, Kasisi Mzwandile Molo, ambaye ni mwanachama wa Baraza la Makanisa la Afrika Kusini (SACC), alimtaja Tutu kama “shujaa wa haki.”
“Ameishi maisha yake kama mtetezi wa ukweli, amani na maridhiano. Ni hali iliyohitaji ushujaa mwingi na kujitolea kwa njia ya kipekee katika jamii ambapo msingi wake ni ubaguzi, udhalilishaji na ukoloni,” akasema Kasisi Molo kwenye mahojiano.
“Alikuwa ishara ya utetezi wa haki kote duniani. Alifanya hivyo kwa manufaa ya mamilioni ya watu bali si kwa maslahi yake binafsi,” akasema.
Kutokana na juhudi zake, alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobeli mnamo 1984.
Alistaafu kutoka maisha ya umma mnamo 2010.