WANDERI KAMAU: Viongozi wa kidini nchini wamwige Desmond Tutu
Na WANDERI KAMAU
SIFA kuu anayopaswa kuzingatia mwanadamu anapoondoka hapa duniani, ni jinsi alivyowasaidia wanadamu wenzake kuepuka janga fulani.
Ni jambo ambalo wanadamu wengi hugundua wakati siku zao za kuondoka hapa duniani zinapokaribia au wanapokumbwa na mkasa fulani maishani mwao.
Katika vitendo vyao vingi, wanadamu wengi huongozwa na mali watakayopata au watakavyojifaidi wao binafsi na jamaa zao. Huwa hawawajali wengine.
Hata hivyo, hicho ni kinyume cha maisha aliyoishi Askofu Desmond Tutu kutoka Afrika Kusini, aliyefariki Jumapili akiwa na umri wa miaka 90.
Ingawa ni kawaida wanadamu kusifiwa wanapofariki na maovu yao kutotajwa, ni wazi Tutu alikuwa kiongozi wa kidini wa kuigwa.
Hakukosa maovu yake kama mwanadamu, ijapokuwa ni wazi aliishi maisha ya kujinyima na kupigania haki za wanadamu—bila ubaguzi wowote.
Kwanza, Tutu alijitokeza kama mwanaharakati wa kisiasa.
Alikuwa miongoni mwa watu maarufu nchini Afrika Kusini waliojitokeza waziwazi kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi.
Kando na hayo, alikuwa mpiganiaji wa haki za binadamu.
Tutu pia alikuwa mwanamageuzi mkubwa, ambaye harakati zake hazikushuhudiwa tu kanisani.
Mnamo 1985 na 1986, alipohudumu kama askofu wa Kanisa la Kianglikana katika miji ya Johannesburg na Cape Town mtawalia, Tutu alitumia nafasi yake kushinikiza mashauriano na mazungumzo kama njia ya kusuluhisha mizozo iliyokuwa ikiliandama kanisa hilo.
Ni kutokana na juhudi zake ambapo kanisa hilo lilianza kuwatawaza makasisi wanawake.
Baada ya Rais FW de Klerk wa Afrika Kusini kumwachilia uongozi marehemu Nelson Mandela kutoka gerezani mnamo 1990, wawili hao waliongoza mazungumzo ya kumaliza mfumo wa utawala wa ubaguzi wa rangi.
Ni kutokana na mazungumzo hayo ambapo taifa hilo lilianza ukurasa mpya wa kiutawala—Waafrika walianza kuhisi kama ‘wenyeji’ katika nchi yao wenyewe!
Mnamo 1994, Tutu pia aliongoza harakati za kuyapatanisha makundi ya Waafrika walioshiriki kwenye harakati za ukombozi, ambayo hayakuwa na uhusiano mwema.
Upeo wa mchango wake katika kutetea na kupigania maslahi na thamani ya ubinadamu ulikuwa kati ya 1996 na 1998, alipoongoza Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC) nchini humo.
Ingawa Waafrika wengi walihisi Wazungu waliowadhulumu wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi walipaswa ‘kuadhibiwa’, Tutu alishinikiza maridhiano kama njia bora zaidi ya kuondoa makovu ya utawala huo.
Hadi sasa, tume hiyo ndiyo inatajwa kuchangia pakubwa uthabiti wa kisiasa unaoshuhudiwa nchini humo hadi sasa.Bila shaka, ingawa Tutu amekosolewa kwa baadhi ya misimamo yake kama kutetea ndoa za watu wa jinsia moja, ni wazi maisha yake yanafaa kuwa mfano kwa viongozi wengi wa kidini nchini.
Mchango wake haukuwa kwenye dini pekee, bali katika usomi, uandishi, utetezi wa haki za binadamu, uhifadhi wa mazingira kati ya mengine.
Ni maisha yanayopaswa kuwafungua macho viongozi wa kidini nchini, kwamba hawapaswi kukita utendakazi wao makanisani pekee.
Sauti zao zinahitajika pakubwa, hasa wakati huu nchi inapoelekea katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
[email protected]