Connect with us

General News

Uingereza yadai Putin tayari kuivamia Ukraine – Taifa Leo

Published

on


Uingereza yadai Putin tayari kuivamia Ukraine

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

UINGEREZA imeilaumu Urusi kwa kupanga njama za kumweka kibaraka wake kuwa kiongozi wa Ukraine.

Mnamo Jumapili, Wizara ya Mashauri ya Uingereza ilimlaumu Rais Vladimir Putin wa Urusi kwa kuendesha njama hizo kichinichini.

Wizara hiyo ilimtaja mbunge wa zamani nchini Ukraine, Yevhen Murayev, “kusukumwa” na Urusi kuchukua uongozi huo.

Kufikia sasa, Urusi inadaiwa kuwapeleka karibu wanajeshi 100,000 kwenye mpaka wake na Ukraine, ijapokuwa imekuwa ikikanusha madai ya kupanga kulivamia taifa hilo.

Mawaziri kadhaa wa Uingereza wameonya kwamba Urusi itajuta ikiwa kutakuwa na uvamizi wa aina yoyote ile nchini Ukraine.

Kwenye taarifa Jumapili, Waziri wa Mashauri wa Uingereza, Liz Truss alisema: “Habari tunazotoa leo zinahusiana na njama ya Urusi kupanga kuivamia Ukraine na kuweka vibaraka wake kama viongozi wapya. Ni lazima Urusi ipunguze mashambulio yake dhidi ya taifa hilo na kuanza mchakato wa kidiplomasia kurejesha amani.”

Akaongeza: “Msimamo wa Uingereza na washirika wake ni kuwa Urusi itajutia hatua yoyote ya kuivamia Ukraine.”

Mnamo 2014, Urusi ilivamia na kuchukua udhitibi wa eneo la Crimea kutoka kwa Ukraine, baada ya taifa hilo kumng’oa mamlakani Rais Viktor Yanukovych, aliyekuwa mshirika wake wa karibu.

Idara za kijasusi za Ukraine na mataifa ya Magharibi zimekuwa zikieleza kuwa kuna uwezekano Urusi kuivamia nchi hiyo wakati wowote baada ya kuwapeleka majeshi yake kwenye eneo la mpakani.

Hata hivyo, Urusi imekuwa ikikanusha uwepo wa mpango wowote wa uvamizi. Badala yake, Rais Putin amekuwa akitoa masharti kwa nchi za Magharibi, baadhi yakiwa Ukraine kuzuiwa kujiunga na Shirika la Kujihami la Mataifa ya Magharibi (NATO).

Vile vile, anataka shirika hilo kusitisha shughuli zote za kijeshi na kukoma kutuma silaha za vita katika nchi za Ulaya Mashariki. Urusi inafasiri hilo kama tishio kwa usalama wake.

Hata hivyo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Urusi iliilaumu Uingereza kwa “kueneza uwongo.”

Murayev alipoteza kiti chake katika Bunge la Ukraine baada ya chama chake kukosa kupata asilimia tano ya kura kwenye uchaguzi wa 2019.

Kwenye mahojiano na gazeti la ‘Observer’ la Uingereza, alisema Wizara ya Mashauri ya Uingereza “inaonekana kuchanganyikiwa.”

“Taarifa za wizara hiyo ni za kukanganya. Binafsi, nimepigwa marufuku kusafiri Urusi. Kando na hilo, akaunti za moja ya kampuni zangu zimefungwa,” akasema.

Uingereza vile vile imetaja wanasiasa wengine wanne wa Ukraine iliosema wamekuwa wakiwasiliana kwa njia ya siri na idara ya ujasusi ya Urusi.

Ilisema wanasiasa hao wamekuwa wakiwasiliana na idara hiyo kuhusu mpango huo wa uvamizi.

Wanasiasa hao ni Mykola Azarov, aliyehudumu kama waziri mkuu wakati wa uongozi wa Rais Yanukovych.

Baada ya mapinduzi ya rais huyo, Azarov alitorokea Urusi kutafuta hifadhi ya kisiasa.

Wengine ni Volodymyr Sivkovych, Serhiy Arbuzov na Andriy Kluyev. Sivkovych alihudumu kama Naibu Msimamizi Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Ukraine na Baraza la Ulinzi wa Kitaifa.

Arbuzov na Kluyev walihudumu kama manaibu waziri mkuu wakati wa utawala wa Rais Yanukovych.

Kiongozi wa chama cha Labour, Keir Starmer, pia ameirai serikali ya Uingereza kufanya kila iwezalo kuilinda Ukraine dhidi ya “uvamizi wa Urusi.”

Nchi zote wanachama wa NATO zimeapa kuisaidia Ukraine ikiwa Urusi itachukua hatua yoyote ya kuivamia.