Ukosefu wa petroli, dizeli watatiza raia
BENSON MATHEKA NA MARTIN MWAURA
SHUGHULI za uchumi Kenya zinakabiliwa na hatari ya kukwama huku uhaba wa mafuta ukiendelea kushuhudiwa maeneo tofauti nchini.
Uhaba huo ambao ulianza mwishoni mwa wiki jana umezidi wenye magari wakitatizika baada ya kukosa petroli na diseli katika vituo vya kuuzia mafuta.
Uchukuzi mjini Murang’a na maeneo yaliyo karibu ulitatizika kutokana na uhaba wa mafuta. Uchunguzi wa Taifa Jumapili ulibaini kwamba vituo vingi vya mafuta eneo hilo vilifungwa kwa kukosa mafuta.
Ni kituo kimoja ambacho kinamilikiwa na chama cha akiba na mikopo cha matatu cha MTN Sacco, kilichokuwa na mafuta kufikia jana asubuhi.
Katika mji wa Machakos, ni vituo vichache vilivyokuwa na petroli na diseli. Hali ilikuwa sawa katika kaunti ya Kwale, Kericho na Migori.
Wamiliki wa magari ya kibinafsi, madereva wa magari ya uchukuzi na wahudumu wa bodaboda walishtuka kukosa mafuta kwenye vituo huku baadhi wakilazimika kukatiza safari zao.
“Hali ni mbaya sana, nimekatiza safari yangu kwa kukosa mafuta ya kuongeza kwenye gari langu,” akasema Bw Joseph Musila aliyekuwa amepanga kusafiri kutoka Nairobi hadi Machakos.
Madereva wa malori ya uchukuzi wa bidhaa pia wameathiriwa na uhaba wa mafuta jambo ambalo huenda likasababisha uhaba wa bidhaa muhimu katika baadhi ya sehemu nchini.
“ Ikiwa hali hii itaendelea hatutaweza kusafirisha bidhaa,” akasema Bw Sospeter Kariuki, anayenunua mboga na matunda maeneo ya bara na kusafirisha hadi Pwani kuuza.
Bw Kariuki anasema uhaba wa sasa wa mafuta unaumiza wafanya biashara ambao tayari wanakabiliwa na hali ngumu kufuatia bei za juu.
Serikali imehusisha uhaba wa mafuta na bei za juu za bidhaa za mafuta na vita vinavyoendelea Ukraine.
Vituo vichache vilivyokuwa na mafuta nchini haviruhusu madereva kununua ya zaidi ya Sh3000 ili kuwezesha wengi kupata bidhaa hiyo.
Wahudumu wa matatu na bodaboda wametishia kupandisha nauli iwapo uhaba wa mafuta utaendelea kushuhudiwa nchini. “Hali ikiendelea hivi, lazima tutapandisha nauli na abiria ndio wataumia,” alisema mmiliki wa matatu jijini Nairobi Joseph Wairigi.
Peter Mwariri, mfanyabiashara kaunti ya Murang’a alisema wamesimamisha magari yao kwa sababu ya kukosa petroli na diseli.
Wamiliki wa vituo vya mafuta walisema hawajui ni lini uhaba wa mafuta unaokumba nchi utaisha. Haya yanajiri huku madereva na wamiliki wa magari wa kaunti zilizo karibu na nchi jirani wakivuka mipaka kununua bidhaa hiyo.
“Uchumi wa nchi utadorora iwapo serikali haitachukua hatua kuokoa hali,” alisema Bw Mwariri. Wakazi walielezea hofu kwamba uhaba wa sasa wa mafuta utafanya bei kupanda kutoka ya Sh135 kwa lita ya petrol. Tayari baadhi ya vituo vya mafuta kaunti ya Murang’a waliongeza bei hadi Sh150.
Next article
Karua aanza kumpigia debe Raila Kirinyaga