Connect with us

General News

Wakenya waache kasumba ya ‘Mtu Wetu’ uchaguzi ujao – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wakenya waache kasumba ya ‘Mtu Wetu’ uchaguzi ujao – Taifa Leo

PETER NGARE: Wakenya waache kasumba ya ‘Mtu Wetu’ uchaguzi ujao

Na PETER NGARE

MWANASAYANSI maarufu Albert Einstein alisema uendawazimu ni kufanya jambo kwa mbinu moja kila mara huku ukitarajia matokeo tofauti.

Mwaka ujao Wakenya wataenda kwenye Uchaguzi Mkuu kuwachagua wanawake na wanaume watakawaongoza kwa miaka mitano ijayo.Katika kiti cha urais, ambacho ndicho kikuu kinachong’ang’aniwa kisiasa nchini, kumejitokeza vigogo ambao wametawala siasa za Kenya kwa miaka na mikaka.

Viongozi hawa wakiwemo Raila Odinga, William Ruto, Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi wote wamehudumu katika serikali tofauti wakishikilia vyeo vikubwa vikubwa.Bw Odinga ashawahi kuwa waziri mkuu na waziri katika serikali za Daniel Moi na Mwai Kibaki, ilihali wenzake Ruto, Mudavadi na Musyoka wamehudumu katika cheo cha makamu wa rais na pia mawaziri.

Nchi ya Kenya kwa sasa inakabiliwa na matatizo tele hasa umaskini. Mamilioni ya vijana hawana ajira, familia nyingi zinalala njaa, huduma za matibabu ni duni, gharama ya maisha inapanda kila uchao na sekta muhimu kama vile kilimo zimo katika hali mbaya.

Kwa kiasi kikubwa, matatizo yanayokumba Kenya kwa sasa ni matokeo ya yale ambayo viongozi wa Kenya, wakiwemo vigogo wanaotaka kuwa marais mwaka ujao, walifanya ama walikosa kufanya walipokuwa madarakani.

Kwa mfano, uhaba wa ajira kwa vijana ni matunda ya viongozi kukosa kuweka mikakati ya kukuza viwanda vya humu nchini.Viongozi hawa walikosa kulinda wawekezaji dhidi ya ada za juu za stima na ushuru,

jambo ambalo limesaidia kulemaza viwanda ambavyo vingesaidia kubuni nafasi zaidi za kazi.Viongozi hao pia wamekosa kulinda wakulima wa humu nchini, ndiposa mahindi, mayai na maziwa kutoka Uganda yanauzwa kwa bei nafuu kuliko ya wakulima wa hapa Kenya.

Viongozi hawa pia hawawezi kuepuka lawama za kuwa sehemu ya ufisadi ambao unatishia kuporomosha taifa hili kiuchumi na kijamii, kwani hawakufanya ya kutosha kuzima uhalifu huu wa jinai.Ni Dhahiri kuwa vigogo hawa ambao sasa wanajinadi kuwa wenye suluhisho kwa matatizo waliyosaidia kubuni hawana jipya la kuwapa Wakenya iwe ni “Bottom Up”, mapeni kidogo kwa maskini kila mwezi ama kuahidi kupunguza ushuru kwa asilimia 50.

Hii ni “danganya toto” wanazorushia wananchi jinsi mvuvi anavyorushia samaki ndoano ili kumnasa na kumla.Lakini cha kushangaza ni kuwa Wakenya, kama ilivyo kawaida yao tangu jadi, wameduwazwa na kundi hili ndogo la “wale wale” ambao wamekuwa wakiwaongoza bila kufanya chochote cha kuboresha maisha ya mwananchi.

Kushabikia kundi hili la wanasiasa ndio Einstein alisema ni kutumia mbinu ile ile huku ukitarajia matokeo tofauti.Hivyo basi, kama Wakenya wanataka uongozi ambao utabadilisha maisha yao kuwa bora na ya kuheshimika, sharti waache kuchagua viongozi wale wale ambao walishindwa zamani wakitarajia kuwa wakati huu watabadilika na kuwa wa msaada kwao.

Wapiga kura wanapasa kujifunza kutokana na historia na kuacha kasumba ya “mtu wetu” wakidhani kuwa atawafaa kwa chochote, hata kama wanajua walipompa fursa katika chaguzi za mbeleni hakusaidia kuwakwamua kutokana na umaskini na shida zingine zinazowakabili.

[email protected]